“Familia ya Martins,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)
“Familia ya Martins,” Hadithi za Mafundisho na Maagano
Aprili 1972–Novemba 1978
Familia ya Martin
Kusubiria baraka za Bwana
Helvécio Martins alikuwa akiendesha gari kwenda nyumbani kutoka kazini huko Rio de Janeiro, Brazil. Barabara ilikuwa imejaa magari kiasi kwamba hakuna hata mmoja wao aliyeweza kusogea. Helvécio alifikiria kuhusu maisha yake. Alikuwa na kazi nzuri. Alimpenda mke wake, Rudá, na watoto wake wawili, Marcus na Marisa. Lakini alihisi kama kuna kitu kilikuwa kinakosekana.
Saints, 4:229–30
Helvécio alitoka nje ya gari na kuanza kusali. “Mungu wangu,” alisema, “Najua upo mahali fulani, lakini sijui wapi.” Alimwambia Baba wa Mbinguni kwamba familia yake ilikuwa inatafuta kitu fulani, na walihitaji msaada Wake. Kisha Helvécio akarudi kwenye gari lake na kuendesha gari kwenda nyumbani.
Saints, 4:230
Baadaye, Bwana aliwatuma wamisionari kutoka Marekani. Walitembelea familia ya akina Martins. Helvécio aligundua kwamba walileta roho ya amani nyumbani kwake. Alijua kwamba, wakati huo, watu wenye ngozi nyeusi mara nyingi hawakutendewa vizuri huko Marekani. Aliuliza, “Dini yenu inawatendeaje watu Weusi?”
Saints, 4:230–31
Wamisionari walieleza kwamba watoto wote wa Mungu wangeweza kubatizwa. Lakini wakati huo, watu weusi wenye mababu kutoka Afrika hawakuweza kushikilia ukuhani au kupokea baraka nyingi za hekaluni. Helvécio na Rudá walikuwa na maswali mengi zaidi. Wamisionari walifanya kadiri walivyoweza kuyajibu.
Saints, 4:231
Kwa miaka mingi, manabii walikuwa wameomba ili kujua wakati baraka za ukuhani na hekalu zingetolewa kwa watu wote.
Saints, 4:71
Helvécio na Rudá waliamua kujaribu kwenda kanisani. Watakatifu huko walikuwa wenye upendo na wakarimu sana. Familia ya Martins ilipenda kile walichojifunza kanisani.
Saints, 4:231–32
Siku moja, akiwa njiani kwenda nyumbani kutoka kanisani, Marcus aliiambia familia yake kwamba aligundua kuwa walionekana kuwa na furaha zaidi. “Najua kinachosababisha hili,” Marcus alisema. “Injili ya Yesu Kristo.” Familia yote ilijua Marcus alikuwa sahihi. Waliamua kubatizwa na kuthibitishwa.
Saints, 4:232
Miaka kadhaa baadaye, Watakatifu huko Brazil walikuwa na shughuli nyingi za kujenga hekalu. Familia ya akina Martins ilikuwa na furaha, lakini pia walikuwa na huzuni. Hawangeweza kuingia hekaluni baada ya kuwekwa wakfu. “Usijali,” Helvécio alimwambia Rudá. “Bwana anajua kila kitu.”
Saints, 4:293–94
Haikuwa rahisi kubaki mwaminifu. Watu waliwafanyia mzaha familia ya akina Martins. Hata marafiki zao hawakuweza kuelewa kwa nini walibaki Kanisani. Lakini Helvécio na familia yake walijua kwamba lilikuwa Kanisa la Yesu Kristo.
Saints, 4:251–52
Siku moja, Helvécio aliporudi nyumbani kutoka kazini, Rudá alisema, “Nina habari za kupendeza!” Baada ya kufunga sana na sala, nabii, Rais Spencer W. Kimball, alikuwa amepokea ufunuo. Mungu alimwambia kwamba mtu yeyote, bila kujali rangi ya ngozi yake, angeweza kupata kila baraka ya ukuhani na hekalu.
Tamko Rasmi 2; Saints, 4:318–19
Familia ya akina Martins na wengine wengi walikuwa wamesubiri kwa muda mrefu. Sasa kusubiri kulikuwa kumekwisha! Helvécio na Marcus walipokea ukuhani. Helvécio, Rudá, na watoto wao waliunganishwa kama familia hekaluni. Sasa wangeweza kupokea baraka zote za injili.
Saints, 4:319–21