2025
Kuabudu
Mei 2025


14:14

Kuabudu

Kwa hivyo kumsujudia Mungu inamaanisha nini kwako wewe na mimi?

“Sasa Yesu alipozaliwa huko Bethlehemu ya Yudea katika siku za Herode mfalme, tazama, walikuja watu wenye hekima kutoka mashariki ya Yerusalemu,

“Wakisema, Yuko wapi yeye aliyezaliwa Mfalme wa Wayahudi? Kwani tumeiona nyota yake mashariki, nasi tumekuja kumsujudia.”

Mamajusi, kama wakati mwingine wanavyoitwa, walikuwa na hekima katika kutafuta na kumsujudia Masiya. Kwao, kusujudu ilimaanisha kuanguka chini mbele Zake na kumpatia Yeye zawadi za dhahabu na vito vya thamani na uvumba.

Kwa hivyo kumsujudia Mungu inamaanisha nini kwako wewe na mimi?

Tunapofikiria kuabudu, mawazo yetu kwa kawaida hugeukia kwenye njia ambazo tunaonyesha kujitolea kwetu kidini vyote kibinafsi na katika ibada za Kanisani. Kama nilivyozingatia suala la kumwabudu Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa, Mwokozi wetu, vipengele vinne vimekuja akilini mwangu: kwanza, vitendo ambavyo vinajumuisha kuabudu kwetu; pili, mitazamo na hisia ambazo zinaonyeshwa katika kuabudu kwetu; tatu, upekee wa kuabudu kwetu; na nne, haja ya kufuata mfano wa Viumbe Watakatifu ambao tunawaabudu.

Kwanza, Vitendo Ambavyo Vinachangia Kuabudu Kwetu

Moja ya aina za kawaida na muhimu zaidi za kuabudu ni kukusanyika katika sehemu zilizotakaswa ili kufanya matendo ya kiibada. Bwana anasema, “Na ili ujilinde na dunia pasipo mawaa, utakwenda kwenye nyumba ya sala na kutoa sakramenti zako katika siku yangu takatifu.” Hii, kweli ndio, motisha yetu ya msingi katika ujenzi wa majengo ya kanisa. Lakini, kama ni lazima, sehemu isiyowekwa wakfu itafaa kama tutawekeza kwa kiwango fulani cha utakatifu.

Mkutano wa Sakramenti

Muhimu zaidi ni tunafanya nini tunapokutana katika siku ya Bwana. Ndiyo, tunavaa vizuri kadiri tuwezavyo kulingana na uwezo wetu—siyo kwa kupita kiasi bali kuvaa kimaadili katika njia inayoonyesha heshima yetu na unyenyekevu kwa Mungu. Mwenendo wetu vile vile ni wa staha na wa heshima. Tunaabudu kwa kuungana katika sala; tunaabudu kwa kuimba nyimbo za dini (siyo tu kusikiliza bali kuimba nyimbo hizo za dini); tunaabudu kwa kufundishana na kujifunza sisi kwa sisi. Yesu anasema, “Kumbuka kwamba kwenye siku hii, siku ya Bwana, utatoa dhabihu zako [ikimaanisha ‘matoleo yako … ya muda, vipaji, au rasilimali, katika kumtumika Mungu na wanadamu wenzako’] na sakramenti zako kwa Aliye Juu Sana, ukiziungama dhambi zako kwa ndugu zako, na mbele za Bwana.” Hatuji pamoja ili kuburudisha au kuburudishwa—kama kwa bendi, kwa mfano—bali kumkumbuka Yeye na “kuelekezwa kwa ukamilifu zaidi” katika injili Yake.

Katika mkutano mkuu wa hivi karibuni zaidi, Mzee Patrick Kearon alitukumbusha kwamba “hatukusanyiki kwenye Sabato ili tu kuhudhuria mkutano wa sakramenti na kuweka alama ya vema kwenye orodha ya mambo ya kufanya. Tunakuja pamoja ili kuabudu. Kuna tofauti yenye umuhimu kati ya haya mawili. Kuhudhuria inamaanisha kuwepo pale. Lakini kuabudu ni kwa makusudi kabisa kumsifu na kumsujudia Mungu wetu katika njia ambayo hutubadilisha!”

Kuitoa Sabato yetu kwa Bwana na madhumuni Yake, hiyo yenyewe ni kitendo cha kuabudu. Miaka kadhaa iliyopita, wakati huo Mzee Russell M. Nelson aliuliza: “Ni kwa jinsi gani tunaweza kuitukuza siku ya Sabato? Nikiwa katika miaka ya ujana wangu, nilijifunza kazi za wengine ambazo ziliorodhesha vitu vya kufanya na vya kutofanya siku ya Sabato. Haikuwa hadi baadaye ndipo nikajifunza kutoka katika maandiko kwamba mwenendo wangu na mtazamo wangu juu ya Sabato vilikuwa ishara kati yangu mimi na Baba yangu wa Mbinguni [ona Kutoka 31:13; Ezekieli 20:12, 20]. Kwa uelewa huo, sikuhitaji tena orodha ya vya kufanya na kutofanya. Nilipohitaji kufanya uamuzi kama shughuli ilikuwa ya kufaa au kutofaa kwa ajili ya Sabato, nilijiuliza mwenyewe, ‘Ni ishara gani ninataka kumwonyesha Mungu?’”

Kuabudu katika siku ya Bwana huonyeshwa na fokasi maalumu juu ya dhabihu ya Yesu Kristo ya kulipia dhambi. Sisi kwa usahihi kabisa na mahususi tunasherehekea Ufufuko Wake siku ya Pasaka lakini pia kila wiki tunapopokea ishara za sakramenti ya Upatanisho Wake, ikijumuisha Ufufuko Wake. Kwa mwenye kutubu, kupokea sakramenti ni onyesho kuu la kuabudu siku ya Sabato.

Kuabudu pamoja kama “mwili wa Kristo” kuna nguvu ya kipekee na faida tunapofundishana, kuhudumiana na kusaidiana sisi kwa sisi. Cha kupendeza, utafiti mmoja wa hivi karibuni uligundua kwamba kwa wale wanaoyatazama maisha yao kiroho kama ni yao tu yawezekana wakashindwa kuweka kipaumbele cha ukuaji wa kiroho au kusema kwamba imani yao ni muhimu sana, au kuwa na muda wa mara kwa mara wa ibada na Mungu. Kama jumuiya ya Watakatifu, tunaimarishana sisi kwa sisi katika kuabudu na katika imani.

Hata hivyo, hatuwezi kusahau matendo ya kila siku ya kuabudu ambayo tunayafanya binafsi na nyumbani. Mwokozi anatukumbusha, “Hata hivyo nadhiri zako zitatolewa katika haki siku zote na kwa nyakati zote.” Dada mmoja kwa hekima alisema, “Siwezi kufikiria njia nzuri zaidi ya kumwabudu Mungu kuliko kuwakaribisha watoto Wake wadogo katika maisha yetu na kuwatunza na kuwafundisha mpango Wake kwa ajili yao.”

Alma na Amuleki waliwafundisha Wazoramu ambao walikuwa wamezuiliwa kuingia katika masinagogi kumwabudu Mungu siyo tu mara moja kwa wiki lakini siku zote, “na mahali popote wanapoweza kuwa.” Walisema kuhusu sala ni kama kuabudu:

“Mfungue roho zenu ndani ya vijumba vyenu, na mahali penu pa siri, na kwenye nyika zenu.

“Ndiyo, na wakati hamumlilii Bwana, hebu mioyo yenu ijae, mdumu katika sala kwake siku zote”.

Pia walizungumzia juu ya kupekua maandiko, kutoa ushuhuda juu ya Kristo, matendo ya hisani na huduma, kupokea Roho Mtakatifu, na kuishi kwa shukrani kila siku. Zingatia wazo hilo: “kuishi kwa shukrani kila siku.” Huzungumzia dhana yangu ya pili:

Mitazamo na Hisia Zinazopatikana katika Kuabudu

Kuhisi na kuelezea shukrani kwa Mungu, kwa kweli, ndicho kinacholeta kuabudu pamoja na hisia za kufanywa upya kwa shangwe kinyume na kuona kama ni jambo moja zaidi la wajibu.

Ibada ya kweli inamaanisha kumpenda Mungu na kuyaweka mapenzi yetu Kwake—ni zawadi ya thamani tunayoweza kutoa Alipoulizwa amri ya kwanza ni ipi katika sheria yote, Yesu alijibu, “Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa akili zako zote.” Yeye pia ameiita hii ni amri kuu.

Huu ulikuwa mpangilio wa kuabudu Kwake mwenyewe kwa Baba. Maisha Yake na dhabihu Yake ya kulipia dhambi viliwekwa wakfu kwa utukufu wa Baba. Kwa uchungu sisi tunakumbuka maombi ya Yesu yanayogusa moyo katikati ya mateso na uchungu usiyofikirika: “Baba yangu, ikiwezekana kikombe hiki kiniepuke,” lakini kisha utiifu Wake, “walakini si kama nitakavyo mimi, bali utakavyo wewe.”

Kristo akiwa Gethsemane.

Kuabudu ni kujitahidi kufuata mfano huu mkamilifu. Sisi hatutafikia ukamilifu katika jambo hili kwa usiku mmoja, lakini ikiwa kila siku “tutatoa dhabihu [Kwake] moyo uliovunjika na roho iliyopondeka,” Yeye atatubatiza tena kwa Roho Wake na kutujaza neema Yake.

Tatu, Upekee wa Kuabudu Kwetu

Katika sehemu ya kwanza ya Mafundisho na Maagano, Bwana anatangaza mashtaka haya ya ulimwengu:

“Kwani wamepotoka kutoka kwenye ibada zangu, na wamevunja agano langu lisilo na mwisho;

“Hawamtakii Bwana kuendeleza haki zake, bali kila mtu huenenda katika njia zake mwenyewe, na akifuata mfano wa mungu wake mwenyewe, ambaye ni mfano wa kitu cha duniani.”

Ni vyema kwetu sisi kukumbuka mfano wa Wayahudi watatu vijana Hanania, Mishaeli na Azaria, waliochukuliwa mateka Babeli muda mfupi baada ya Lehi na familia yake kuondoka Yerusalemu. Ofisa wa Kibabeli aliwapa majina mapya ya Shadraka, Meshaki na Abednego. Baadaye, watatu hawa walipokataa kusujudia sanamu iliyowekwa na Mfalme Nebukadreza, aliamuru kwamba watupwe ndani ya tanuru la moto, akiwaambia, “Naye ni nani Mungu yule atakayewaokoa ninyi na mikono yangu?”

Unaweza kukumbuka jibu lao la ujasiri:

“Mungu wetu tunayemtumikia aweza kutuokoa na tanuru ile iwakayo moto, naye atatuokoa na mkono wako, Ee Mfalme.

“Lakini kama si hivyo, ijulikane kwako … ya kuwa sisi hatukubali kuitumikia miungu yako, wala kuisujudia hiyo sanamu ya dhahabu uliyoisimamisha.”

Shadraka, Meshaki na Abednego waliokolewa katika lile tanuru la moto mkali.

Tanuri lilikuwa na moto mkali uliowaua wale waliowatupa mle ndani, lakini Shadraka, Meshaki na Abed-nego walikuwa hawajadhurika. “Kisha Nebukadreza alizungumza, na kusema, Na ahidimiwe Mungu wa Shadraka, Meshaki, na Abed-nego, ambaye … amewakomboa watumishi wake ambao walimwamini, … na kutoa miili yao, ili wasipate kumtumikia wala kumwabudu mungu ye yote isipokuwa Mungu wao wenyewe.” Walimtumaini Yehova kwa ajili ya ukombozi, “lakini kama siyo,” ambayo ni, hata kama Mungu katika hekima Yake asingezuia vifo vyao, bado wangebaki wakweli kwake Yeye.

Chochote kinachochukua kipaumbele juu ya kumwabudu Baba na Mwana” kinakuwa ni sanamu. Wale wanaomkataa Mungu kama chanzo cha ukweli au kukataa uwajibikaji wowote kwake Yeye, kwa hakika wao wenyewe wanakuwa kama mungu wao. Mtu anayeweka uaminifu kwa kikundi au sababu mbele ya uelekeo wa kiungu anaabudu mungu wa uongo. Hata wale wanaokusudia kumwabudu Mungu lakini hawashiki amri Zake wanatembea katika njia zao wenyewe: “Wanajongea karibu nami kwa midomo yao, lakini mioyo yao iko mbali nami.” Lengo la kuabudu kwetu ni la kipekee kwa “Mungu pekee wa kweli, na Yesu Kristo, ambaye [Yeye] amemtuma.”

Mwisho, Haja ya Kufuata mfano wa Baba na Mwana

Mwishowe, jinsi tunavyoishi yawezekana kuwa ndiyo bora, aina halisi zaidi ya kuabudu. Kuonyesha mapenzi yetu inamaanisha kufuata mfano wa Baba na Mwana—tukikuza sifa na tabia zao ndani yetu. Ikiwa, kama inavyosemwa, kuiga ni namna ya kujipendekeza kwa dhati kabisa, basi tunaweza kusema kwa heshima kwa Mungu, kufuata mfano ni aina ya heshima zaidi. Hii inapendekeza jitihada kamili, inayokubalika kwa upande wetu ya kutafuta utakatifu. Lakini kuwa zaidi kama Kristo pia ni matokeo ya kiasili kabisa ya matendo yetu ya kuabudu. Kirai cha Mzee Kearon alichokitoa mapema kuhusu kuabudu, “katika njia ambayo inatubadilisha” ni cha kipekee. Kuabudu kiukweli ni ya kubadilisha.

Huu ndio uzuri wa njia ya agano—njia ya kuabudu, upendo na uaminifu kwa Mungu. Tunaingia njia hiyo kwa ubatizo, tukiahidi kujichukulia juu yetu jina la Kristo na kushika amri Zake. Tunapokea kipawa cha Roho Mtakatifu, mjumbe wa neema za Mwokozi ambazo zinakomboa na kutuosha kutokana na dhambi pale tunapotubu. Tungeweza hata kusema kwamba katika kutubu tunamwabudu Yeye.

Kisha hufuata ibada za ukuhani za ziada na maagano yanayofanyika katika nyumba ya Bwana ambayo yanatutakasa zaidi sisi. Sherehe hizi na ibada za hekaluni zinaunda aina ya juu zaidi ya kuabudu.

Rais Russell M. Nelson amesisitiza kwamba “kila mwanaume na kila mwanamke ambaye anashiriki katika ibada za ukuhani na ambaye anafanya na kushika maagano na Mungu anao ufikiaji wa moja kwa moja wa nguvu za Mungu.” Hii siyo tu ile nguvu tunayoichota ili kuhudumu na kubariki. Pia ni nguvu ya kiungu ambayo inatenda kazi ndani yetu ili kutuosha na kututakasa. Tunapotembea katika njia ya agano, ile “nguvu itakasayo ya uchamungu inadhihirika” ndani yetu.

Basi sisi, kama Wanefi na Walamani wa kale, ‘tuanguke chini miguuni mwa Yesu … kumwabudu.” Sisi, kama ilivyoamriwa na Yesu, “tuanguke chini na kumwabudu Baba katika jina la [Mwana].” Na tupokee Roho Mtakatifu na kufungua mioyo yetu kwa Mungu, tusiwe na miungu wengine mbele yake Yeye, na kama wanafunzi wa Yesu Kristo tuige tabia Zake katika maisha yetu wenyewe. Ninashuhudia kwamba tufanyapo haya, tutapata uzoefu wa shangwe katika kuabudu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.