2025
“Hivyo Watu Wote Watatambua Ya Kuwa Ninyi Mmekuwa Wanafunzi Wangu”
Mei 2025


15:5

“Hivyo Watu Wote Watatambua Ya Kuwa Ninyi Mmekuwa Wanafunzi Wangu”

Upendo wetu kwa Mungu na watoto Wake ni ushuhuda wenye nguvu kwa ulimwengu kwamba hili kweli ni Kanisa la Mwokozi.

Miaka mingi iliyopita mimi na Dada Uchtdorf tulikuwa tukisafiri kupitia kusini mwa Ujerumani. Ilikuwa kabla tu ya Pasaka, na tulimwalika rafiki mwema, ambaye hakuwa muumini wa Kanisa hili, ili kujiunga nasi katika ibada yetu ya Jumapili. Tulimpenda rafiki huyu mpendwa, kwa hivyo ilikuwa kawaida kushirikiana naye jinsi tulivyohisi kuhusu Mwokozi na Kanisa Lake na tumwalika aje na aone! Dada yule alikubali mwaliko huo na kujiunga nasi kwenye mikutano ya tawi lililo karibu.

Kama umewahi kumleta rafiki kanisani kwa mara ya kwanza, pengine unaweza kusimulia jinsi nilivyohisi Jumapili hiyo asubuhi. Nilitaka kila kitu kiende kikamilifu. Rafiki yetu alikuwa mtu mwenye elimu ya juu, mtu wa kiroho. Kwa dhati nilitarajia mikutano ya tawi hili ingeleta hisia nzuri kwake na kuliwakilisha vyema Kanisa.

Tawi lilikutana katika vyumba fulani vya kukodi kwenye ghorofa ya pili ya duka la vyakula. Ili kufika huko, ilitubidi kupanda ngazi nyuma ya jengo, tukipita kwenye harufu nzuri iliyotokana na bidhaa zilizohifadhiwa humo.

Mkutano wa sakramenti ulipoanza, nilifikiria kuhusu uzoefu huu wa mara ya kwanza kwa rafiki yangu, na sikuweza kujizuia kutambua mambo ambayo yalinifanya ninywee kidogo. Uimbaji, kwa mfano, haukusikika kama Kwaya ya Tabernacle. Watoto wasiotulia, wenye kelele waliweza kusikika wakati wa sakramenti. Wanenaji walifanya wawezavyo, lakini hawakuwa na ustadi wa kuzungumza mbele ya watu. Niliketi bila raha mkutanoni, nikitumaini kwamba labda Shule ya Jumapili ingekuwa bora zaidi.

Haikuwa.

Asubuhi yote nilikuwa na wasiwasi kuhusu kile ambacho rafiki yetu lazima afikirie kuhusu kanisa hili tulilokuwa tumempeleka.

Baadaye, tulipokuwa tukirudi nyumbani, niligeuka kuzungumza na rafiki yetu. Nilitaka kueleza kwamba hili lilikuwa tawi moja tu dogo na halikuwakilisha Kanisa kwa ujumla. Lakini kabla sijasema neno lolote, yeye aliongea.

“Mambo yalikuwa vizuri,” alisema.

Sikuwa na cha kusema.”

Aliendelea, “Nimefurahishwa sana na jinsi watu wanavyotendeana katika kanisa lenu. Wote wanaonekana kutoka katika asili tofauti, na bado ni wazi kwamba wanapendana kwa dhati. Hivi ndivyo nadhani Kristo alitaka Kanisa Lake liwe.”

Naam, nilitubu upesi mtazamo wangu wa kuhukumu. Nilitaka mikutano yenye picha kamili ili kumvutia rafiki yangu. Lakini kile ambacho washiriki wa tawi hili walikuwa wamekipata kilikuwa roho kamilifu ya moyo wa upendo, wema, subira na huruma.

“Kwamba Imani Ipate Kuongezeka katika Dunia”

Akina kaka na akina dada wapendwa, marafiki wapendwa, ninalipenda Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ni Kanisa la kweli na lililo hai la Mwokozi, na linafundisha utimilifu uliorejeshwa wa injili ya Yesu Kristo. Nguvu na mamlaka yake ya ukuhani yanaishi hapa. Yesu Kristo mwenyewe anaongoza Kanisa hili, kupitia watumishi ambao Yeye amewaita na kuwaidhinisha hata nabii aliye hai, Rais Russell M. Nelson. Amewapa Watakatifu wa Siku za Mwisho misheni ya kipekee ya kuwakusanya watoto wa Mungu na kuandaa ulimwengu kwa Ujio wa Pili wa Mwokozi. Natoa ushuhuda wangu kwamba haya yote ni kweli.

Lakini ni muhimu kukumbuka kwamba wakati watu wengi wanakumbana na Kanisa la Yesu Kristo kwa mara ya kwanza, hawafikirii kuhusu mamlaka ya ukuhani au ibada au kukusanywa kwa Israeli. Wanachoweza kugundua, zaidi ya yote, ni jinsi wanavyohisi wanapokuwa pamoja nasi na jinsi tunavyotendeana.

“Mpendane,” Yesu alisema. “Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi Wangu.” Mara nyingi sana, ushuhuda wa kwanza wa mtu juu ya Yesu Kristo huja wakati anapohisi upendo miongoni mwa wanafunzi wa Yesu Kristo.

Mwokozi alitamka kwamba Yeye alirejesha Kanisa Lake ili “imani … ipate kuongezeka katika dunia.” Kwa hivyo, watu wanapotembelea mikutano yetu ya Kanisa, Mwokozi anawataka waondoke wakiwa na imani yenye nguvu zaidi katika Yeye! Upendo ambao marafiki wetu wanausikia miongoni mwetu utawainua kuwa karibu zaidi na Yesu Kristo! Hili ndilo lengo letu rahisi kila mara tunapokusanyika.

Mtu yeyote anayetafuta imani kuu zaidi katika Kristo au muunganiko wa karibu zaidi na Baba wa Mbinguni anapaswa kuhisi yuko nyumbani katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Kuwaalika kwenye mikutano yetu kunaweza kuwa jambo la kawaida na la kiasili kama vile kuwaalika nyumbani mwetu.

Kilicho Bora na Halisi

Sasa, ninagundua kuwa ninaelezea kile kilicho bora. Na katika maisha haya ya duniani, mara chache tunapata uzoefu wa kile kilicho bora. Na “hadi mchana mkamilifu” daima kutakuwa na pengo kati ya kilicho bora na halisi. Kwa hiyo, tunapaswa kufanya nini iwapo Kanisa halionekani kama mchana mkamilifu? Wakati, kwa sababu yoyote ile, kata yetu bado hairutubishi imani na upendo mkamilifu? Au mnapohisi kwamba hapatufai?

Jambo moja ambalo hatupaswi kufanya ni kukata tamaa juu ya kilicho bora!

Katika ukurasa wa jina wa Kitabu cha Mormoni unajumuisha onyo hili muhimu: “Kama kuna makosa,” inasema, “ni mapungufu ya wanadamu; kwa hivyo, usilaumu vitu vya Mungu.”

Je, inawezekana kitabu—au kanisa au mtu—kuwa na “mapungufu” na “makosa” na bado ikawa kazi ya Mungu?

Jibu langu kwa sauti kubwa ni ndiyo!

Kwa hivyo, tunaposhikilia viwango vya juu vya Bwana, tuwe na subira pia na sisi kwa sisi. Kila mmoja wetu ni kazi inayoendelea, na sote tunamtegemea Mwokozi kwa maendeleo yoyote tunayofanya. Hiyo ni kweli kwetu sisi binafsi, na ni kweli kwa ufalme wa Mungu duniani.

Bwana anatualika sisi sio tu kujiunga na ufalme Wake lakini pia kujishughulisha kwa shauku katika kuujenga. Mungu huona watu walio na “moyo mmoja na nia moja.” Na kuwa wa moyo mmoja, tunapaswa kutafuta mioyo safi, na hilo linahitaji badiliko kuu la moyo.

Lakini hiyo haimaanishi kubadilisha moyo wangu ili uendane na wako. Wala haimaanishi kubadilisha moyo wako ili kuendana na wangu. Inamaanisha sisi sote tunabadilisha mioyo yetu ili kuendana na Mwokozi.

Ikiwa bado hatujafikia hapo, kumbuka kwa msaada wa Bwana, hakuna lisilowezekana.

Kufaa na Kuwa Sehemu Ya

Na ikiwa unaona kama hapakufai kabisa, tafadhali fahamu kuwa hauko peke yako. Je, sisi sote hatujakuwa katika hali za maisha wakati ambapo tulihisi kama ni mgeni katika chumba? Nimepata uzoefu huu zaidi ya mara moja. Nilipokuwa na umri wa miaka 11, familia yangu ililazimika kuondoka nyumbani kwetu na kuhamia eneo lisilojulikana. Kila kitu kilikuwa tofauti na nilivyozoea. Na lafudhi yangu iliwadhihirishia watoto wengine kuwa mimi nilikuwa tofauti na kile wao walichozoea. Wakati ambapo nilihitaji sana urafiki na kuwa sehemu yao, nilihisi mpweke na aliye uhamishoni.

Hapa duniani, tofauti nyingi tunazoziona—tofauti ambazo wengine hutumia kututenganisha—zinahusiana na mambo ya kidunia: mwonekano wa sura, utaifa, lugha, mavazi, mila na kadhalika. Lakini “Mungu haangalii kama binadamu aangaliavyo. Wanadamu huitazama sura ya nje, lakini Bwana huutazama moyo.”

Kutoka kwenye mtazamo Wake, kuna aina moja inayokuja mbele ya nyingine zote: mtoto wa Mungu. Na sisi sote tunafaa vyema katika hili.

Ni kawaida kutaka kuwa karibu na watu wanaoonekana, wanaozungumza, wanaotenda na wanaofikiri kama sisi. Kuna mahali kwa ajili ya hilo.

Lakini katika Kanisa la Mwokozi, tunakusanya watoto wote wa Mungu ambao wako tayari kukusanywa na wale wanaoutafuta ukweli. Sio mwonekano wetu wa kimwili, mitazamo ya kisiasa, utamaduni au ukabila vinavyotuleta pamoja. Sio historia yetu ya pamoja inayotuunganisha. Ni lengo letu la pamoja, upendo wetu kwa Mungu na jirani, ahadi zetu kwa Yesu Kristo na injili Yake iliyorejeshwa. Sisi tu “wamoja katika Kristo.”

Umoja tunaotafuta siyo wa kumtaka kila mtu asimame mahali pamoja; ni wa kuwafanya watu wote waelekee upande ule ule mmoja—kuelekea kwa Yesu Kristo. Sisi tu wamoja, si kwa sababu ya mahali tulipokuwa bali pale tunapojitahidi kwenda, si kwa sababu ya sisi ni nani bali vile tunavyotafuta kuwa.

Hivyo ndivyo Kanisa la kweli la Kristo lilivyo.

Mwili Mmoja

Ikiwa unampenda Mungu, ukitaka kumjua vyema kwa kumfuata Mwanawe, basi wewe ni wa hapa. Ikiwa kwa dhati unatafuta kutii amri za Mwokozi—ingawa bado hujawa mkamilifu—basi wewe unatosha kabisa kuwa katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.

Na vipi kama wewe ni tofauti na watu walio karibu nawe? Hiyo haikufanyi kuwa mtu asiyefaa—inakufanya wewe uwe sehemu inayohitajika ya mwili wa Kristo. Wote wanahitajika katika mwili wa Kristo. Masikio husikia mambo ambayo macho hayawezi kamwe. Miguu hufanya mambo ambayo mikono haiwezi kufanya.

Hiyo haimaanishi kuwa kazi yako ni kubadilisha kila mtu kuwa kama wewe ulivyo. Lakini inamaanisha kwamba una jambo muhimu la kuchangia—na kwamba una jambo muhimu la kujifunza!

Sauti Moja

Katika kila kipindi cha mkutano mkuu, tunabarikiwa na muziki wa kutia moyo kutoka kwa kwaya zenye vipaji. Unaposikiliza, unaweza kugundua kwamba waimbaji wote hawaimbi noti ile ile. Wakati fulani sehemu moja hubeba tuni, wakati fulani sehemu nyingine. Lakini wote huchangia sauti nzuri, na wameungana vyema. Kila mwanakwaya ana lengo moja kuu: kumsifu Mungu na kuinua mioyo yetu Kwake. Kila mmoja anapaswa kuweka akili na moyo wake kwenye kusudi lile lile la kimungu. Na hilo linapotokea, wanakuwa kweli sauti moja.

Ikiwa wewe bado si muumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, tunakualika ujiunge nasi tunapofurahia “wimbo wa upendo wa ukombozi wa Mwokozi.” Tunawahitaji. Tunawapenda. Kanisa litakuwa bora zaidi kwa juhudi zako za kumtumikia Bwana na watoto Wake.

Ikiwa tayari umeonyesha, kupitia ubatizo, kupitia kufanya maagano na Mungu, hamu yako ya “kuja katika zizi la Mungu, na kuitwa watu wake,” asante kwa kuwa sehemu ya kazi hii kuu na ya kiungu na kwa kusaidia kulifanya Kanisa la Yesu Kristo kuwa vile Mwokozi anataka liwe.

Kama nilivyojifunza kutoka kwa rafiki yangu huko Ujerumani, upendo wetu kwa Mungu na watoto Wake ni ushuhuda wenye nguvu kwa ulimwengu kwamba hili kweli ni Kanisa la Mwokozi.

Mungu na atubariki kutafuta kwa subira lakini kwa bidii kuishi kulingana na maadili ambayo Mwokozi, Mkombozi na Bwana wetu ameweka kwa ajili yetu—ili wote wapate kujua kwamba sisi ni wanafunzi Wake. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Yohana 13:34–35, Toleo Jipya la King James.

  2. Mafundisho na Maagano 1:21

  3. Ona Mafundisho na Maagano 46:5–6.

  4. Mafundisho na Maagano 50:24.

  5. Musa 7:18.

  6. Ona Mafundisho na Maagano 97:21.

  7. Ona Alma 5:14.

  8. Ona Luka 1:37.

  9. 1 Samweli 16:7, Tafsiri Mpya ya Kiingereza.

  10. Ona Russell M. Nelson, “Choices for Eternity” (worldwide devotional for young adults, Monday, May 15, 2022), Gospel Library.

  11. Wagalatia 3:28.

  12. Ona Mafundisho na Maagano 6:36.

  13. Ona 1 Wakorintho 12:12–27. Katika mwili wa Kristo, hatupuuzi tofauti, na hatuzivumilii tu. Tunashukuru kwa mchango wa kipekee ambao kila mwanachama hutoa, kwa manufaa ya mwili mzima.

  14. Vile vile itakuwa si sahihi kwa sikio kuutazama mwili na kusema, “Mimi si kama jicho; lazima pasiwe na mahali kwangu hapa,” itakuwa si sahihi vile vile kwa jicho kuliambia sikio, “Wewe si kama mimi; hatuna haja nawe hapa” (ona 1 Wakorintho 12:16, 21).

  15. Alma 5:26.

  16. Mosia 18:8. Tunapobatizwa, tunashuhudia kwamba, miongoni mwa mambo mengine, tunataka kuwa sehemu ya watu ambao “wanachukuliana mizigo” na “kuomboleza pamoja na wale [wanaoomboleza]” na “kuwafariji wale wanaohitaji faraja” (mistari ya 8–9). Kwa maneno mengine, tunapojiunga na Kanisa la Yesu Kristo, tunasema—kwa unyenyekevu, lakini kwa uwazi—kwamba tunataka kuwa zaidi kama Mwokozi wetu mpendwa, na tunataka kufanya hivyo pamoja.