Mathayo 27; Luka 23; Yohana 19
Yesu Anautoa Uhai Wake Kwa ajili Yetu
Dhabihu ya kutuokoa kutokana na dhambi na mauti.
Baada ya Pilato kuamua kwamba Yesu alipaswa kusulubiwa, aliwaambia askari wake wamwondoe Yesu. Walimchapa, wakamtemea mate, wakaweka taji la miiba juu ya kichwa Chake, na kumdhihaki.
Marko 15:15–20
Askari walimfanya Yesu abebe msalaba mzito wa mbao. Walimpeleka mahali pa nje ya Yerusalemu palipoitwa Golgotha.
Yohana 19:17
Askari walipigilia misumari kwenye mikono na miguu ya Yesu msalabani. Yesu alimwomba Baba Yake wa Mbinguni awasamehe askari, kwa sababu hawakujua walikuwa wakimsulubisha Mwana wa Mungu.
Luka 23:33–34; ona pia Tafsiri ya Joseph Smith katika tanbihi 34c
Wahalifu wawili walisulubiwa pamoja na Yesu siku hiyo. Mmoja wao alimwambia, “Ikiwa wewe ni Kristo, jiokoe wewe mwenyewe na sisi.”
Luka 23:39
Mhalifu mwingine alisema wao walistahili adhabu yao, lakini Yesu hakuwa amefanya kosa lolote. Alimwomba Yesu amkumbuke katika ufalme Wake. Yesu alimwambia kwamba punde wangekuwa pamoja katika ulimwengu wa roho.
Luka 23:40–43
Wanawake wengi waliomfuata Yesu Kristo walikuwa wamekuja msalabani kuwa pamoja Naye. Mmoja wa wanawake hao alikuwa Mariamu, mama yake Yesu. Yesu alimwona na kumwambia Yohana, mmoja wa Mitume Wake, kuwa amtunze.
Yohana 19:25–27; ona pia Luka 8:1–3; Marko 15:40–41.
Kwa saa tatu, giza liliifunika nchi. Yesu alijisikia mpweke sana. Alihisi kama Baba Yake wa Mbinguni alikuwa amemwacha.
Mathayo 27:45–46
Hatimaye, Yesu alijua kwamba alikuwa amekamilisha mateso Yake. Alisema, “Baba, imekwisha, mapenzi yako yametimia.” Kisha Yesu akainamisha kichwa Chake na kukata roho. Ili kuona kama kweli alikuwa amekufa, askari alimchoma ubavuni kwa mkuki.
Tafsiri ya Joseph Smith, Mathayo 27:54 (katika Mathayo 27:50, tanbihi a); Yohana 19:28–30, 34.
Wakati Yesu alipokufa, dunia ilitetemeka. Miamba ilivunjika vipande vipande. Pazia la hekalu, pazia linalofunika mahali patakatifu zaidi hekaluni, likapasuka vipande viwili.
Mathayo 27:51
Askari waliogopa. “Hakika huyu alikuwa Mwana wa Mungu,” walisema.
Mathayo 27:54
Wanafunzi wa Yesu waliuzonga zonga mwili Wake katika sanda ya kitani safi na kumweka kaburini katika bustani. Baadaye, walivingirisha jiwe kubwa mbele ya mlango wa kaburi.
Mathayo 27:57–61; Yohana 19:38–41