Matendo ya Mitume 9:1–31
Yesu Anamtokea Sauli
Mwaliko wa kutubu na kumfuata Bwana
Sauli alikuwa Mfarisayo—kiongozi wa Wayahudi ambaye aliyajua maandiko vizuri. Lakini Sauli hakuamini kwamba Yesu alikuwa ndiye Mwokozi. Mara nyingi aliwaweka wafuasi wa Yesu gerezani. Siku moja Sauli alisafiri kwenda mji ulioitwa Dameski kuwakamata baadhi ya wafuasi wa Yesu na kuwapeleka Yerusalemu kuadhibiwa.
Matendo ya Mitume 9:1–2; 22:4–5; 26:5
Sauli alipokuwa akisafiri, ghafla nuru ikamwangazia. Ilikuwa angavu kuliko jua. Sauli alianguka chini. Alisikia sauti ikisema, “Sauli, Sauli.” Kisha sauti ikamuuliza Sauli kwa nini alikuwa anapigana dhidi ya Yesu na kuwaumiza wanafunzi Wake.
Matendo ya Mitume 9: 3–4; 26:13–14
Sauli aliuliza nani alikuwa akizungumza. Sauti ikasema, “Mimi ndimi Yesu.” Sauli aliogopa na kushangaa. Alimuuliza Yesu kile alichopaswa kufanya. Yesu alimwambia Sauli, “Simama, na uingie mjini.” Huko angejifunza kile alichopaswa kufanya baada ya hapo.
Matendo ya Mitume 9:5–6
Sauli alitii na kusimama. Lakini alikuwa kipofu sasa. Hakuweza kuona kitu chochote. Watu waliosafiri pamoja naye walimwongoza kwenda mji wa Dameski. Kwa siku tatu, Sauli hakula wala kunywa chochote.
Matendo ya Mitume 9:8–9
Mmoja wa wanafunzi wa Yesu aliyeishi Dameski alikuwa Anania. Yesu alimtembelea Anania katika ono na kumwambia aende kumsaidia Sauli.
Matendo ya Mitume 9:10–12
Lakini Anania alikanganyikiwa. Alikuwa amesikia juu ya Sauli. Alijua ni kiasi gani Sauli alikuwa amepigana dhidi ya wanafunzi wa Yesu.
Matendo ya Mitume 9:13–14
Yesu alimwomba Anania amsaidie Sauli licha ya hilo. Yesu alisema kwamba alikuwa amemchagua Sauli kuipeleka injili Yake kwa watu wengi ambao hawakuwa Wayahudi na hawakujua kumhusu Yeye.
Matendo ya Mitume 9:15–16
Anania alimtii Yesu. Alimpata Sauli na kumpatia baraka. Anania alimwita “Ndugu Sauli.”
Matendo ya Mitume 9:17
Anania alisema kwamba Yesu alikuwa amemtuma ili Sauli aweze kuponywa na kujazwa na Roho Mtakatifu. Pale pale, Sauli aliweza kuona tena.
Matendo ya Mitume 9:17–18
Sauli alibatizwa. Kisha alimfundisha kila mtu katika mji huo kuhusu Yesu Kristo. Watu walishangaa kwamba Sauli alikuwa amebadilika sana. Kwa maisha yake yote yaliyosalia, Sauli aliitwa Paulo. Aliwafundisha watu wote, Wayahudi na wengine wengi, kumwamini Yesu. Paulo akawa Mtume wa Yesu Kristo.
Matendo ya Mitume 9:18–22, 29–31; 13:9