Yohana 8:1–11
Watu Wanataka Kumwadhibu Mwanamke Aliyetenda Dhambi
“Enenda zako, wala usitende dhambi tena”
Mapema asubuhi moja, Yesu Kristo alikwenda hekaluni huko Yerusalemu. Watu wengi walikusanyika kumzunguka Yeye ili kumsikiliza Yeye akifundisha.
Yohana 8:1–2
Wakati Yesu alipokuwa akifundisha, baadhi ya viongozi wa Kiyahudi walimleta mwanamke kwa Yesu. Alikuwa amekamatwa akivunja moja ya amri za Mungu. Kulingana na sheria, mwanamke huyo alipaswa kuuawa na watu kwa kutupiwa mawe.
Yohana 8:3–5
Wanaume walimwuliza Yesu nini kinapaswa kutokea kwake. Walikuwa wakitumia hila ili kumjaribu Yesu. Walijua kwamba Yeye asingetaka mwanamke adhurike. Lakini kama Yesu angesema mwanamke huyu hapaswi kuadhibiwa, basi wangeweza kusema kwamba Yeye hakuwa anatii sheria.
Yohana 8:6
Lakini Yesu hakuwajibu wao. Aliinama chini na kuandika kwenye mchanga. Wanaume wale walimwuliza tena kile wanachopaswa kufanya.
Yohana 8:6–7
Hatimaye, Yesu alisimama na kuwatazama wale wanaume. Yeye alisema kwamba kama ye yote kati yao hajawahi kutenda dhambi, angeweza kuwa wa kwanza kumtupia jiwe.
Yohana 8:7
Kisha Yesu akainama tena na kuendelea kuandika kwenye mchanga. Watu wote walijua kwamba walikuwa na dhambi pia. Mmoja mmoja, waliondoka.
Yohana 8:8–9
Yesu alitazama kote na kumwona yule mwanamke tu amesimama pale. Yeye alimuuliza je, wameenda wapi wale watu wote waliotaka kumwadhibu. Alimwambia wote walikuwa wameondoka. Yesu alimwambia mwanamke, “Enenda zako, wala usitende dhambi tena.” Tangu wakati huo na kuendelea, mwanamke yule alimwamini Yesu.
Yohana 8:9–11; Tafsiri ya Joseph Smith, Yohana 8:11; katika Yohana 8:11, tanbihi c.