2025
Hisani—Ishara ya Uanafunzi wa Kweli
Mei 2025


11:29

Hisani—Ishara ya Uanafunzi wa Kweli

Hatma halisi ya uanafunzi ni kuwa jinsi Yesu Kristo alivyo.

Rais Russell M. Nelson hivi majuzi alitualika “kufanya uanafunzi wetu kuwa kipaumbele chetu cha juu zaidi.” Mwaliko huo wenye nguvu umenichochea kutafakari kwa kina kuhusu uanafunzi wangu binafsi kwa Yesu Kristo.

Uanafunzi Ni Juhudi ya Makusudi

Mwanafunzi ni mfuasi au anayejifunza kwa mwingine. Wanafunzi ni “wanagenzi” ambao hujitolea maisha yao kuwa kama mwalimu wao. Hivyo, kuwa mwanafunzi wa Yesu Kristo kunamaanisha zaidi ya kuamini mafundisho na injili Yake. Inamaanisha zaidi ya kuukubali uungu Wake na kumkubali kama Mwokozi na Mkombozi wetu, kadiri ambavyo hilo ni muhimu sana.

Rais Dallin H. Oaks alieleza: “Kumfuata Kristo si jambo la kawaida au la wakati fulani. Ni dhamira endelevu na njia ya maisha ambayo inapaswa kutuongoza nyakati zote na katika mahali popote.” Uanafunzi ni safari ya makusudi ambayo tunachukua ili kubadilishwa kupitia dhabihu ya upatanisho ya Bwana na nguvu Yake ya kuwezesha. Hatma halisi ya uanafunzi ni kuwa jinsi Yesu Kristo alivyo—hata kufikia kiwango ambapo tunapokea “mfano Wake katika nyuso [zetu].”

Ili kuwa wanafunzi wa Bwana, lazima tuige mawazo na matendo Yake kwa makusudi kila siku—kwa mfano, utiifu Wake, unyenyekevu, na subira. Tunapojumuisha sifa hizi hatua kwa hatua katika utambulisho wetu wenyewe, tunakuwa “washiriki wa asili [Yake] ya uungu.” Uigaji huu wa tabia ya Mwokozi ndio kiini cha kumwabudu Yeye. Kama Rais Nelson alivyofundisha, “Kumwabudu kwetu Yesu kunaonyeshwa vyema zaidi kwa kumwiga Yesu.”

Ishara ya Uanafunzi wa Kweli

Kati ya sifa nyingi za kiungu za Yesu Kristo tunazopaswa kuiga, moja inasimama kama sifa kuu na kujumuisha zingine zote. Sifa hiyo ni upendo Wake msafi, au hisani. Wote wawili, nabii Mormoni na Mtume Paulo wanatukumbusha kwamba bila hisani, “[sisi] si kitu.” Au, kama ilivyofunuliwa kwa Nabii Joseph Smith, bila “hisani, [sisi] hatuwezi kufanya lolote.”

Mwokozi Mwenyewe alibainisha upendo kama alama au ishara ambayo kwayo wanafunzi Wake wa kweli wangetambuliwa wakati alipotangaza:

“Amri mpya nawapa, Mpendane; kama nilivyowapenda ninyi, nanyi mpendane vivyo hivyo.

“Hivyo watu wote watatambua ya kuwa ninyi mmekuwa wanafunzi wangu, mkiwa na upendo ninyi kwa ninyi.”

Hisani ni dhana tajiri ambayo inaweza kuwa ngumu kufafanua lakini inatambulika kwa urahisi na wote wanaoguswa nayo. Hubiri Injili Yangu inafundisha kwamba “hisani, kama imani, huongoza kwenye matendo.” Kwa kweli, hisani inaweza kufafanuliwa kuwa “upendo kwa vitendo.” Maelezo haya yanatoa umaizi mkubwa katika taarifa ya muhtasari wa maisha ya Mwokozi—Yeye “alienda huku na huko akitenda mema.”

Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunapaswa kutafuta kuiga jinsi Bwana wetu alivyoonyesha upendo Wake safi kwa wengine. Ingawa Mwokozi hudhihirisha hisani kwa njia nyingi, ningependa kutilia maanani mifumo mitatu maalum ya hisani Yake ambayo inaonekana kwa urahisi kwa wanafunzi Wake wa kweli.

Hisani Ni Kuonyesha Huruma

Kwanza, Mwokozi alionyesha hisani kwa kuwa na huruma. Wakati wa huduma Yake miongoni mwa Wanefi kama ilivyoandikwa katika Kitabu cha Mormoni, Bwana aliwaalika watu kurudi nyumbani na kutafakari juu ya mambo Aliyofundisha na kujiandaa kwa ajili ya kurudi Kwake siku iliyofuata. Kisha kumbukumbu inasema:

“Walikuwa wakitokwa na machozi, na walimtazama kwa uthabiti kana kwamba wangemwomba akae nao kwa muda mrefu kidogo.

“Na akawaambia: Tazama, matumbo yangu yamejawa na huruma juu yenu.”

Huruma ni sehemu ya hisani inayotaka kupunguza mateso. Akiwa amejawa na huruma, Bwana aliwaponya wagonjwa na walioteseka kati ya watu. Baadaye, Aliwabariki watoto wao huku malaika wakishuka kutoka mbinguni na kuwazunguka. Alifanya matendo haya ya huruma, ya upendo, na mengine mengi, kwa sababu Yeye “alisukumwa na huruma.”

Nilipokuwa nikitumikia kama mishonari kijana huko Amerika Kusini, mimi pia nilinufaika kutokana na huruma ya rafiki mpendwa. Jioni moja nilipokuwa nikiendesha gari kuelekea nyumbani kwa rais wetu wa misioni, kijana mmoja akiwa kwenye baiskeli aligeuka ghafla mbele ya gari langu. Ilifanyika haraka sana kiasi kwamba sikuweza kukwepa mgongano. Kwa bahati mbaya, kijana huyu alifariki kwa mgongano ule. Nilihuzunika sana kwa kupoteza maisha yake. Nikiwa na hofu na mshtuko wakati ukweli wa kutisha wa kile ambacho kilikuwa kimetoka uliponiingia, nilipelekwa jela na kufungwa. Sikuwa nimewahi kuogopa vile na kuwa peke yangu. Nilijawa na kukata tamaa na hofu kwamba ningefungwa gerezani maisha yangu yote.

Mimisionari mwenzangu, Mzee Brian Kochever, alipata habari kuhusu ajali hiyo na akasukumwa kwa huruma. Alikuja gerezani na kuwasihi maofisa waruhusiwe kukaa na mimi katika chumba cha gereza ili nisiwe peke yangu. Kwa muujiza, walikubali. Hadi leo, ninahisi shukrani nyingi kwa kitendo cha mwanafunzi huyu cha upendo kama wa Kristo, ambao ulinituliza, kunifariji, na kunipa ujasiri wakati wa dhiki kuu maishani mwangu. Huruma Yake ya hisani ilikuwa ishara ya uanafunzi wake. Kama Rais Nelson alivyosema, “Njia moja rahisi ya kumtambua mfuasi wa kweli wa Yesu Kristo ni kwa huruma kiasi gani mtu huyo huwatendea wengine.”

Hisani Ni Uhudumiaji kwa Mahitaji Yasiyosemwa

Mfano mwingine wa jinsi Mwokozi anavyoonyesha upendo Wake ni kupitia kukumbuka Kwake na huduma Yake kwa mahitaji ambayo hayajasemwa ya wengine. Kwa yule mtu aliyekuwa mlemavu wa miguu kwa muda wa miaka 38 bila mtu wa kumsaidia, Bwana alimwinua na kumtia moyo kuishi kwa haki. Kwa mwanamke aliyekamatwa katika uzinzi, Alitoa tumaini na faraja badala ya hukumu. Kwa mtu aliyepooza ambaye alishushwa kutoka juu ya paa, Bwana alitoa msamaha wa dhambi, sio uponyaji wa mwili tu.

Nilipoitwa kuhudumu kama askofu, watoto wetu sita wadogo walifanya mikutano ya sakramenti kuwa changamoto kwa mke wangu, Cristin, ambaye alilazimika kuwamamia peke yake wakati mimi nikiwa nimeketi jukwaani. Kama unavyoweza kufikiria, watoto wetu mara nyingi hawakuwa na staha. Walipotambua hali yake, washiriki wawili wa kata yetu, John na Debbie Benich, walianza kuketi na Cristin kila Jumapili ili kusaidia. Ukarimu wao uliendelea kwa miaka mingi, na wakawa babu na bibi mbadala wa familia yetu. Kama vile Bwana, wanafunzi hawa walikuwa wameona hitaji lisilosemwa na wakatenda kwa upendo—ishara kuu ya ufuasi wao.

Hisani Ni Kuewasaidia Wengine Katika Njia ya Agano

Hatimaye, upendo mkamilifu wa Mwokozi unafokasi katika kuwawezesha watoto wote wa Mungu kutimiza uwezekano wetu wa kiungu ili tuweze “kushiriki wokovu wake, na nguvu za ukombozi wake.” Tunapozidi kuwa kama Bwana wetu, hamu yetu ya kuwasaidia kaka na dada zetu kwenye njia ya agano itaongezeka kwa njia za asili.

Kwa mfano, tunaweza kuinua na kufanya urafiki na wale wanaohisi kuchukizwa au kusahauliwa, kuwasaidia wale ambao ni wapya kwenye mkutano wetu kujisikia wamekaribishwa, au kuwaalika marafiki kuabudu pamoja nasi katika mkutano wa sakramenti—pengine Pasaka hii ijayo. Kuna njia zisizo na idadi za kuwatia moyo na kuwasaidia wengine katika upigaji wao hatua ikiwa kwa kukusudia na kwa sala tutatafuta msaada wa kimbingu ili kuwa na macho ya kuona na moyo wa kuhisi jinsi Yesu Kristo anavyowaona na kuhisi kwa ajili yao.

Kuwasaidia wengine kwenye njia yao ya agano kunaweza kuchukua namna ya tendo lisilo la kawaida la huduma. Kwa mfano, nilipokuwa katika jukumu langu la sasa huko Ufilipino, nilijifunza kuhusu familia ya Agamata. Walibatizwa mwaka 2023, na kisha kwa shauku wakaweka tarehe ya kuunganishwa kama familia katika Hekalu la karibu la Urdaneta Ufilipino. Hata hivyo, kabla tu ya miadi ya familia, vimbunga kadhaa vilipiga eneo hilo. Kaka Agamata, mkulima wa mpunga, hakuweza kupanda mazao yake wakati wa dhoruba kali. Tufani zilipopita, alihitaji kupanda mpunga haraka huku ardhi ikiwa imelowa maji—hali bora ya kupanda. La kusikitisha, safari ya hekaluni ingelazimika kuahirishwa.

Wamisionari wakisaidia kupanda mpunga.
Wamisionari wakipanda mpunga.

Wanafunzi wawili, Mzee na Dada Cauilan, pamoja na wamisionari wa huduma watatu vijana, walisikia kuhusu matatizo ya familia ya Agamata na wakatoa msaada japokuwa hawakuwa na uzoefu wa ukulima. Wakifanya kazi chini ya jua kali, walisaidia kupanda miche, na kuwaruhusu akina Agamata kukamilisha kazi yao na kuhudhuria kuunganishwa hekaluni kama ilivyopangwa. Mzee Cauilan alisema kwamba “[nyuso za akina Agamata] ziling’ara wakati tulipowaona wamevaa mavazi meupe katika nyumba ya Bwana. Shangwe tuliyoisikia wakati tukimhudumia yule mmoja ni furaha isiyo na kifani!”

Familia ya Agamata ikiwa nje ya hekalu.

Akina Agamata sasa wanafurahia baraka tele za kuunganishwa kama familia ya milele kwa sababu wanafunzi wenzao wachache ambao walijawa na hisani—ishara ya ufuasi wao—waliamua kuwasaidia kaka na dada zao kusonga mbele katika njia yao ya agano.

Akina kaka na akina dada, uanafunzi wa Yesu Kristo ndiyo njia pekee ya kupata furaha ya kudumu. Ni njia iliyojaa matendo ya makusudi na yenye lengo la upendo kwa wengine. Ingawa njia ya ufuasi inaweza kuwa ngumu na yenye changamoto, na wakati fulani tunaweza kuhangaika na kukosea, tunaweza kupata faraja kwamba Mungu anatukumbuka na anatamani kutusaidia kila wakati tunapojaribu. Isaya anatukumbusha kwamba “Mungu atatushika mkono, akisema … , Usiogope, mimi nitakusaidia.”

Tukiwa hakikisho hili kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni akilini, ninasali kwa dhati kwamba tuweze kufuata mwaliko wa Rais Nelson wa kufanya ufuasi wetu uwe kipaumbele. Na “tusali kwa Baba kwa nguvu zote za moyo” ili “tujazwe na upendo huu, ambao ameuweka juu ya wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo; … ili wakati atakapoonekana tuwe kama yeye” kwa sababu tunabeba ishara ya uanafunzi wa kweli, ambayo ni “hisani … upendo msafi wa Kristo.”

Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo ndiye Mwokozi wetu aliye hai, mtukufu, Mkombozi, Mfano, na rafiki yetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Russell M. Nelson, “Bwana Yesu Kristo Atakuja Tena,” Liahona, Nov. 2024, 121.

  2. Ona Merriam-Webster.com Dictionary, “disciple.”

  3. Dallin H. Oaks, “Kumfuata Kristo,” Liahona, Nov. 2024, 23.

  4. Alma 5:14; ona pia Alma 5:19.

  5. Ona 2 Petro 1:3–8.

  6. Russell M. Nelson, “Perfection Pending,” Ensign, Nov. 1995, 87.

  7. Moroni 7:46; ona pia 1 Wakorinto 13:3.

  8. Mafundisho na Maagano 18:19; msisitizo umeongezwa.

  9. Yohana 1:34–35; msisitizo umeongezwa.

  10. Hubiri Injili Yangu: Mwongozo wa Kushiriki Injili ya Yesu Kristo (2023), 127.

  11. Matendo ya Mitume 10:38.

  12. Ona 3 Nefi 17:3.

  13. 3 Nefi 17:5–6.

  14. Ona Merriam-Webster.com Dictionary, “compassion.”

  15. Ona 3 Nefi 17:7–25.

  16. Mathayo 9:36; 14:14; Marko 1:41; 6:34.

  17. Maafisa wa polisi waliniweka gerezani kama sehemu ya utaratibu wao wa kawaida wa ajali iliyosababisha kifo. Walinitenganisha na mwenzangu kwa sababu mimi nilikuwa dereva. Nilikuwa gerezani kwa siku mbili. Wakati wa uchunguzi wa polisi, waligundua kwamba kijana huyu alikuwa amelewa wakati wa ajali hiyo na kwamba huenda hilo lilichangia kugeuka kwake ghafla mbele ya gari letu lililokuwa likiendeshwa. Nilifika mbele ya hakimu kwa ajili ya kusikilizwa rasmi, ambapo iliamuliwa kwamba hakukuwa na ushahidi wa kosa au uzembe bali kwamba hii ilikuwa tu ajali mbaya na ya kutisha.

  18. Ona Mathayo 25:31–40, hususani mstari wa 36.

  19. Russell M. Nelson, “Wapatanishi Wanahitajika,” Liahona, Mei 2023, 98.

  20. Ona Yohana 5:2–9, 14

  21. Ona Yohana 8:1–11.

  22. Ona Marko 2:1–12.

  23. Omni 1:26.

  24. Ona Mafundisho na Maagano 76:12.

  25. Ona 2 Nefi 26:24.

  26. Mawasiliano binafsi na Darwin Serrano Cauilan, Des. 1, 2024.

  27. Isaya 41:13.

  28. Moroni 7:48.

  29. Moroni 7:47.