Hadithi za Maandiko
Fumbo la Wanawali Kumi—Kuwa tayari kwa ajili ya Yesu kuja tena


Mathayo 25:1–13

Fumbo la Wanawali Kumi

Kuwa tayari kwa ajili ya Yesu kuja tena

Wanafunzi wa Yesu wanamwuliza Yeye atarudi lini.

Wanafunzi wa Yesu walijua kwamba siku moja, baada ya Yeye kurudi kwa Baba Yake, Yesu angerudi duniani. Walimwuliza jinsi ambavyo wangejua wakati Yeye atakaporudi. Walitaka kuwa tayari kwa ajili Yake. Ili kuwajibu, Yesu aliwambia fumbo.

Mathayo 24–3

Wanawake kumi wanakwenda kwenye harusi.

Katika fumbo, wanawake kumi walikuwa wanakwenda kwenye harusi. Harusi ilikuwa usiku, hivyo wanawake walilazimika kuchukua taa zilizojaa mafuta ili ziangaze njia yao. Watano kati ya wanawake hao walikuwa na busara na walileta mafuta mengi. Wale watano wengine walikuwa wapumbavu na hawakuleta mafuta ya kutosha.

Mathayo 25:1–4

Wanawake wanalala wakati wakimsubiria bwana harusi.

Wanawake walilazimika kumsubiria bwana harusi na kundi lake la harusi kuja. Lakini bwana harusi alichukua muda mrefu. Wakati wakisubiri, wote walilala.

Mathayo 24–5

Mtu anasema kwamba bwana harusi hatimaye anakuja.

Usiku wa manane, mtu alisema kwa sauti kwamba bwana harusi hatimaye alikuwa anakuja! Ilikuwa ni wakati wa wanawake kujiunga naye katika sherehe ya harusi.

Mathayo 25:6

Wanawake watano wanaweza kuwasha taa zao. Wanawake wengine watano hawana mafuta yoyote.

Wanawake wote waliinua taa zao ili kuangaza njia yao. Lakini wanawake watano ambao hawakuleta mafuta ya kutosha hawakuwa na mwanga wowote. Mafuta yao yalikuwa yametumika wakati walipokuwa wakimsubiria bwana harusi.

Mathayo 25:7–8

Wanawake wasiokuwa na mafuta wanaenda kununua zaidi.

Wanawake watano wasiokuwa na mafuta waliwaomba wengine kuwagawiya yao. Lakini hakukuwa na mafuta ya kutosha ya kugawana. Wanawake watano wasiokuwa na mafuta haraka walikwenda kununua zaidi.

Mathayo 25:8–9

Bwana harusi anawasili na kuzungumza na wanawake watano ambao wako tayari.

Walipokuwa wameenda, bwana harusi akaja! Wanawake watano waliokuwa tayari walikwenda naye kwenye harusi hiyo.

Mathayo 25:10

Wanawake waliokwenda kununua mafuta hawakuweza kuingia kwenye harusi.

Wakati wanawake wengine waliporudi, mlango ulikuwa umefungwa. Waligonga mlango na kuomba bwana harusi awaruhusu waingie ndani. Lakini walikuwa wamechelewa sana. Hawangeweza kuingia kwenye harusi.

Mathayo 25:11–12

Yesu anawafundisha wafuasi Wake kuwa tayari wakati Yeye anaporudi.

Yesu ni kama bwana harusi katika fumbo. Hakuna ajuaye wakati Yeye atakapokuja tena. Ni Baba wa Mbinguni pekee anajua hilo. Kwa hivyo Yesu aliwaambia wafuasi Wake wawe tayari kama wanawake watano ambao walikuwa na mafuta ya kutosha. Watu wanaotii amri za Bwana na kumfuata Roho watakuwa tayari wakati Yesu Kristo atakapokuja tena.

Mathayo 24:36; 25:13; Mafundisho na Maagano 45:56–57