Matendo ya Mitume 10
Kornelio na Marafiki Zake Wanampokea Roho Mtakatifu
Injili ni kwa ajili ya kila mtu
Kornelio alikuwa kiongozi wa askari wa Kirumi. Yeye na familia yake walimwamini Mungu, lakini hawakuwa Wayahudi na hawakujua kuhusu Yesu Kristo. Kornelio alishiriki kile alichokuwa nacho na maskini na kumwomba Mungu mara kwa mara.
Matendo ya Mitume 10:1–2
Alasiri moja, malaika alimjia Kornelio alipokuwa akifunga na kusali. Malaika alisema, “Kornelio, sala yako imesikika.” Mungu alikuwa ameona ukarimu wake. Malaika alimwambia Kornelio amtafute Mtume Petro, ambaye alikuwa anakaa katika mji ulioitwa Yafa. Petro angemwambia Kornelio nini cha kufanya.
Matendo ya Mitume 10:3-6, 30–32
Kornelio aliwaambia watumishi wake kile ambacho malaika alisema. Aliwatuma kwenda Yafa kumwomba Petro aje kumtembelea.
Matendo ya Mitume 10:7–8
Huko Yafa, Petro alikuwa juu ya paa la nyumba akisali. Alikuwa na njaa na alikuwa karibu kwenda kula, wakati ghafla alipoona ono.
Matendo ya Mitume 10:9–10
Petro aliona nguo kubwa ikishuka kutoka mbinguni, ikiwa imejaa kila aina ya wanyama na ndege. Kisha Petro akasikia sauti ikisema alipaswa kula wanyama hao. Lakini hawa walikuwa wanyama ambao Wayahudi hawakuruhusiwa kuwala. Sheria ya Musa ilisema walikuwa najisi. Petro hakutaka kuwala.
Matendo ya Mitume 10:11–14
Sauti ilisema kwamba kama Mungu amefanya kitu kuwa safi, hakipaswi kuitwa najisi. Ono lilirudia mara tatu. Petro alijiuliza ono lile lilimaanisha nini.
Matendo ya Mitume 10:15–17
Hapo ndipo, Roho alimwambia Petro kwamba watu watatu walikuwa wanamtafuta. “Nenda pamoja nao,” Roho alisema, “kwani nimewatuma.”
Matendo ya Mitume 10:16–21
Watu hao watatu walikuwa watumishi wa Kornelio. Walimwambia Petro kuhusu malaika ambaye Kornelio alikuwa amemwona na kuuliza kama Petro angekuja kumfundisha. Wayahudi kwa kawaida hawakuingia katika nyumba za watu ambao hawakuwa Wayahudi, na Mitume hawakuwafundisha injili. Lakini akikumbuka ono lake, Petro aliamua kwenda.
Matendo ya Mitume 10:22, 28.
Wakati Petro alipowasili, Kornelio alikuwa akimsubiri pamoja na marafiki wengi na wanafamilia. Alimwambia Petro kuwa walikuwa tayari kusikia chochote ambacho Mungu alikuwa amemwamuru awaambie.
Matendo ya Mitume 10:26, 33.
Sasa Petro alielewa kitu ambacho Mungu alikuwa anamfundisha katika lile ono. Petro alimwambia kila mtu kwamba Mungu hapendelei taifa moja au kundi la watu zaidi ya lingine. Mungu humkubali mtu yeyote ambaye anamfuata Yeye na mwenye kutenda yaliyo mema. Petro aliwafundisha Kornelio na familia yake na marafiki zake kuhusu Yesu Kristo.
Matendo ya Mitume 10:34–43
Alipokuwa akifundisha, Roho Mtakatifu alimjia kila mtu aliyekuwa anasikiliza. Petro aliwaalika kubatizwa katika jina la Yesu Kristo. Petro alikuwa amejifunza kwamba watoto wote wa Mungu wanakaribishwa katika Kanisa la Yesu Kristo. Injili ya Yesu Kristo ilihubiriwa kwa kila mtu.
Matendo ya Mitume 10:44–48