Kweli kwa Imani Ambayo Wazazi Wetu Wameitunza
Tafadhali jifunze na upokee nguvu kutoka kwa imani na ushuhuda wa wale waliokuja kabla yako.
Nikiwa natembelea Hekalu la Nashville Tennessee kwa ajili ya ukaguzi wa hekalu, nilipata fursa ya kutembezwa ndani kama sehemu ya kazi hii, nilikagua nyumba hii nzuri ya Bwana. Nilivutiwa sana hasa na picha ya Mary Wanlass inayoitwa Carry On iliyotundikwa ukutani katika ofisi ya matroni.
Hii ni hadithi inayohusiana na picha:
“Huko Missouri katika mwaka 1862 Mary Wanlass mwenye umri wa miaka 14 alimwahidi mama yake wa kambo aliyekaribia kufa kwamba angeona kwamba baba yake mlemavu [na ndugu zake wanne wadogo wote watafika] kwenye Bonde la Great Salt Lake. … Mary aliendesha maksai na ng’ombe wa maziwa ambao walivuta mkokoteni, ambapo baba yake [alikuwa amelazwa, na] aliwatunza ndugu … zake. Baada ya safari ya kila siku, alilisha familia kwa kuchuna mimea ya chakula, maua, na matunda. Dira yake pekee ilikuwa ni maelekezo aliyokuwa ameyapokea ya kuendelea kusafiri magharibi ‘hadi mawingu kuwa milima.’
“Walifika Utah Valley mwezi Septemba, baada ya kusafiri majira yote ya kuchipua na majira ya joto. Baba yake alifariki muda mfupi baada ya familia hiyo kuishi katika Kaunti ya Utah, ambapo Mary baadaye aliolewa na kulea familia yake [mwenyewe].
Hii ni hadithi ya kushangaza ya imani na nguvu ya msichana wa miaka 14 ambaye anaweza kumsaidia kila mmoja wetu leo “endelea tu.”
“Endelea tu,”—au kwa kutafsiriwa kijuujuu katika lugha yangu ya asili ya Kiholanzi, Gewoon doorgaan—pia ni kauli mbiu ya maisha ya mama na baba yangu.
Wazazi na wakwe zangu ni waanzilishi katika familia yetu. Wamevuka “mawanda” yao wenyewe, kama wale wote wanaokuja katika Kanisa, zizi la Bwana, kila siku. Hadithi zao hazihusiani na ng’ombe na mikokoteni lakini zina athari sawa kwa vizazi vijavyo.
Walikumbatia injili na walibatizwa wakati wa miaka yao ya ujana. Wazazi wangu wote wawili walikuwa na wakati mgumu utotoni. Baba yangu alikulia katika kisiwa cha Java katika Indonesia. Wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia, alitenganishwa kwa nguvu na familia yake na akatupwa korokoroni katika kambi ya mateso, ambapo alipata shida zisizoelezeka katika umri mdogo.
Mama yangu alilelewa katika nyumba iliyovunjika na pia aliteseka kutokana na njaa na ugumu wa Vita vya Pili vya Dunia. Wakati mwingine hata alilazimika kutumia kula tunguu la tulipu. Kwa sababu ya matendo ya baba yake na talaka yake ya baadaye kwa mama yake, wakati mwingine ilikuwa vigumu kwake kumwona Baba wa Mbinguni kama Baba mwenye upendo.
Wazazi wangu walikutana katika shughuli za Kanisa na baadaye kuamua kuoana na kuunganishwa katika Hekalu la Bern Switzerland. Wakisubiri katika kituo cha reli, baada ya kutumia akiba yao ndogo ya mwisho kwa safari ya hekalu, walishangaa jinsi wangefikia mwisho lakini walikuwa na uhakika kwamba yote yatakuwa sawa. Na ndivyo ilivyokuwa!
Walianza kulea familia yao kwenye nyumba ya kimaskini sana fleti ya chumba kimoja cha darini katikati ya Amsterdam. Baada ya miaka kadhaa ya kufua nguo zao kwa mkono, hatimaye walikuwa wamehifadhi pesa za kutosha kununua mashine ya kufulia. Kabla tu ya kununua, askofu aliwatembelea, akiomba mchango wa ujenzi wa nyumba ya mkutano huko Amsterdam. Waliamua kutoa yote waliyokuwa wamehifadhi kwa ajili ya mashine ya kufulia na kuendelea kufua kwa mkono.
Kama familia tulipitia baadhi ya magumu, kama tu familia nyingine yo yote. Haya yametufanya kuwa na nguvu na yameimarisha imani yetu katika Bwana Yesu Kristo, kama vile wakati Alma alipokuwa akishiriki hadithi yake na mwanawe Helamani, ambapo alimwambia kwamba alikuwa amesaidiwa katika majaribu na shida za kila aina kwa sababu alikuwa ameweka imani yake kwa Bwana Yesu Kristo.
Ni kwa jinsi gani watu wawili ambao waliopata majaribu mengi katika miaka yao ya ujana walikuwa wazazi bora zaidi ambao ningeweza kutamani? Jibu ni rahisi: walikumbatia injili kikamilifu na kuishi kwa maagano yao hadi leo hii!
Baada ya zaidi ya miaka 65 ya ndoa, mama yangu, ambaye aliugua ugonjwa wa Alzheimer, alifariki mwezi Februari. Baba yangu, akiwa umri wa miaka 92 na bado anaishi nyumbani, alimtembelea mara nyingi kadiri awezavyo hadi alipofariki. Wakati fulani uliopita aliwaambia ndugu zangu wadogo kwamba uzoefu wa kutisha katika kambi ya Indonesia wakati wa Vita vya Pili vya Dunia ulikuwa umemwandaa kumtunza mke wake kwa uvumilivu kwa miaka mingi hivi kwani aliugua na kudhoofika kutokana na ugonjwa huu wa kutisha na pia kwa siku ya kutisha ilibidi akabidhi huduma yake ya msingi kwa wengine na hakuweza kuwa kando yake tena. Kauli mbiu yao imekuwa na bado ni “Kuendelea tu,” kuwa na tumaini kamili katika Kristo kuinuliwa katika siku ya mwisho na kukaa pamoja Naye katika utukufu milele na milele.
Imani yao na shuhuda zao ni nguvu ya kuendelea kwa vizazi ambavyo vimekuja baada yao.
Katika kijiji ambacho mke wangu alikulia, wazazi wake, ambao walikuwa watu wazuri wa kanisa, walikumbatia injili kama wanandoa vijana waliooana wakati mke wangu akiwa binti yao wa miaka miwili na mtoto pekee wakati huo. Uamuzi wao wa kuwa waumini wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho ulikuwa na athari kubwa katika maisha yao kwani walitengwa na wanakijiji na hata familia zao. Ilichukua miaka mingi, barua za upendo kwa wanafamilia, na huduma kwa jamii kabla ya hatimaye kukubaliwa.
Katika tukio moja wakati baba wa mke wangu alikuwa akihudumu kama askofu, alishtakiwa kwa uwongo kwa kitu fulani na mara moja alipumzishwa. Mama mkwe wangu aliumia sana kiasi kwamba alimwambia mume wake ikiwa wanapaswa kuendelea kwenda kanisani. Alijibu kwamba bila shaka wataendelea kwenda kanisani kwa kuwa hili sio kanisa la wanadamu, lakini hili ni Kanisa la Yesu Kristo.
Ilichukua muda mrefu kabla ya ukweli kujulikana na msamaha uliombwa. Kile kilichopaswa kuwavunja moyo kikaja kuongeza nguvu na kusadiki kwao.
Kwa nini baadhi yetu tunachukulia kawaida tu imani na shuhuda za wazazi wetu ambao kupitia taabu zao zote wamebaki waaminifu? Je, tunafikiria kwamba hawana uelewa kamili wa vitu? Hawakudanganywa na hawajadanganywa! Wamekuwa na uzoefu mwingi sana na Roho na wanaweza kusema pamoja na Nabii Joseph, “Nilijua, … na sikuweza kukanusha.”
Je, hupendi wimbo kuhusu jeshi la Helamani, unaopatikana katika Kitabu cha Nyimbo za Watoto?
Hata wakati hii inaweza kutokuwa hivyo, kama mama yangu alivyopitia akiwa mtoto, unaweza kuwa mmoja wa wale “wazazi wazuri ambao wanampenda Bwana” na kutoa mfano mzuri kwa wengine.
Je, tunahisi kwamba hii ni kweli kabisa wakati tunaimba? Je, unahisi kwamba wewe ni “kama jeshi la Helamani” na kwamba “mtakuwa wamisionari wa Bwana kuuleta ulimwengu kwenye ukweli Wake”? nimehisi mara nyingi wakati nikiimba wimbo huu katika mazingira kadhaa ya KNV na mikusanyiko mingine ya vijana.
Au tunahisi vipi wakati tunapoimba wimbo “Tupo Waaminifu wa Imani”?
Kwa wale wa kizazi kinachoinuka popote ulipo na katika hali yoyote unayoweza kujikuta, tafadhali jifunze na upokee nguvu kutoka kwa imani na ushuhuda wa wale ambao waliokuja kabla yako. Itakusaidia kuelewa kwamba ili kupata au kukuza ushuhuda, dhabihu zitalazimika kufanywa na kwamba “dhabihu hutuletea baraka za mbinguni.”
Kufikiria juu ya dhabihu ambayo itabariki maisha yako, tafadhali fikiria na kuomba kuhusu mwaliko wa nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, alipoomba “kila kijana anayestahili, mwenye uwezo ajiandae na kutumikia misheni. Kwa wavulana Watakatifu wa Siku za Mwisho, huduma ya ummisionari ni jukumu la kikuhani. …
“Kwa … ninyi akina dada wenye uwezo, misheni pia ni kitu chenye nguvu, lakini ni, fursa, ya hiari.”
Unaweza kuitwa kama mmisionari wa huduma au wa kufundisha. Aina zote mbili za wamisionari huchangia lengo moja la kuleta nafsi kwa Kristo, kila mmoja kwa njia yake ya kipekee na yenye nguvu.
Katika aina zote mbili za huduma, utamwonyesha Bwana unampenda Yeye na kwamba unataka kumjua Yeye vizuri zaidi. Kumbuka, “kwani ni vipi mtu atamjua yule bwana ambaye hajamtumikia, na aliye mgeni kwake, na yuko mbali katika mawazo na nia za moyo wake?”
Sisi sote, iwe sisi ni kizazi cha kwanza katika injili au cha tano, tunapaswa kujiuliza, Ni hadithi gani za imani, nguvu, na kujitolea kwa selestia nitakazopitisha kwa kizazi kijacho?
Hebu sote tuendelee katika juhudi zetu za kumjua Mwokozi wetu, Yesu Kristo, vizuri na kumfanya Yeye kuwa kitovu cha maisha yetu. Yeye ndiye mwamba ambao lazima tujenge ili wakati nyakati zitakapokuwa ngumu, tutaweza kusimama imara.
Hebu tuwe “wakweli kwa imani ambayo wazazi wetu wameitunza, kweli kwa ukweli ambao mashahidi wameangamia, kwa amri ya Mungu, roho, moyo, na mkono, waaminifu na wa kweli tutasimama milele.” Katika jina la Yesu Kristo, amina.