“Telii Anamtumikia Bwana,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)
“Telii Anamtumikia Bwana,” Hadithi za Mafundisho na Maagano
Aprili 1844–Machi 1852
Telii Anamtumikia Bwana
Kujenga Kanisa huko Tubuai
Mwanamke aliyeitwa Telii aliishi katika kisiwa kidogo kilichoitwa Tubuai. Wamisionari kutoka makanisa tofauti wakati mwingine walimtembelea Tubuai, lakini kwa kawaida hawakukaa kwa muda mrefu. Siku moja mnamo 1844, Telii alifurahi kusikia kwamba wamisionari kutoka Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho walikuwa wamewasili Tubuai.
Mafundisho na Maagano 1:1; 133:8
Wamisionari walikuwa njiani kuelekea kwenye baadhi ya visiwa vikubwa. Lakini watu wa Tubuai waliwataka kukaa na kufundisha injili. Telii na mumewe, Nabota, walisema wamisionari wangeweza kukaa nyumbani mwao. Mmoja wa wamisionari, Addison Pratt, alikubali.
Saints, 1:573–74
Telii na Nabota walishiriki kila kitu walichokuwa nacho na Addison. Walimfundisha kuzungumza lugha yao. Addison aliwafundisha kuhusu Yesu Kristo.
Roho Mtakatifu aliwaambia Telii na Nabota kwamba injili ya Mwokozi ni ya kweli. Walikuwa watu wa kwanza kubatizwa Tubuai.
Saints, 1:573–74
Telii, Nabota, na Addison wakawa marafiki wakubwa. Walisafiri pamoja na kufundisha injili huko Tubuai na visiwa vingine. Wakati watu walipojaribu kuwaambia Watakatifu huko Tubuai kwamba hawapaswi kujiunga na Kanisa, Telii aliwafundisha kutoka kwenye maandiko kwamba Kanisa ni la kweli.
Saints, 2:27, 45
Telii alitaka kuwasaidia watu wengi zaidi huko Tubuai kujifunza injili ya Yesu Kristo. Aliweka maandiko kwenye muziki na kualika makundi makubwa kuimba pamoja naye jioni. Kuimba nyimbo za Telii kuliwasaidia watu wengi kujifunza kutoka kwenye maandiko na kukumbuka kile walichojifunza.
Miaka kadhaa baadaye, wamisionari zaidi walikuja Tubuai, ikijumuisha familia ya Addison. Telii aliwakaribisha nyumbani kwake. Alifanya kazi na mke wa Addison, Louisa, kuwahudumia wanawake wa Tubuai.
Saints, 2:133–34
Baada ya muda, wamisionari walilazimishwa kuondoka Tubuai na visiwa vingine. Lakini Telii aliendelea kufundisha na kuwaongoza Watakatifu. Kwa sababu ya mfano na huduma ya Telii, Kanisa huko Tubuai lilibaki imara.
Saints, 2:150–51