Hadithi za Maandiko
Mary na Caroline Rollins


“Mary na Caroline Rollins,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)

“Mary na Caroline Rollins,” Hadithi za Mafundisho na Maagano

Novemba 1830–Julai 1831

Mary na Caroline Rollins

Upendo imara kwa ajili ya maandiko

Mary Rollins akiwasikia wamisionari wakizungumza kuhusu Kitabu cha Mormoni.

Mary Rollins alikuwa na umri wa miaka 12 wakati wamisionari walipotembelea Kirtland, Ohio. Aliwasikia wakizungumza kuhusu Kitabu cha Mormoni. Wakati huo, kulikuwa na nakala moja tu ya kitabu hiki katika Kirtland, na kiongozi wa Kanisa aitwaye Isaac Morley ndiye aliyekuwa nacho.

Mary akiomba kuazima Kitabu cha Mormoni.

Mary alienda nyumbani kwa Kaka Morley na kuomba kukiona Kitabu hicho; Kaka Morley alimwacha akishike. Mary aliuliza kama angeweza kukipeleka nyumbani.

Mary akimsihi akiazime Kitabu cha Mormoni.

Kaka Morley hakutaka kumpa Mary nakala yake ya kitabu hicho. Hakuwa amesoma mengi bado. Mary alimsihi Kaka Morley aache aazime.

Mary akisoma Kitabu cha Mormoni.

Kaka Morley alikubali. Alisema Mary anaweza kuchukua kitabu hicho nyumbani kama angekirudisha mapema siku iliyofuata. Mary alikichukulia kama hazina. Alikaa usiku mzima akikisoma.

Mary akirudisha kitabu kwa Isaac Morley.

Wakati Mary aliporudisha kitabu, Kaka Morley alishangazwa na kiasi alichokuwa amekisoma. “Mtoto,” alisema, “chukua kitabu hiki nyumbani na kimalizie. “Ninaweza kukisubiria”

Mary anakutana na Joseph Smith.

Mary alikuwa mtu wa kwanza katika Kirtland kusoma Kitabu cha Mormoni chote. Punde baada ya kumaliza, alikutana na Nabii Joseph Smith. Alipogundua ni kiasi gani Mary alikipenda Kitabu cha Mormoni, alisema kwamba angeweza kuwa na nakala ya Kaka Morley. Yeye angempa Kaka Morley kitabu kingine.

Mary akitazama Kitabu cha Amri kikichapishwa.

Baadaye mwaka huo, Mary na familia yake walihamia Independence, Missouri. Alikuwa na shauku ya kutazama wakati viongozi wa Kanisa walipoanza kuweka pamoja kitabu kipya kilichoitwa Kitabu cha Amri. Kingekuwa na mafunuo mengi ambayo Yesu Kristo alikuwa ameyatoa kwa Joseph Smith.

Mafundisho na Maagano 67; 70:1–4; Saints, 1:178

Watu wenye hasira wakiharibu mtambo wa kupiga chapa.

Lakini baadhi ya watu huko Independence hawakulipenda Kanisa. Waliwataka Watakatifu kuondoka. Siku moja, wanaume wenye hasira walivunja jengo ambapo Kitabu cha Amri kilikuwa kikichapishwa. Walitupa mutambo wa kupiga chapa nje ya dirisha na kutawanya kurasa zake mtaani.

Saints, 1:177-78

Mary na Caroline wakijificha nyuma ya uzio.

Mary na dada yake, Caroline, walikuwa wakitazama kutoka nyuma ya uzio. Mary alimwambia Caroline kwamba alitaka kuokoa kurasa kabla hazijaharibiwa. Caroline alikuwa na hofu ya watu wenye hasira. “Watatuua,” yeye alisema. Lakini Mary na Caroline walijua kwamba kurasa hizo zilikuwa na neno la Mungu kwao.

Saints, 1:178

Mary na Caroline wakikimbia.

Akina dada hawa walisubiri mpaka wanaume wale walipokuwa hawaangalii upande wao. Akina dada walikimbia mtaani na kunyakua kurasa nyingi kadiri walivyoweza. Walipokuwa wakikimbia, baadhi ya watu waliwaona na kuwapigia kelele ili waache. Mary na Caroline walishikilia kurasa kwa nguvu zaidi na kukimbia kwa haraka kadiri walivyoweza kwenye shamba la mahindi lililokuwa karibu.

Saints, 1:178–79

Mary na Caroline wakijificha katika shamba la mahindi.

Wanaume wawili waliwafukuza akina dada hawa kwenye shamba la mahindi. Mahindi yalikuwa marefu sana, Mary na Caroline hawakuweza kuona wapi walikuwa wakienda. Walijiangusha wenyewe ardhini na kuficha kurasa hizo chini ya miili yao. Walisikiliza kwa utulivu wakati wale wanaume wawili wakitembea kupita kwenye mahindi wakiwatafuta.

Saints, 1:179

Mary na Caroline wanamsikiliza Joseph Smith.

Punde wanaume wakakata tamaa ya kuwatafuta. Mary na Caroline walikuwa salama! Walikuwa wameokoa kurasa za mafunuo ya Bwana kwa ajili ya Kitabu cha Amri. Leo mafunuo hayo yako katika kitabu cha Mafundisho na Maagano.

Saints, 1:179