Hadithi za Maandiko
Miujiza wakati wa Safari ya Paulo kwenda Rumi—Bwana anambariki mtumishi Wake


Matendo ya Mitume 21–22; 26–28

Miujiza wakati wa Safari ya Paulo kwenda Rumi

Bwana anambariki mtumishi Wake

Paulo anakamatwa Yerusalemu.

Roho alimwambia Paulo aende Yerusalemu. Watu wengi huko hawakupenda kile Paulo alichofundisha kuhusu Yesu Kristo. Walimkamata na kumfunga kwa minyororo. Paulo alimwambia kila mtu kuhusu wakati alipoona mwanga kutoka mbinguni, alipoisikia sauti ya Yesu, na akabatizwa.

Matendo ya Mitume 21:4, 12–13, 27–40; 22:1–16

Yesu anamtokea Paulo gerezani.

Paulo aliwekwa gerezani. Alipokuwa huko, Yesu alitokea na kusema, “Uwe na moyo mkuu, Paulo.” Alisema kwamba Paulo angemtolea ushuhuda huko Rumi.

Matendo ya Mitume 23:10–11

Paulo anashuhudia juu ya Yesu Kristo

Paulo aliletwa mbele ya magavana na mfalme. Kwa ujasiri alishuhudia juu ya Yesu Kristo kwa hawa watawala wenye nguvu. Alitaka kila mtu kuamini katika Kristo.

Matendo ya Mitume 24:10–27; 25:6–8, 17–19; 26:1–29

Paulo anawaambia wafanyakazi wa merikebu kusubiri mpaka hali ya hewa itakapokuwa nzuri zaidi.

Mfalme alimpeleka Paulo huko Rumi ili kuhukumiwa na Kaisari, mfalme. Paulo alisafiri kwa merikebu pamoja na wafungwa wengine, wakipumzika njiani. Katika kituo kimoja, Paulo alijua kwamba punde ingekuwa majira ya baridi. Kama wangeendelea kwenda, wangekuwa katika hatari kubwa. Aliwaambia wafanyakazi wa ile merikebu kusubiri hadi hali ya hewa itakapokuwa nzuri zaidi.

Matendo ya Mitume 27:1–10

Merikebu inakumbwa na dhoruba.

Hakuna aliyemwamini Paulo, hivyo waliendelea kusafiri. Dhoruba kubwa ilikuja, na merikebu ilisukwa sukwa na mawimbi kwa siku nyingi. Hawakuweza kuona jua au nyota. Walidhani kuwa watakufa baharini.

Matendo ya Mitume 27:11–20

Malaika anamtokea Paulo kwenye merikebu.

Usiku mmoja, malaika wa Mungu alimtembelea Paulo na kusema, “Usiogope, Paulo.” Malaika alisema kwamba Paulo angeweza kufika Rumi, kama Bwana alivyoahidi. Alisema kwamba Mungu angemlinda kila mtu kwenye merikebu—hakuna hata mmoja wao atakayekufa.

Matendo ya Mitume 27:23–24

Paulo anawaambia watu kwenye merikebu kuhusu malaika.

Paulo alimwambia kila mtu kile ambacho yule malaika alikisema. “Iweni na moyo mkuu,” Paulo alisema, “kwani ninamwamini Mungu.”

Matendo ya Mitume 27:21–25

Paulo na wengine katika kisiwa kinachoitwa Melita.

Siku kadhaa baadaye, merikebu ilivunjika na kuzama. Lakini kama vile malaika alivyoahidi, hakuna mtu kwenye merikebu ile aliyekufa. Wote waliogelea hadi kwenye kisiwa kilichoitwa Melita.

Matendo ya Mitume 27: 40–44; 28:1–31

Watu wa Melita wanamsaidia Paulo na wengine.

Watu walioishi huko Melita walikuwa wakarimu kwa Paulo na wengine waliotoka kwenye merikebu. Walikoka moto ili kwamba kila mtu aweze kupata joto.

Matendo ya Mitume 28:2

Nyoka anamuuma Paulo, lakini hakuumia.

Ghafla, nyoka alitoka motoni na kumuuma Paulo mkononi. Lakini Paulo hakuumia. Yeye alitikisa tu mkono kumwondoa yule nyoka. Watu walishangazwa!

Matendo ya Mitume 28:3-6

Paulo anatoa baraka kwa baba yake Publio.

Mtu aliyeitwa Publio alimruhusu Paulo akae nyumbani kwake. Baba yake Publio alikuwa mgonjwa sana. Paulo aliweka mikono yake juu ya yule mtu na kutumia nguvu za Mungu kumponya.

Matendo ya Mitume 28:7–8

Paulo akiwasili Rumi.

Paulo alitumia miezi mitatu akiwa Melita. Bwana alimsaidia kufanya miujiza mingi, kuwabariki na kuwaponya watu ambao walikuwa wagonjwa. Kisha, kama vile Bwana alivyoahidi, Paulo alisafiri kwenda Rumi.

Matendo ya Mitume 28:9–16

Paulo akifundisha kuhusu injili akiwa mfungwa.

Paulo bado alikuwa mfungwa wakati alipokuwa Rumi. Lakini walinzi wake waliruhusu watu kumtembelea. Paulo alifundisha kuhusu Yesu Kristo kwa yeyote ambaye angesikiliza. Aliandika pia barua kwa waumini wa Kanisa katika sehemu nyingi. Baadhi ya barua hizi, nyaraka, ziko katika Agano Jipya.

Matendo ya Mitume 28:16–31