“Matatizo huko Missouri,” Hadithi za Mafundisho na Maagano (2024)
“Matatizo huko Missouri,” Hadithi za Mafundisho na Maagano
Julai 1831–Julai 1833
Matatizo huko Missouri
Kushika imani imara katika nyakati za hatari
Watakatifu wengi walikuja kuishi Independence, Missouri. Bwana aliwataka kujenga mji wa Sayuni huko. Lakini Watakatifu na watu ambao walikuwa tayari wanaishi huko Independence hawakuelewana. Hawakukubaliana kuhusu mambo mengi. Baadhi ya watu katika mji huo walikasirika na walitaka kuwafanya Watakatifu waondoke.
Mafundisho na Maagano 57:1–3; Saints, 1:171–74
Edward Partridge alikuwa askofu wa huko Independence. Alikuja kwenye mkutano na viongozi wa mji huo. Walisema Watakatifu wanalazimika kuondoka Independence. Askofu Partridge alijua kwamba Mungu aliwataka Watakatifu kujenga Sayuni katika Independence. Alisema Watakatifu hawangeweza kuondoka.
Saints, 1:176
Wanaume wenye hasira walianza kubomoa nyumba na majengo ambayo Watakatifu walikuwa wamejenga.
Saints, 1:177–78, 182
Wanaume waliwatoa Askofu Partridge na mtu mwingine aliyeitwa Charles Allen kutoka majumbani mwao. Waliwaburuza watu hao wawili hadi katikati ya mji.
Saints, 1:179
Askofu Partridge alisema, “Kama lazima niteseke kwa ajili ya dini yangu, si zaidi ya wengine walivyofanya kabla yangu.” Wanaume wale walimsukuma Askofu Partridge na Charles chini ardhini. Waliweka lami ya moto na manyoya kote kwenye miili yao.
Saints, 1:179–80
William McLellin, muumini wa Kanisa huko Independence, alisikia kuhusu kile watu wenye hasira walichokuwa wakifanya. Aliogopa na kukimbilia msituni kujificha.
Saints, 1:182
William alijiuliza nini kingetokea kama watu wenye hasira wangempata. Je, bado angesema Kitabu cha Mormoni kilikuwa cha kweli, hata kama wangejaribu kumuua kwa ajili yake?
Saints, 1:182–83
Marafiki wa William, Oliver Cowdery na David Whitmer walimpata msituni. William alijua kwamba Oliver na David waliamini katika Kitabu cha Mormoni. Malaika aliwaonyesha mabamba ya dhahabu. “Niambie,” William aliwauliza, “je, kweli Kitabu cha Mormoni ni cha kweli?”
Saints, 1:183
Oliver na David walimwambia William kwamba Kitabu cha Mormon ni cha kweli. Wao walisema kwamba hata kama watu wenye hasira wangejaribu kuwaua, hawataacha kamwe kushiriki ushuhuda wao kwa watu. “Ninawaamini ninyi,” William alisema.
Mafundisho na Maagano 17:3–6; Saints, 1:183