“Mzee Ozani Farias,” Liahona, Mei 2025.
Mzee Ozani Farias
Sabini Mkuu mwenye Mamlaka
Kusali kuhusu maamuzi yenye changamoto ikawa msingi kwa Mzee Ozani Farias tangu akiwa na umri mdogo. Mzee Farias alisali baada ya kukutana na wamisionari katika umri wa miaka 15. Alisali kuhusu misioni, elimu, ndoa, na fursa za ajira.
Na hata wakati ambapo njia haikuwa wazi, alijua kile alichopaswa kufanya.
“Mungu daima anakuwa wa kwanza,” alisema. “Mtumikie Yeye kwanza. Tumeona baraka kubwa kutokana na kufanya hivi.”
Kufuata misukumo kutoka kwa Roho Mtakatifu kamwe hakujamwongoza yeye na mkewe kwenye upotovu, alisema. “Nimejifunza nguvu ya ufunuo binafsi. Mungu huzungumza na watoto Wake. Na Mungu ana mpango kwa ajili yetu.”
Ozani Barboza Marques Farias alizaliwa Recife, Brazil, mnamo Oktoba 19, 1969, kwa José Osanã Farias na Severina Barbosa Marques. Yeye na mkewe, Giovanna de Medeiros Prata Farias, waliunganishwa katika Hekalu la São Paulo Brazil mnamo Januari 18, 1994. Wana watoto watatu.
Mzee Farias alipata shahada ya kwanza katika uhasibu kutoka Chuo Kikuu cha Katoliki cha Pernambuco, shahada ya uzamili katika fedha kutoka Chuo Kikuu cha Pernambuco, na shahada ya uzamili ya utawala wa biashara kutoka Getulio Vargas Foundation. Amefanya kazi na Kanisa katika nafasi tofauti tofauti, ikiwa ni pamoja na meneja wa fedha, meneja wa rasilimali watu, na hivi karibuni kama mkurugenzi wa mambo ya kimwili katika Eneo la Brazil.
Mzee Farias kwa sasa anahudumu kama rais wa misioni ya Georgia Atlanta. Pia amehudumu kama mshauri katika urais wa kigingi, karani wa kigingi, mshiriki wa baraza kuu, askofu, mshauri katika uaskofu, na mwalimu wa Watoto.