“Kuijenga Nauvoo,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)
“Kuijenga Nauvoo,” Hadithi za Mafundisho na Maagano
1840–1842
Kuijenga Nauvoo
Mipango ya Bwana kwa ajili ya jiji zuri
Bwana aliwaambia Watakatifu kukusanyika katika sehemu mpya. Ilikuwa karibu na mto mkubwa uitwao Mississippi. Ardhi ilikuwa oevu na yenye matope. Kwa baadhi ya watu, haikuonekana kama mahali pazuri pa kujenga mji. Lakini Nabii Joseph Smith alijua kwamba kwa msaada wa Bwana, wangeweza kuifanya iwe nzuri.
Mafundisho na Maagano 124:25; Watakatifu, 1:417
Watakatifu walianza kufanya kazi kwa bidii ili kupafanya kuwa mahali pazuri pa kuishi. Nabii Joseph aliuita mji huu Nauvoo, ikimaanisha “mahali pazuri.”
Watakatifu, 1:417
Bwana aliwaambia Watakatifu kujenga nyumba huko Nauvoo ambapo wasafiri wangeweza kuja na kupumzika. Alitaka Nauvoo kuwa mahali ambapo kila mtu alihisi kukaribishwa.
Mafundisho na Maagano 124:22–24, 60; Watakatifu, 1:426
Bwana alimwambia Nabii Joseph kwamba alikuwa na mipango mikuu kwa ajili ya Nauvoo. Aliwataka Watakatifu Wake kukusanyika hapa ili waweze kujenga hekalu. Aliwaomba wafanye kazi kwa bidii kadiri wawezavyo kujenga nyumba Yake. Watakatifu kwa haraka walianza kufanya kazi.
Mafundisho na Maagano 124:25–28, 44, 55; Watakatifu, 1:420–21, 425–27
Bwana aliwataka Watakatifu kujenga hekalu kwa sababu Alikuwa na baraka kubwa za kuwapa. Ndani ya hekalu, wangefanya maagano, au ahadi maalumu na Bwana. Pia wangejifunza kuhusu mpango wa furaha wa Baba wa Mbinguni kwa watoto Wake wote.
Mafundisho na Maagano 124:29–41; Watakatifu, 1:453–55
Watakatifu walifanya kazi kwa bidii kujenga hekalu, kama vile Bwana alivyoamuru. Ilichukua muda mrefu, lakini walikuwa na shauku kuhusu siku ambapo kila mmoja angeweza kujifunza kuhusu ahadi maalum ambazo Bwana alikuwa nazo kwa ajili yao katika hekalu Lake.
Watakatifu, 1:453–55