Luka 2; Mathayo 2:1–15
Mwokozi Anazaliwa
Ahadi ya Mungu inatimizwa
Yusufu na Mariamu waliishi Nazareti. Mariamu alikuwa punde anakaribia kupata mtoto. Kila mtu ilibidi aende kwenye mji wao wa nyumbani ili kuandikishwa. Hii ilimaanisha kwamba Yusufu na Mariamu walitakiwa kwenda Bethlehemu, mji wa Yusufu. Iliwabidi wasafiri safari ndefu kufika huko.
Luka 2:1–5
Safari haikuwa rahisi kwa Mariamu. Kwa sababu watu wengi walikuwa wamekuja Bethlehemu, Mariamu na Yusufu hawangeweza kupata mahali pa Mariamu kujifungua mtoto wake.
Luka 2:6–7
Walipata mahali ambapo wanyama kwa kawaida waliwekwa. Katika sehemu hii ya unyenyekevu, Yesu alizaliwa. Mariamu na Yusufu walimpenda na kumtunza mtoto Yesu. Walimfunika Yeye kwa nguo ili kumsaidia kuwa na joto na faraja. Walimlaza kulala horini, ambapo kwa kawaida lilikuwa likitumika kuwalisha wanyama.
Luka 2:6–7
Katika eneo la karibu, wachungaji walikuwa wakiwalinda kondoo wao wakati wa usiku. Ghafla, mwanga mkali uliangaza kote kuwazunguka, na malaika akatokea. Wachungaji waliogopa.
Malaika aliwaambia wasiogope, kwa sababu alikuwa na habari njema! Mwokozi alikuwa amezaliwa Bethlehemu, na wangeweza kumkuta amelala horini. Kisha malaika zaidi walikuja, wakisema, “Atukuzwe Mungu juu mbinguni, na duniani iwe amani kwa watu aliowaridhia.”
Luka 2:10–15
Wachungaji waliharakisha kwenda Bethlehemu na kumpata mtoto Yesu, kama vile malaika alivyosema. Waliwaambia watu kuhusu mambo ya kupendeza waliyokuwa wameyaona na kusikia. Walijua Yesu alikuwa mtoto maalum.
Luka 2:16–17
Mariamu na Yusufu walimpeleka mtoto Yesu hekaluni ili kumkabidhi Yeye kwa Mungu. Hapo walikutana na mtu mmoja aliyeitwa Simeoni. Roho Mtakatifu alikuwa amemwambia Simeoni kwamba angekuja kukutana na Mwokozi kabla ya yeye kufa. Alimbeba mtoto na kusema Yesu angewaokoa watoto wote wa Mungu. Yusufu na Mariamu walistaajabishwa na yale aliyoyasema.
Luka 2:22–35
Hekaluni kulikuwa na mtu mwingine aliyeitwa Anna. Mume wake alikuwa amefariki miaka mingi iliyopita. Sasa Anna alitumia muda wake wote kumwabudu Mungu hekaluni. Alimshukuru Mungu kwa nafasi ya kukutana na Mwokozi. Wakati wowote alipokutana na mtu aliyekuwa akimsubiri Mwokozi, aliwaambia kuhusu Yesu.
Luka 2:36–38
Wakati Yesu alipozaliwa, mamajusi katika nchi nyingine waliiona nyota mpya. Walijua ilimaanisha kwamba mtoto maalum alizaliwa ambaye angekuwa Mwana wa Mungu na Mwokozi wa ulimwengu. Walianza safari ndefu kumtembelea mtoto huyu na kumwabudu Yeye. Walitaka kumletea Yeye zawadi ili kuonyesha upendo wao Kwake.
Mathayo 2:1–7; ona Tafsiri ya Joseph Smith katika maelezo, 2a
Baada ya kusafiri kwa muda mrefu, mamajusi walikuja Yerusalemu. Walisema kwamba mfalme mpya wa Wayahudi, Mwokozi, alikuwa amezaliwa, na walikuwa wamekuja kumsujudia. Waliuliza wapi wangeweza kumpata mfalme mpya.
Mathayo 2:1–2
Mfalme aliyeitwa Herode alisikia kwamba mamajusi walikuwa wanamtafuta mfalme mpya. Alikuwa na wasiwasi. Makuhani wake na waandishi walimwambia kwamba maandiko yalisema mfalme mpya angezaliwa Bethlehemu. Herode aliwaambia mamajusi watafute katika Bethlehemu na kisha warudi na kumwambia watakapompata mfalme mpya.
Mathayo 2:3–8
Mamajusi walikuja Bethlehemu. Waliifuata nyota, ambayo iliwaongoza kwa Yesu. Walipompata Yeye na Mariamu na Yusufu, walimpa Yesu zawadi tatu maalum na kumsujudia. Mungu aliwaonya wasirudi kwa Herode, hivyo walienda nyumbani kwa njia nyingine.
Mathayo 2:9–12
Baada ya mamajusi kuondoka, Yusufu alipata ndoto. Katika ndoto, malaika alimwambia Yusufu kwamba Herode alikasirika. Yusufu alihitaji kuwapeleka Mariamu na Yesu hadi Misri ili kuwaweka salama.
Mathayo 2:13
Yusufu aliamka mara moja. Aliondoka kwenda Misri pamoja na Mariamu na Yesu wakati bado ni usiku.
Mathayo 2:14
Mariamu, Yusufu, na Yesu walikaa Misri mpaka malaika alipowaambia kwamba Herode alikuwa amekufa na ilikuwa salama kurudi. Kisha walirudi na kuishi katika Nazareti.
Mathayo 2:15, 19–23