Hadithi za Maandiko
Yesu katika Birika la Bethzatha—Anamponya mtu aliyekuwa ameugua kwa muda mrefu


Yohana 5:1–17

Yesu Kristo katika Birika la Bethzatha

Anamponya mtu aliyekuwa mgonjwa kwa muda mrefu

Watu wakiwa wamekusanyika kwenye Birika la Bethzatha.

Huko Yerusalemu, palikuwa na mahali palipoitwa Birika la Bethzatha. Watu waliamini kwamba birika hili lilikuwa na nguvu za uponyaji. Watu wengi ambao walikuwa wagonjwa, vipofu, au hawawezi kutembea walikuja kwenye birika hili.

Yohana 5:2–3

Watu wakiingia ndani ya maji ili kuponywa.

Watu waliamini kwamba, wakati fulani, malaika alishuka chini na kuyatibua maji ya birika. Mtu wa kwanza kuingia ndani ya maji baada ya kutibuliwa angeponywa ugonjwa wowote waliokuwa nao. Watu wengi walijaribu kuwa wa kwanza kuingia katika birika.

Yohana 5:4

Mtu mgonjwa akiwa amelala karibu na birika.

Mmoja wa watu kwenye birika alikuwa mtu ambaye hakuweza kutembea. Alikuwa ameugua kwa miaka 38. Alitaka kuingia ndani ya birika ili kuponywa, lakini wakati wowote alipojaribu, mtu mwingine aliingia kwanza.

Yohana 5:5–7

Yesu anamwona mtu huyu mgonjwa.

Siku moja ya Sabato, Yesu alikuwa Yerusalemu. Yeye alipokuwa akitembea katika mji, alikuja kwenye Birika la Bethzatha na kumwona mtu amelala pale.

Yohana 5:6

Yesu anamuuliza mtu yule kama anataka kuponywa.

Yesu alijua kwamba mtu yule alikuwa mgonjwa kwa muda mrefu sana na hakuweza kutembea. Yesu alimwuliza kama alitaka kuponywa.

Yohana 5:6

Mtu yule anamwambia Yesu kwamba hakuna mtu wa kumsaidia.

Mtu yule alimwambia Yesu kwamba hakukuwa na mtu wa kumsaidia kuingia birikani, na wakati maji yalipotibuliwa, wengine daima wangeingia mbele yake.

Yohana 5:7

Yesu anamponya mtu yule.

Yesu alimwambia mtu yule, “Simama, jitwike godoro lako, na uende.” Mara moja, mtu yule aliponywa! Kisha alisimama na kuchukua godoro lake. Kwa mara ya kwanza katika miaka 38, angeweza kutembea!

Yohana 5:8–9

Viongozi wanamuuliza mtu yule kwa nini anafanya kazi siku ya Sabato.

Viongozi wa Wayahudi walimwona mtu aliyekuwa amejitwika godoro lake. Walisema kwamba hakuwa akiiheshimu siku ya Sabato, kwa sababu walidhani kwamba kujitwika godoro ilikuwa kama kufanya kazi. Mtu yule alieleza kwamba alikuwa ameponywa punde tu, na mtu aliyemponya alimwambia ajitwike godoro lake.

Yohana 5:10–11

Viongozi wanamkasirikia Yesu kwa kuponya siku ya Sabato.

Viongozi waligundua kwamba ni Yesu aliyemponya mtu yule na kumwambia ajitwike godoro lake siku ya Sabato. Walimkasirikia Yesu na walitaka kumuua. Yesu aliwaambia Yeye alikuwa anafanya tu mambo ambayo Baba Yake wa Mbinguni alikuwa amemfundisha kuyafanya.

Yohana 5:15–17