Matendo ya Mitume 1–4
Mitume wa Yesu Wanaliongoza Kanisa Lake
Kufundisha, kubatiza, kuponya, na kushiriki kila kitu
Baada ya Yesu kurudi kwa Baba Yake wa Mbinguni, Mitume ndiyo waliokuwa viongozi wa Kanisa. Walifundisha injili ya Mwokozi, waliwaalika watu kujiunga na Kanisa Lake, na walifanya miujiza mingi kwa nguvu za Mungu. Yesu aliahidi kuwasaidia kwa kumtuma Roho Mtakatifu.
Matendo ya Mitume 1:8–13; 2:41–47
Kwa sababu Yuda alikuwa amefariki, kulikuwa na Mitume kumi na mmoja tu. Mitume walisali kujua Mungu alimtaka nani achukue nafasi ya Yuda na kuwa shahidi maalum wa Yesu Kristo. Mungu alimchagua mtu aliyeitwa Mathiya. Alikuwa mmoja wa Mitume Kumi na Wawili.
Matendo ya Mitume 1:15–26
Katika sikukuu maalum ya Kiyahudi, wanafunzi walikuwa pamoja Yerusalemu. Ghafla, ilisikika kama upepo kutoka mbinguni uliijaza ile nyumba. Waliona nuru kama moto ukiwaka juu yao, na wote walijazwa Roho Mtakatifu. Kwa sababu ya Roho Mtakatifu, wangeweza kuzungumza katika lugha zingine.
Matendo ya Mitume 2:1–4
Wakati watu katika Yerusalemu waliposikia kuhusu hili, umati mkubwa ulikusanyika. Japokuwa watu katika umati walikuwa wanatoka nchi nyingi na walizungumza lugha tofauti, kila mmoja alisikia kile Mitume walichokisema katika lugha yake mwenyewe. Watu walishangazwa!
Matendo ya Mitume 2:5–13
Petro alisimama na kuzungumza na umati. Aliwaambia kuhusu Yesu Kristo. Alishuhudia kwamba Yesu ni Mwokozi na alikuwa amefufuka.
Matendo ya Mitume 2:14–36
Wakati watu waliposikia haya, walihisi kwamba walihitaji kubadilika. Waliwauliza Mitume kile walichopaswa kufanya.
Matendo ya Mitume 2:37
Petro akawaambia, “Tubuni, mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.” Takribani watu 3,000 walibatizwa na kujiunga na Kanisa siku hiyo.
Matendo ya Mitume 2:38–43
Baadaye, Petro na Yohana walikwenda hekaluni. Walimwona mtu ambaye hakuweza kutembea. Aliketi pale kila siku, akiwaomba watu pesa.
Matendo ya Mitume 3:1–2
Yule mtu aliwaomba Petro na Yohana pesa. Walisimama na kumwangalia. Petro alisema, “Tutazame sisi.”
Matendo ya Mitume 3:3–4
Petro alisema kwamba hawakuwa na fedha wala dhahabu. Lakini walikuwa na kitu kizuri zaidi. “Kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti,” alisema, “simama uende.” Petro alimsaidia kusimama. Kwa mara ya kwanza katika maisha yake, mtu yule aliweza kutembea! Alikuwa na furaha sana aliruka na kuingia hekaluni pamoja na Petro na Yohana.
Matendo ya Mitume 3:6–8
Watu walishangazwa. Petro aliwaambia kwamba haikuwa nguvu zake au nguvu za Yohana ambazo zilimponya mtu yule. Aliponywa kwa nguvu ya Yesu Kristo na imani katika Yeye. Petro aliwaambia watubu na wamwamini Yesu.
Matendo ya Mitume 3:9–26
Baadhi ya viongozi wa Wayahudi hawakupenda kile Petro na Yohana walichokuwa wakikifundisha. Walisema kwamba hakuna aliyeruhusiwa kufundisha kuhusu Yesu.
Matendo ya Mitume 4:1–18
Petro na Yohana walisema wangemtii Mungu, na Mungu aliwataka wawaambie watu kile walichokijua kuhusu Yesu Kristo.
Matendo ya Mitume 4:19–20
Mitume waliendelea kufundisha injili ya Mwokozi kwa nguvu kubwa. Watu zaidi na zaidi walijiunga na Kanisa Lake. Walijazwa na Roho. Walipendana na kushiriki kila kitu. Waliuza kile walichokuwa nacho na wakawapa pesa Mitume ili kuwapa maskini.
Matendo ya Mitume 4:31–37