“Parley Anaomba Msamaha,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)
“Parley Anaomba Msamaha,” Hadithi za Mafundisho na Maagano
Januari–Julai 1837
Parley Anaomba Msamaha
Ushuhuda wa rafiki unajenga imani yake
Ilipofika wakati kwa Thankful na Parley Pratt kupata mtoto wao, walirudi nyumbani kutoka misheni yao huko Kanada. Walikuwa na mtoto wa kiume mwenye afya kama vile Bwana alivyowaahidi.
Saints, 1:270
Kwa huzuni, Thankful alifariki saa chache baada ya mtoto kuzaliwa. Parley alijua asingeweza kumtunza mtoto bila yeye. Alimwomba mwanamke huko Kirtland amtunze mtoto wakati akirudi Kanada kumaliza misheni yake.
Saints, 1:270
Huko Kirtland, Joseph Smith alianzisha benki kupata fedha kwa ajili ya kazi ya Mungu. Aliwaomba watu kuiruhusu benki kutumia fedha zao ili wengine waweze kuikopa. Lakini, kwa sababu nyingi, benki haikuwa na pesa za kutosha na ilibidi ifungwe. Benki nyingine nchini Marekani zilikuwa zikianguka pia.
Saints, 1:260–61, 264–68
Maisha yakawa magumu kwa Watakatifu. Baadhi walipoteza kazi zao na sasa hawakuwa na pesa za kutosha kununua chakula au nguo. Baadhi ya watu walimkasirikia Joseph, hata baadhi ya marafiki zake wa karibu. Walidhani Joseph hakuwa nabii wa kweli kwa sababu benki ilianguka.
Saints, 1:264–68, 272–275
Wakati haya yakitokea, Parley alirudi nyumbani kutoka misheni yake. Matatizo ya benki yalifanya maisha kuwa magumu kwa Parley pia. Hangekuwa na pesa za kutosha kulipia nyumba yake, na asingekuwa na mahali pa kuishi.
Saints, 1:270–71
Sasa Parley alimkasirikia Joseph pia. Alimwandikia Joseph barua. Alimwambia Joseph kwamba bado aliamini katika Kitabu cha Mormoni. Lakini pia alisema mambo yasiyo ya ukarimu kuhusu Nabii. Alimwambia Joseph kuwa kwanza alikuwa amekosea kuanzisha benki.
Saints, 1:271
Baadaye, baadhi ya marafiki wa Parley kutoka Kanada walikuja Kirtland. Parley alikuwa amewafundisha injili, na walikuwa na furaha ya kumwona tena.
Saints, 1:279–80
Lakini pia walishangazwa kwamba Parley na wengine wengi walikuwa wamepoteza imani yao kwamba Joseph Smith alikuwa nabii.
Saints, 1:279–80
Mmoja wa marafiki wa Parley kutoka Kanada alikuwa John Taylor. Wakati Parley alipomwona, alimwambia John jinsi alivyomkasirikia Joseph Smith. Alimwambia John asimfuate tena Joseph.
Saints, 1:280
John alimkumbusha Parley kwamba walipokuwa Kanada, Parley alikuwa ameshiriki ushuhuda wake kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa kweli. “Sasa nina ushuhuda ule ule,” John alisema. “Kama kazi ilikuwa kweli miezi sita iliyopita, ni kweli leo. Kama Joseph Smith alikuwa nabii hapo mwanzo, basi hata sasa yeye ni nabii.”
Saints, 1:280
Parley alijua rafiki yake John alikuwa sahihi. Alihuzunika kuhusu barua yake ya hasira kwa Joseph. Alijua kwamba Joseph alikuwa akifanya kwa uwezo wake wote kufanya kazi ya Bwana. Matatizo ya benki hayakumaanisha kwamba Joseph hakuwa nabii wa kweli wa Yesu Kristo.
Saints, 1:283
Parley alikwenda nyumbani kwa Joseph. Alimwambia Joseph kwamba alihuzunika kuhusu mambo yasiyo ya ukarimu aliyosema. Joseph alimsamehe Parley, akasali kwa ajili yake, na akambariki. Parley alihudumu misheni nyingi zaidi na kuwaambia watu ulimwenguni kote kwamba Joseph Smith alikuwa nabii wa Bwana.
Mafundisho na Maagano 64:7–11; Saints, 1:283