2025
Shangwe Kupitia Ufuasi wa Agano
Mei 2025


10:58

Shangwe Kupitia Ufuasi wa Agano

Tunapojifunga wenyewe na kutenda kama wafuasi wa agano, katika kiwango cha uwezo wowote ule, uhusiano wetu na Baba na Mwana unarutubishwa, shangwe yetu inaongezeka na mtazamo wetu wa milele unapanuka.

Siku moja mnamo 2023, Uyanga Altansukh alikuwa anafanya kazi kaskazini mwa jiji la Darkhan Mongolia wakati rais wa misheni ya Mongolia alipoingia sehemu yake ya kazi. Kwa maneno yake:

“Nilimwona na niliwaza alikuwa na nuru hii angavu katika uso wake. Alikuwa mkarimu sana na mcheshi kwa wale waliomzunguka na nilihisi ukunjufu. Kabla hajaondoka, nilimuuliza baadhi ya maswali. Siku chache baadaye, alikuja kazini kwangu tena na kuniomba kama ningehudhuria kanisa lake. Nilidhani ingekuwa jambo la kufaa. Nilikuwa na wasiwasi kwa ajili ya kesho ya watoto wangu, kwani jamii ilionekana kujawa na msongo wa hisia na giza. Nilitaka watoto wangu wawe kama mtu huyu aliye na nuru katika nyuso zao, wakisambaza shangwe kwa wengine wanaowazunguka.

“Siku moja wamisionari walitufundisha sheria ya zaka. Watoto wangu walisema kwa msisimko,‘Mama, sisi lazima tulipe zaka yetu.’ Niliweza kuona imani ya watoto wangu wakati ule. Kabla sijajiunga na Kanisa, nilitazama mkutano mkuu na kumsikiliza Rais Russell M. Nelson akizungumza. Alitangaza mahekalu mapya kote ulimwenguni na kusema kwamba hekalu jipya litajengwa katika Ulaanbaatar, Mongolia. Nilifurahi na kutokwa na machozi, ingawa sikuelewa ni kwa nini. Kwa shangwe hii, ningeweza kueleza kwamba imani yangu na ushuhuda wangu vilikuwa vinakua.”

Uyanga, kama mamilioni wengine, ni sehemu ya mkusanyiko mkubwa wa Israeli katika maandalizi ya Ujio wa Pili wa Yesu Kristo. Ameanza safari yake katika njia ya agano na amekuwa mfuasi wa Kristo. Inamaanisha nini kuwa mfuasi wa Kristo? Ninathamini neno la Kijapani la mfuasi—deshide ikimaanisha kaka mdogo na shi ikimaanisha mtoto.

Yesu Kristo alitangaza, “Hapo mwanzo nilikuwepo na Baba, na Mimi ndiye Mzaliwa wa Kwanza.” Kwa sababu ya Yeye ni nani na kile ambacho amekifanya, tunamwabudu Yeye, tunamheshimu, tunamtukuza na tunamfuata Yeye. Kristo ametukomboa sisi, na tuna shukrani daima kwa ajili ya dhabihu Yake isiyo na mwisho na ya upatanisho.

Tuna Baba wa Mbinguni, ambaye anatupenda sisi kama watoto Wake. Upendo Wake kwetu ni mkamilifu. Yesu Kristo na misheni Yake inaonyesha upendo Wake kwa ajili yetu. Kama Yohana alivyoandika, “Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe wa pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele.”

Katika hamu yetu ya kuelewa kile tusichokijua, tunaweza wakati mwingine kutegemea uzoefu wetu wa duniani, au vitu tunavyovijua. Kwa mfano, tunaweza kujifunza kiasi fulani juu ya Mungu Baba kupitia uzazi wetu wenyewe na mahusiano ya kifamilia ya duniani. Hata hivyo, tunapaswa kuwa waangalifu katika kutumia mifanano hii sana katika jaribio letu la kumwelewa Baba yetu wa Mbinguni. Sifa za Mungu Baba zinazidi sifa za mwanadamu yeyote mwenye mapungufu na aliyeanguka. Mungu Baba ni Baba mkamilifu. Yeye anapenda kwa ukamilifu, ni mkarimu, mwenye subira, na anaelewa na ni mtukufu kikamilifu. Tunaweza kumtumainia Yeye kikamilifu. Upendo wa Kristo huakisi upendo wa Mungu Baba na ni mwakilishi wa upendo huo.

Yesu Kristo ni vyote mfano na njia. Katika Kristo, tunaweza kuelewa vyema sifa kamili za Baba na mpango Wake. Kupitia Kristo, tumepatiwa nguvu wezeshi za kushinda uelekeo wa wanaume na wanawake wa asili ili kwamba tuweze kuwa zaidi kama Baba.

Kama tu vile Baba yetu wa Mbinguni, Yesu Kristo ni mwenye rehema na haki kamilifu. Hizi sifa za kiungu za haki na rehema hazipo katika upinzani. Sifa hizi zinakamilishana. Vyote haki na rehema huonyesha upendo kamili wa Mungu kwa watoto Wake. Tunaweza kuwatumainia Mungu Baba na Yesu Kristo kwa sababu Wao ni wenye haki na wema kwetu sote.

Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, wamefungamana kikamilifu katika madhumuni na upendo. Kwa sababu Mungu na Yesu Kristo wanatupenda, tumepatiwa fursa na fadhila za kama wanafunzi wa kweli ili kufanya maagano na Wao. Kwa kufanya hivyo kwetu, uhusiano wetu na Kristo unapanuka: “Na sasa, kwa sababu ya agano lile ambalo mmefanya mtaitwa watoto wa Kristo, wanawe, na mabinti zake; kwani tazama, siku hii amewazaa kiroho; kwani mnasema kwamba mioyo yenu inabadilishwa kwa imani katika jina lake; kwa hivyo, amewazaa na mkawa wanawe na mabinti zake.”

Kama wanafunzi, tunapofanya na kushika maagano, tunabarikiwa kwa nguvu ya kiroho. Tunaunganika na Kristo na Mungu Baba katika uhusiano maalum na tunaweza kupata uzoefu wa upendo Wao na shangwe katika kipimo kilichotengewa wale ambao wamefanya na kushika maagano. Uwezo wetu wa kuhisi kipimo kamili cha upendo wa Mungu, au kuendelea katika upendo Wake, unategemeana na hamu na matendo yetu ya haki.

Katika Yohana sura ya 15, mstari wa 9, tunasoma, “Kama vile Baba alivyonipenda mimi, ndivyo nami nilivyowapenda ninyi.” Na kisha tunapatiwa mwaliko: “kaeni katika pendo langu.”

Katika mstari unaofuata, tunapewa njia ya kuendelea katika upendo Wake: “Mkizishika amri zangu, mtakaa katika pendo langu; kama vile mimi nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.”

Sisi kisha tunaona dhumuni la kushika amri katika mstari wa 11: “Hayo nimewaambia, ili furaha yangu iwe ndani yenu, na furaha yenu itimizwe.”

Kupitia ufuasi wa kweli wa agano, tunaweza kuanza kuelewa vyema asili ya Mungu na shangwe ambayo Yeye hutaka watoto Wake wote wapate. Tunaweza pia kuanza kuelewa baadhi ya kanuni ambazo hapo mwanzo zilionekana kukanganya. Kwa mfano, ni kwa jinsi gani Mungu ana utimilifu wa shangwe wakati baadhi ya watoto Wake wanateseka sana? Jibu lipo katika mtazamo mkamilifu wa Mungu na katika mpango Wake mkamilifu. Yeye hutuona kutoka mwanzo hadi uwezekano wetu wa utukufu wa hapo baadaye. Yeye ametoa njia, kupitia Mwanawe Yesu Kristo, kwa ajili yetu sote, watoto Wake, ya kushinda maumivu, mateso, dhambi, hatia na upweke wa maisha ya duniani. Mungu ametoa kwa ajili yetu njia na chaguo.

Mifano ya wale ambao wamepata uzoefu wa shangwe kupitia ufuasi inaweza kutusaidia kuelewa vyema dhana hii. Pengine umesikia kirai hiki kwamba tuna furaha tu kama vile mtoto wetu asiye na furaha. Nimeona kwamba hili halihitaji kuwa hivyo. Mama yangu mwenye umri wa miaka 94 ana zaidi ya wazawa 200 walio hai. Wakati wowote ule, angalau mmoja wa hawa 200 atakuwa hana furaha. Kama kauli hii ni kweli, mama yangu angekuwa katika hali ya kila siku ya kukosa furaha, wakati sivyo hivyo. Wale wanaomjua wanajua jinsi alivyo na shangwe.

Sasa nitashiriki uzoefu mwingine. Mnamo Januari ya 2019, mimi pamoja na mke wangu, Debbie, tulialikwa kwenye ofisi ya Rais Nelson. Alikuwa ameweka kiti chake karibu nasi, na tuliketi magoti yetu yakikaribia yake. Baada ya kutupatia wito wetu wa sasa, Rais Nelson alimgeukia Debbie na kufokasi kwake. Alikuwa mkarimu, mwenye upendo, mpole na aliyejawa na shangwe, kama baba mkamilifu au babu. Aliushikilia mkono wa Debbie na kuugonga taratibu, akimhakikishia kwamba itakuwa SAWA na kwamba familia yetu ingebarikiwa. Ilionekana kwetu wakati ule kwamba sisi tulikuwa watu muhimu sana kwake na kwamba yeye alikuwa na wakati wote ulimwenguni kwa ajili yetu. Tuliondoka ofisini kwake mchana ule wa Ijumaa tukihisi hakikisho, kupendwa na wenye shangwe.

Jumatatu tuliona habari. Wakati siku ile ile ambayo Rais Nelson alikuwa pamoja nasi, mmoja wa mabinti zake alikuwa amefariki kutokana na saratani. Tulishangaa. Mioyo yetu ilijaa tulipoomboleza kwa ajili yake na familia yake. Mioyo yetu pia ilijawa na shukrani kwa ajili ya usikivu wake wa kama Kristo kwetu hali akiomboleza binti yake ambaye alikuwa anateseka.

Tulipotafakari uzoefu huu, tulijiuliza wenyewe, “Ni kwa jinsi gani yeye angekuwa mkarimu hivi, mwenye upendo, na hata mwenye shangwe katika wakati mgumu kama huu?” Jibu ni kwa sababu yeye anajua. Anajua kwamba Kristo amekuwa mshindi. Anajua atakuwa binti yake tena na atakuwa naye milele yote. Shangwe na mtazamo wa milele huja kupitia kuunganishwa kwa Mwokozi kwa kufanya na kushika maagano na kupitia ufuasi wa kama Kristo.

Rais Nelson amefundisha: “Kama vile Mwokozi anavyotoa amani ambayo ‘inapita akili yote,’ [Wafilipi 4:7], Yeye pia anatoa kiwango, kina, upana wa furaha ambayo inapita uelewa wa mwanadamu au uelewa wa kimwili. Kwa mfano, inaonekana haiwezekani kuwa na furaha wakati mtoto wetu anapoumwa na ugonjwa usiotibika, au unapopoteza kazi yako, au mwenza wako anapokusaliti. Hata hivyo hiyo ndiyo furaha anayotoa Mwokozi.”

Tunapofanya na kushika maagano, sisi kiasili tunageukia kuwa na shauku ya kuwasaidia wengine kuhisi kipimo cha shangwe na upendo tunaohisi katika uhusiano wetu wa kimaagano. Tunaweza kuwa sehemu ya hii kazi kubwa sana hapa ulimwenguni leo—kuikusanya Israeli. Tunaweza kuwaleta watoto wa Mungu kwa Kristo. Kama vile nabii Yakobo alivyofundisha: “Na heri ninyi; kwani kwa sababu mmekuwa na bidii katika kutumikia na mimi katika shamba langu la mizabibu, na mmetii amri zangu, na kuniletea tena matunda ya kawaida, … mtapokea shangwe na mimi kwa sababu ya matunda ya shamba langu la mizabibu.”

Tunapojifunga wenyewe na kutenda kama wafuasi wa agano, katika kiwango cha uwezo wowote ule, uhusiano wetu na Baba na Mwana unarutubishwa, shangwe yetu inaongezeka na mtazamo wetu wa milele unapanuka. Kisha sisi tunavikwa na nguvu na tunaweza kuhisi shangwe katika kipimo kilichotengewa kwa ajili ya wafuasi wa kweli wa agano wa Mungu. Katika jina takatifu la Yesu Kristo, amina.

Muhtasari

  1. Mafundisho na Maagano 93:21.

  2. Ona Mathayo 1:21; 2 Nefi 2:6

  3. Yohana 3:16.

  4. Mosia 5:7.

  5. Ona Russell M. Nelson, “Agano Lisilo na Mwisho,” Liahona, Okt. 2022, 4–11.

  6. Ona Dale G. Renlund, “Experience God’s Love” (Brigham Young University devotional, Dec. 3, 2019), speeches.byu.edu.

  7. Yohana 15:9–11.

  8. Ona Alma 7:11–13.

  9. Russell M. Nelson, “Shangwe na Kunusurika Kiroho,” Liahona,, Nov. 2016, 82.

  10. Ona Russell M. Nelson, “Hope of Israel” (worldwide youth devotional, June 3, 2018), Gospel Library.

  11. Yakobo 5:75.

  12. Ona “Hesed, God’s Covenant Love, Is the Reason We Build Temples and Perform Ordinances: Instruction from President Russell M. Nelson,” general conference leadership meeting, Oct. 2024, Gospel Library.