“Mzee B. Corey Cuvelier,” Liahona, Mei 2025.
Mzee B. Corey Cuvelier
Sabini Mkuu mwenye Mamlaka
Wakati Mzee B. Corey Cuvelier alipotangaza kuwa anaondoka kwenye kazi yake na kuwa rais wa misioni kwa ajili ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho, wenzake waliuliza, “Je, wewe ni mwendawazimu?”
Mzee Cuvelier alisema wenzake walipata shida kuelewa kwa nini angeacha kazi yake nzuri kwa miaka mitatu. Lakini maswali yao yalikuwa fursa, alisema, “kushiriki kwa nini tunafanya kile tunachofanya na kwa nini tunaamini kile tunachoamini na katika nani tunaamini. Huyo ni Yesu Kristo.”
Brian Corey Cuvelier alizaliwa Januari 12, 1969, huko Los Angeles, California, ambako aliasiliwa na kulelewa. Baba yake, Heinz Joachim Cuvelier, alikuwa afisa wa polisi. Mama yake, Joann Leslie Jarnecke Cuvelier, alikuwa mtunza nyumba. Yeye ni mtoto wa kwanza kati ya watoto wanne.
Kama mmisionari kijana, Mzee Cuvelier alihudumu katika Misioni ya Brazil São Paulo South. Alihitimu kutoka Chuo Kikuu cha Brigham Young mwaka 1994 akiwa na shahada katika mahusiano ya umma. Alijiunga na Kampuni ya Mafuta ya Shell mnamo 1996, ambako alifanya kazi katika vitengo mbalimbali vya biashara vya Amerika ya Kaskazini.
Mzee Cuvelier alimuoa Wendi Sue Manwaring mnamo Julai 18, 1992, katika Hekalu la Los Angeles California. Wao ni wazazi wa wavulana wanne. Akina Cuvelier walihudumu kama viongozi wa misioni katika Misioni ya Brazil Curitiba South kuanzia mwaka 2016 hadi 2019 na walikuwa wakiishi Katy, Texas, wakati wa wito wake.
Hapo awali, Mzee Cuvelier alihudumu kama Sabini wa Eneo katika Amerika ya Kaskazini Eneo la Kusini Magharibi, rais wa kigingi, mshauri katika urais wa kigingi, mjumbe wa baraza kuu, askofu, mshauri katika uaskofu, na rais wa Wavulana katika kata.