2025
Toba Yako Haimchoshi Yesu Kristo; Inaongeza Shangwe Yake
Mei 2025


11:44

Toba Yako Haimchoshi Yesu Kristo; Inaongeza Shangwe Yake

Mwaliko wa kutubu ni dhihirisho la upendo wa Mungu. Kusema ndiyo kwa mwaliko huo ni dhihirisho la upendo wetu.

Miaka kadhaa iliyopita nikiwa safarini Florida, niliketi nje nikisoma kitabu. Kichwa chake cha habari kilipendekeza kwamba bado tunaweza kufika mbinguni, japokuwa sisi si wakamilifu sasa. Mwanamke aliyepita kando aliuliza, “Unadhani inawezekana?”

Nilitazama juu, nikiwa nimekanganyikiwa, na kisha nikatambua alikuwa akizungumzia kitabu nilichokuwa nakisoma. Nilisema kitu cha kipuuzi kama, “Vema, sijafika mbali kwenye kusoma, lakini nitakujuza kitakavyohitimisha.”

Ee, jinsi gani natamani ningerudi tena kwenye wakati ule! Ningemwambia, “Ndiyo, inawezekana! kwa sababu mbinguni si kwa ajili ya watu walio wakamilifu; ni kwa ajili ya watu waliosamehewa, wanaomchagua Kristo tena na tena.”

Leo ninataka kuzungumza na wale kati yetu ambao wakati mwingine mnahisi, “Toba na msamaha huonekana kufanya kazi kwa kila mtu isipokuwa mimi.” Wale ambao kwa siri wanajiuliza, “Kwa kuwa naendelea kufanya makosa yaleyale, pengine hivi ndivyo jinsi nilivyo.” Wale ambao, kama mimi, wana siku ambapo njia ya agano huonekana kama mwinuko mkali, ni kama vile kupanda mlima wa agano!

Mmisionari wa kupendeza huko Australia, Mzee QaQa kutoka Fiji, alishiriki hisia sawa na hiyo katika ushuhuda wake wa kuondoka: “ninajua kwamba Mungu ananipenda, lakini nyakati zingine najiuliza, je, Mungu anajua kwamba mimi Ninampenda?’ Kwa sababu mimi si mkamilifu na ninaendelea kufanya makosa.”

Katika swali lile moja la dhati, la kuchochea hisia, Mzee QaQa alifupisha kile ambacho mara kwa mara ninakihofia. Pengine unajiuliza pia, ukiwaza, “ninajaribu sana, lakini je, Mungu anajua kwamba ninajaribu kwa dhati? Ninapoendelea kukosea, je, Mungu anajua bado ninampenda?

Inanihuzunisha kukubali hili, lakini nilikuwa nikipima uhusiano wangu na Mwokozi kwa jinsi nilivyokuwa nikiishi kikamilifu. Nilidhani maisha ya utiifu yalimaanisha kamwe nisingehitaji kutubu. Na nilipofanya makosa, ambapo ilikuwa ni kila siku, nilijiweka mbali na Mungu, nikidhani, “Lazima atakuwa amekatishwa tamaa na mimi.”

Hiyo siyo kweli kabisa.

Nimejifunza kwamba ikiwa utangoja hadi uwe safi vya kutosha au mkamilifu vya kutosha ili kwenda kwa Mwokozi, utakuwa umeelewa vibaya!

Vipi ikiwa tungefikiria kuhusu amri na utiifu katika njia tofauti?

Ninashuhudia kwamba wakati Mungu anajali kuhusu makosa yetu, Yeye anajali zaidi kile kinachotokea baada ya kufanya makosa. Je, tutakwenda kumgeukia tena na tena? Je, tutakwenda kubaki kwenye njia hii ya agano?

Pengine unasikia maneno ya Bwana “Ikiwa [wewe] wanipenda, zishike amri zangu” na unahisi kupoteza ujasiri kwa sababu hujazishika amri zote. Acha nikukumbushe kuwa kutubu pia ni amri! Kwa hakika, inaweza kuwa amri iliyojirudia sana katika maandiko.

Katika maneno ya Alma, “Ee vile natamani ningekuwa malaika na ningekuwa na matarajio ya moyo [wangu] … na kuhubiri toba,” hakuwa akijaribu kutuaibisha kwa kuonesha makosa yetu. Alitaka kuhubiri toba ili wewe na mimi tuweze kuepuka kuteseka ulimwenguni. Sababu moja ya Alma kuchukia dhambi ni kwa sababu inatusababishia maumivu.

Nyakati zingine ninapaswa kukumbuka, kama vile ujumbe ulio kwenye paji langu la uso, kwamba amri ni njia za kututoa kwenye maumivu. Na toba hali kadhalika. Nabii wetu amesema, “Mwokozi anatupenda siku zote lakini hasa wakati tunapotubu.”

Hivyo Bwana anaposema, “Tubuni, Tubuni,” vipi ikiwa utamfikiria akisema, “ninakupenda. “Ninakupenda.” Pata taswira ya Yeye akikusihi kuachana na mazoea yanayokusababishia maumivu, akikualika utoke gizani na uigeukie nuru Yake.

Katika kata ya binti yangu Carly, kuhani mpya alipiga magoti kubariki sakramenti na badala ya kusema, “Ili waweze kufanya hivi kwa ukumbusho wa damu ya Mwanao,” bila kukusudia akasema “Ili waweze kufanya hivi kwa ukumbusho wa upendo wa Mwanao.” Machozi yalijaza macho ya Carly pale ukweli wa maneno yale ulipozama ndani.

Mwokozi wetu alikuwa radhi kuteseka maumivu ya Dhabihu Yake ya Kulipia Dhambi kwa sababu anakupenda. Hakika, wewe ni “furaha iliyowekwa mbele yake” wakati alipoteseka.

Mwaliko wa kutubu ni dhihirisho la upendo wa Mungu.

Kusema ndiyo kwa mwaliko huo ni dhihirisho la upendo wetu.

Vuta taswira ya picha yako pendwa ya Kristo. Sasa mfikirie akitabasamu kwa shangwe kila mara unapotumia zawadi Yake, kwa sababu Yeye ni “mng’aro mkamilifu wa tumaini.”

Ndiyo, toba yako haimchoshi Yesu Kristo; inaongeza shangwe Yake!

Hebu tulifundishe hilo!

Kwa sababu toba ndiyo habari yetu nzuri zaidi!

Hatubaki kwenye njia ya agano kwa kutofanya makosa kamwe. Tunabaki kwenye njia kwa kutubu kila siku.

Na wakati tunapotubu, Mungu anasamehe bila kutuaibisha, kutulinganisha na yeyote au kutugombeza kwa sababu hili ni jambo lilelile tulilokuwa tunalifanyia toba wiki iliyopita.

Anapendezwa kila mara anapotuona tukiwa magotini. Anafurahia kutusamehe kwa sababu Kwake Yeye sisi tuna furaha!

Je, huisi kwamba hilo ni kweli?

Kwa nini basi ni vigumu kwetu kuamini?!

Shetani, mshitaki mkuu na mdanganyi, hutumia aibu kututenga mbali na Mungu. Aibu ni hisia ya kiza kinene kiasi kwamba ukiiondoa mwilini mwako, itakuwa na uzito halisi au ujazo.

Aibu ni sauti inayokudidimiza ikisema, “Ulikuwa unafikria nini?” “Umewahi kweli kufanya jambo kwa usahihi?”

Aibu haituambii kwamba tumefanya kosa; inatuambia kwamba sisi ni makosa yetu. Unaweza hata kusikia, “Jifiche.” Mjaribu anafanya kila kitu katika uwezo wake kuweka uzito ndani, akituambia gharama ni kubwa sana, kwamba itakuwa rahisi kama hili litabaki gizani, akiondoa tumaini lote.

Shetani ni mwizi wa tumaini.

Na unapaswa kusikia hili, hivyo nitasema maneno haya kwa sauti: Wewe si sauti kichwani mwako au makosa uliyoyafanya. Unaweza kuhitaji kusema hilo kwa sauti pia. Mwambie Shetani, “Sio leo.” Mweke nyuma yako.

Hisi mvuto ule, huzuni ya kimungu inayokugeuza kwa Mwokozi wako na tazama neema Yake ikiingia maishani mwako na ndani ya maisha ya wale unaowapenda. Ninaahidi kwamba dakika ile tunapoleta moyo uliovunjika kwa ujasiri Kwake, Yeye kwa haraka yuko pale.

Ikiwa ulimwona mtu akizama, je, usingenyosha mkono kumwokoa? Je, unaweza kufikiria Mwokozi wako akiukataa mkono wako ulionyooshwa? Ninamfikiria akipiga mbizi majini, akishuka chini ya vitu vyote ili kutuinua ili tuweze kuvuta hewa safi! Hakuna anayeweza kuzama chini zaidi ya pale nuru ya Kristo inapoangaza.

Mwokozi daima ni mng’aavu zaidi ya giza la aibu. Yeye kamwe hatashambulia thamani yako. Hivyo tazama kwa makini.

  • Fikiria kwamba mkono huu huwakilisha thamani.

  • Mkono huu huwakilisha utiifu. Pengine umeamka asubuhi hii, ukasema sala yenye maana na kupekua maandiko ili kuisikia sauti ya Mungu. Umefanya maamuzi mazuri na unawatendea watu wanaokuzunguka kama vile Kristo alivyotenda. Unasikiliza mkutano mkuu! Utiifu wako uko hapa!

  • Au pengine mambo hayakwenda vizuri sana. Umepambana hivi karibuni kufanya vitu vidogo na rahisi ili kuunganika na mbingu. Umefanya baadhi ya maamuzi ambayo haujisikii fahari kuyafanya.

  • Thamani yako iko wapi? Je, mkono huu umesogea hata kidogo?

Thamani yako haijafungwa kwenye utiifu. Thamani yako iko palepale, haibadiliki kamwe. Ulipewa na Mungu na hakuna chochote ambacho wewe au mwingine yeyote anaweza kufanya kuibadilisha. Utiifu huleta baraka; hilo ni kweli. Lakini thamani si moja ya baraka hizo. Thamani yako daima ni “kubwa mbele ya Mungu,” bila kujali maamuzi yako yamekupeleka wapi.

Japo ninafanya makosa, ninataka kubaki katika uhusiano wa agano na Kristo na nitakuambia kwa nini.

Nilichukua masomo ya kupiga mbizi wakati nakua na kujifunza kwamba majaji wanapotoa alama za upigaji mbizi, wanaangalia utekelezaji. Je, kuingia kulikuwa wima kabisa, vidole vikiwa vimenyooshwa na urushaji mdogo wa maji? Kisha wanafanya jambo fulani kubwa zaidi. Wanajumlisha pamoja kiwango cha ugumu.

Kila mmoja anapiga mbizi kwa kiwango chake cha ugumu. Na Mwokozi wako ndiye pekee anayejua kwa hakika kiwango cha ugumu unachopigia mbizi. Ninataka uhusiano na mtu anayenielewa, anayeujua moyo wangu na jinsi ninavyojaribu kwa juhudi zote!

Yeye anajua ukungu wa giza unashuka kwetu sote wasafiri na kwamba safari yetu inapitia kwenye mto wenye uchafu—hivyo hata wakati tunaposhikilia fimbo ya chuma, tutarushiwa maji.

Kuja kwa Kristo ni kusema, “Unaweza kunisaidia?” kwa tumaini, hakikisho lililofunuliwa kwamba mikono Yake imenyooshwa kwako daima. Ninaamini mtazamo huu mpya wa toba humaanisha kwamba japo bado, hatuna utiifu mkamilifu, tunajaribu utiifu wa upendo kwa Mungu sasa, tukichagua kubaki, tena na tena, kwa sababu tunampenda.

Mnawakumbuka watu wa Mfalme Benjamini, ambao hawakuwa na nia ya kutenda uovu tena bali kutenda mema daima? Je, mnadhani walifungasha mahema yao, wakaenda nyumbani na hawakutenda makosa tena? Bila shaka hapana! Tofauti ni kwamba hawakutaka tena kutenda dhambi. Walikuwa na utiifu wa upendo kwa Mungu! Mioyo yao iligeuka na kumgeukia Mungu wakati wakipambana!

Mara moja, ufukweni, nilimwona ndege akipaa katika upepo, akipigapiga mabawa yake kwa nguvu, akikaribia kupata hasira, lakini akibaki sehemu moja. Kisha nikamwona ndege mwingine, juu zaidi. Alikuwa kwenye anga la juu na alikuwa akielea kwa urahisi, bila bughudha katika upepo. Hiyo ndiyo tofauti ya kujaribu kufanya hili sisi wenyewe na kumgeukia Mwokozi, tukimruhusu atuinue, kwa “uponyaji katika mbawa zake.”

Kama viongozi wa misioni huko Australia, wakati wa kuonana mara ya mwisho na kila mmisionari, tulizungumza kuhusu 3 Nefi 17, ambapo watu walikuwa karibu na Mwokozi na waliweza kumsikia Akisali kwa ajili yao. Tuliuliza, “Ikiwa ungeweza kumsikia Mwokozi akisali kwa ajili yako, unadhani angesema nini?”

Kusikia majibu yao ulikuwa moja ya uzoefu wa kiroho zaidi wa maisha yangu. Kila mmoja wa wale wamisionari angetulia, na machozi yangejaza macho yao pale tulipowakumbusha, kwamba “Mwokozi wako anajua kiwango cha ugumu unaoupitia. Yeye ameuhisi!”

Hiki ndicho wamisionari wale walijibu taratibu na kwa unyenyekevu: Mmisionari mmoja wa kike alisema “Yesu angemwambia Baba, ‘huyu anafanya kadiri ya uwezo wake. Ninajua jinsi gani anavyojaribu kwa uwezo wake wote.’” Mmisionari wa kiume alisema, “Kwa yote yanayotokea katika maisha yake, ninajivunia yeye.”

Hebu tujaribu hili. Usiku wa leo, kabla hujasali, mfikirie Yesu Kristo akiwa kando yako. Yeye ni Mwombezi wako kwa Baba. Jiulize “Ni kipi Mwokozi wangu angemwambia Baba kunihusu?”

Na kisha nyamaza.

Isikilize sauti ile inayosema mambo mazuri kuhusu wewe—sauti ya Mwokozi, rafiki yako mwema na Baba yako wa Mbinguni, ambaye hakika yupo. Kumbuka, upendo Wao na thamani yako daima ni kubwa, bila kujali chochote!

Ninasimama hapa kushuhudia kwamba Yesu Kristo hutoa nuru kwa wale wanaokaa gizani. Hivyo, katika siku zile unapohisi sauti ile ikikuambia ujifiche, kwamba unapaswa kujificha kwenye chumba chenye giza ukiwa peke yako, ninakualika uwe jasiri na umwamini Kristo! Simama, tembea na uwashe Nuru—Mng’aro wetu Mkamilifu wa Tumaini.

Ukiwa umefunikwa na nuru Yake, utawaona watu waliokuzunguka ambao wamehisi upweke pia, lakini sasa, wakiwa na nuru iliyowashwa, wewe na wao mtastaajabu, “Kwa nini tulikuwa na hofu gizani? Na kwa nini tulibaki huko kwa muda mrefu?”

“Na Bwana wa Nuru akufunike katika mikono Yake na akufariji na kukupenda daima.” Na tumpende Yeye siku zote na tumchague tena na tena. Katika jina la Yesu Kristo, amina.