Kujiamini Katika Uwepo wa Mungu
Wakati kwa bidii tunapotafuta kuwa na hisani na wema kujaza maisha yetu, kujiamini kwetu kwenye kusonga karibu na Mungu kutaongezeka.
Wapendwa wangu akina kaka na akina dada, nina shukrani kuzungumza nanyi leo kwenye mkutano huu mkuu muhimu. Macho yangu yanazidi kuzeeka. Asanteni kwa uelewa wenu wakati ninapotoa ujumbe wangu.
Tunaishi kwenye siku yenye kasi kuu ya ukuaji wa Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Ninajazwa na shangwe wakati nionapo maendeleo katika maeneo mengi.
Ninavutiwa hasa na vijana. Wanatoa huduma kwa idadi kubwa. Wanawatafuta mababu zao na kufanya ibada hekaluni. Vijana wetu wa kiume na wa kike wanawasilisha maombi kwa ajili ya huduma ya umisionari kwa idadi kubwa. Kizazi chipukizi kinainuka kama wafuasi imara wa Yesu Kristo.
Hivi karibuni nilikutana na kitukuu wangu mpya wa kike. Ninapotafakari changamoto atakazopitia maishani mwake, ninahisi hamu kubwa ya kumsaidia kujenga imani yake katika Yesu Kristo. Kuishi injili ya Yesu Kristo ni muhimu kwa ajili ya furaha yake ya baadae.
Kitukuu wangu, kama kila mmoja wetu, atakutana na changamoto. Tutapitia magonjwa, kukata tamaa, majaribu na hasara. Changamoto hizi zinaweza kupoteza kujiamini kwetu binafsi. Hata hivyo, wafuasi wa Yesu Kristo wana uwezo wa kufikia aina tofauti ya kujiamini.
Wakati tunapofanya maagano na Mungu na kuyashika, tunaweza kupata kujiamini kunakozaliwa kwa roho. Bwana alimwambia Nabii Joseph Smith kwamba kujiamini kwetu kunaweza “kuwa imara mbele za Mungu.” Fikiria faraja ya kuwa na kujiamini mbele za Mungu!
Wakati ninapoongelea kuhusu kuwa na kujiamini mbele za Mungu, ninarejelea kuwa na kujiamini kumwendea Mungu sasa hivi! Ninarejelea kwenye kusali kwa kujiamini kwamba Baba wa Mbinguni hutusikia, kwamba Yeye huelewa mahitaji yetu vyema zaidi kuliko sisi. Ninarejelea kwenye kuwa na kujiamini kwamba Yeye hutupenda zaidi ya tunavyoweza kuelewa, kwamba Yeye hutuma malaika kuwa pamoja nasi na wale tuwapendao. Ninarejelea kuwa na kujiamini kwamba Yeye anatamani kumsaidia kila mmoja wetu kufikia uwezekano wetu wa juu zaidi wa jinsi tunavyoweza kuwa.
Sasa, tunapataje kujiamini huko? Bwana anajibu swali hilo kwa maneno haya: “Na moyo wako … ujae hisani kwa wanadamu wote, … na wema uyapambe mawazo yako bila kukoma; ndipo kujiamini kwako kutakuwa imara katika uwepo wa Mungu.”
Huu ndio ufunguo! Katika maneno ya Bwana mwenyewe, hisani na wema hufungua njia ya kuwa na kujiamini katika uwepo wa Mungu! Akina kaka na akina dada, tunaweza kufanya vitu hivi! Kujiamini kwetu kweli kunaweza kuwa imara katika uwepo wa Mungu, sasa hivi!
Acha tutafakari vyote viwili hisani na wema.
Kwanza, hisani. Miaka miwili iliyopita, niliwaalika, kama wanafunzi wa agano wa Yesu Kristo, kuwa wapatanishi. Ninarudia nilichokisema wakati ule: “Hasira kamwe haishawishi. Uhasama haumjengi yeyote yule. Ubishi kamwe hauleti suluhisho lenye mwongozo.
Hisani ya kweli kwa watu wote ni kielelezo cha wapatanishi! Ni muhimu sana kwamba tuwe na hisani kwenye mazungumzo yetu, kote kwenye umma na binafsi. Ninawashukuru wale kati yenu ambao mliweka ushauri wangu uliopita mioyoni mwenu. Lakini bado tunaweza kufanya vizuri zaidi.
Uhasama uliopo sasa kwenye mazungumzo ya umma na mitandao ya kijamii ni wa kuashiria hatari. Maneno ya chuki ni silaha za maangamizi. Mabishano humzuia Roho Mtakatifu kuwa mwenza wetu daima.
Kama wafuasi wa Yesu Kristo, tunapaswa kuonyesha njia kama wapatanishi. Wakati hisani inapokuwa sehemu ya asili yetu, tutaepuka ushawishi wa kuwadhalilisha wengine. Tutaacha kuwahukumu wengine. Tutakuwa na hisani kwa wote wenye hali tofauti tofauti. Hisani kwa watu wote ni muhimu kwa ajili ya ukuaji wetu. Hisani ni msingi wa sifa ya uungu.
Acha tumsihi Baba yetu wa Mbinguni atujaze mioyo yetu na hisani kuu—hasa kwa wale ambao ni vigumu kuwapenda.—kwani hisani ni zawadi kutoka kwa Baba yetu wa Mbinguni kwa wafuasi wa kweli wa Yesu Kristo. Mwokozi ni Mwana Mfalme wa Amani. Tunapaswa kuwa vyombo Vyake kwa ajili ya amani.
Sasa, acha tuongelee kuhusu wema. Bwana anatuambia tuyapambe mawazo yetu kwa wema daima. Fikiria msaada utakaoupokea kwa ajili ya wazo lolote chanya unapolikuza kwa wema. Wema hufanya kila kitu kuwa kizuri zaidi na cha furaha zaidi! Kwa upande mwingine, fikiria nini kitatokea wakati unapoongeza wema kwenye wazo lisilo jema, wazo la kikatili, au wazo la kuleta huzuni. Wema utayaondoa mawazo hayo. Wema utakufanya huru dhidi ya mawazo ya hofu na ya kutatiza.
Akina kaka na akina dada, wakati uovu unaongezeka zaidi ulimwenguni, tunahitaji kuongezeka kwenye wema. Mawazo yetu, maneno na matendo yanahitajika kuwa na wema usioshindwa na kujazwa na upendo msafi wa Kristo kwa wanadamu wote. Fursa kuu mbele yetu ni ya kuwa watu ambao Mungu anatutaka tuwe.
Kuabudu mara kwa mara kwenye nyumba ya Bwana huongeza uwezo wa vyote hisani na wema. Hivyo, wasaa hekaluni huongeza kujiamini kwetu katika uwepo wa Bwana. Wasaa zaidi ndani ya nyumba ya Bwana utatusaidia kujiandaa kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Mwokozi, Yesu Kristo. Hatujui siku au saa ya ujio Wake. Lakini ninajua kwamba Bwana ananipa msukumo kutusihi tuwe tayari kwa ajili ya siku ile “iliyo kuu na ya kuogofya.”
Wakati kwa bidii tunapotafuta kuwa na hisani na wema kujaza maisha yetu, kujiamini kwetu kwenye kusonga karibu na Mungu kutaongezeka. Ninawaalika kuchukua hatua za makusudi za kukua katika kujiamini kwenu katika uwepo wa Bwana. Kisha, tunapokwenda kwa Baba yetu wa Mbinguni tukiwa na ongezeko la kujiamini, tutajazwa kwa shangwe zaidi, na imani yenu katika Yesu Kristo itaongezeka. Tutaanza kupata uzoefu wa nguvu ya kiroho ambayo huzidi matumaini yetu makuu.
Tunamshukuru Bwana kwa ongezeko la ujenzi wa mahekalu katika miaka ya hivi karibuni. Kupitia mwongozo Wake, leo tunatangaza mipango ya kujenga hekalu kwenye kila moja ya maeneo haya 15:
-
Reynosa, Mexico
-
Chorrillos, Peru
-
Rivera, Uruguay
-
Campo Grande, Brazil
-
Porto, Portugal
-
Uyo, Nigeria
-
San Jose del Monte, Philippines
-
Nouméa, New Caledonia
-
Liverpool, Australia
-
Caldwell, Idaho
-
Flagstaff, Arizona
-
Rapid City, South Dakota
-
Greenville, South Carolina
-
Norfolk, Virginia
-
Spanish Fork, Utah
Ninashuhudia kwamba Yesu Kristo, Mkombozi wa Israeli, huongoza hili Kanisa, Kanisa Lake. Anajiandaa kurudi tena. Na iwe vivyo hivyo kwetu kujiandaa kumpokea. Juu ya hilo ninasali katika jina la Yesu Kristo, amina.