Ripoti ya Idara ya Kanisa ya Ukaguzi wa Mahesabu, 2024
Kwa Urais wa Kwanza wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho
Ndugu Wapendwa: Tukiongozwa na ufunuo, kama ilivyorekodiwa katika sehemu ya 120 ya Mafundisho na Maagano, Baraza la Mpangilio wa Zaka—linalojumuisha Urais wa Kwanza, Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, na Uaskofu Simamizi—huidhinisha matumizi ya fedha za Kanisa. Idara za Kanisa hutoa fedha kwa mujibu wa bajeti, sera, na taratibu zilizoidhinishwa.
Ukaguzi wa mahesabu ya Kanisa, ambao unaojumuisha wataalamu walioidhinishwa na huru kutoka kwenye idara zingine zote za Kanisa na vitengo, una wajibu wa kufanya ukaguzi wa mahesabu kwa lengo la kutoa uhakika kuhusu michango iliyopokelewa, matumizi yaliyofanywa, na ulinzi wa mali za Kanisa.
Kwa kuzingatia ukaguzi uliofanywa, Ukaguzi wa Mahesabu ya Kanisa unatoa msimamo kwamba, katika nyanja zote, michango iliyopokelewa, matumizi yaliyofanywa, na mali za Kanisa kwa mwaka 2024 vimerekodiwa na kusimamiwa kwa mujibu wa bajeti ya Kanisa, sera, na utendaji wa kiuhasibu ulioidhinishwa. Kanisa linafuata utendaji uliofundishwa kwa waumini wake wa kuishi ndani ya bajeti, kuepuka madeni, na kuweka akiba kwa ajili ya wakati wa uhitaji.
Kwa heshima imewasilishwa,
Idara ya Kanisa ya Ukaguzi wa Mahesabu
Jared B. Larson
Mkurugenzi Mtendaji