Baraka za Kufidia
Huku hali nyingi katika maisha zinaweza kuwa nje ya udhibiti wetu, lakini hakuna yeyote kati yetu asiyeweza kufikiwa na baraka za Bwana zisizo na kikomo.
Kuhudumu katika Uaskofu Kiongozi, nimekuwa na fursa ya kukutana na Watakatifu wa Siku za Mwisho kote ulimwenguni katika maeneo na tamaduni tofauti. Nimekuwa nikiendelea kuvutiwa na imani yetu ya kudumu na kujitolea kwa Bwana Yesu Kristo. Lakini pia nimeguswa na hali tofauti na mara nyingi ngumu ambazo wengi wenu mnakabiliana nazo—changamoto kama vile ugonjwa, ulemavu, uchache wa rasilimali, fursa chache za ndoa au elimu, unyanyasaji unaofanywa na wengine, na vizuizi vinginevyo au vipingamizi. Nyakati fulani, majaribu haya yanaweza kuonekana kuzuia maendeleo yako na kujaribu jitihada zako za dhati za kuishi injili kikamilifu, ikifanya kuwa vigumu zaidi kuhudumu, kuabudu na kutimiza majukumu matakatifu.
Marafiki zangu wapendwa, kama utahisi kupungukiwa au kukatishwa tamaa na hali za maisha yako, nataka ujue hili; Bwana anakupenda wewe binafsi. Anajua hali zako, na mlango wa baraka Zake unabaki wazi kwako bila kujali changamoto unazokabiliwa nazo.
Nimejua ukweli huu kupitia uzoefu binafsi ambao, ingawa unaonekana usio wa kipekee, umeacha alama ya kudumu kwangu. Katika umri wa miaka 22, wakati nikihudumu katika Jeshi la Anga la Ufaransa huko Paris, nilifurahishwa kujua kwamba Mzee Neal A. Maxwell, Mtume wa Bwana, angeongea katika mkutano huko Champs-Élysées. Hata hivyo, kabla tu ya tukio hili, nilipokea amri ya kumwendesha ofisa mwandamizi kwenda uwanja wa ndege katika muda ule ule ambao mkutano ulipangwa kufanyika.
Nilikuwa nimevunjika moyo. Nikidhamiria kuhudhuria, nilimshusha ofisa yule na kuwahi kwenye mkutano. Baada ya kupata mahali pa kuegesha gari, nilikimbia haraka kuelekea Champs-Elysées mahali pa mkutano na niliwasili nikiwa sina pumzi zikibaki dakika tano tu kabla ya mkutano kumalizika. Nilipoingia tu, nilimsikia Mzee Maxwell akisema, “Sasa nitawapeni baraka za kitume.” Katika wakati huo, nilipata uzoefu kiroho mzuri, usiosahalika. Nilizidiwa na Roho na maneno ya baraka yalionekana kupenya kila nyuzi ya nafsi yangu kana kwamba yalikuwa yamekusudiwa kwa ajili yangu mimi tu.
Kile nilichokipitia siku ile kilikuwa kidogo lakini dhihirisho lenye nguvu la kipengele cha kufariji cha mpango wa Mungu kwa ajili ya watoto Wake: Wakati hali zilizo nje ya uwezo wetu wa kudhibiti zinapotuzuia kutimiza matamanio yetu ya haki ya mioyo yetu, Bwana atafidia katika njia zinazoturuhusu sisi kupokea baraka Zake zilizoahidiwa.
Ukweli huu wa kutia moyo umejikita katika kanuni tatu muhimu zinazopatikana katika injili ya urejesho ya Yesu Kristo:
-
Mungu anampenda kila mmoja wetu kikamilifu. “Anatualika [sisi] sote kuja Kwake na kupokea wema Wake.” Mpango Wake wa ukombozi unahakikisha kwamba kila mmoja, pasipo tofauti, atapewa fursa ya haki ya siku moja kupokea baraka za wokovu na kuinuliwa.
-
Kwa sababu Mungu ni mwenye haki na mwenye huruma na mpango Wake ni mkamilifu, Yeye hatatuwajibisha kwa vitu vilivyo nje ya udhibiti wetu. Mzee Neal A. Maxwell alieleza kwamba “Mungu … anazingatia siyo tu tamaa zetu na matendo yetu, bali pia viwango vya ugumu ambavyo hali zetu tofauti huziweka juu yetu.”
-
Kupitia Yesu Kristo na Upatanisho Wake, sisi tunaweza kupata nguvu ya kuvumilia na mwishowe kuzishinda changamoto zote za maisha yetu. Kama Alma alivyofundisha, Mwokozi alijichukulia juu Yake siyo tu dhambi za wenye kutubu, bali pia “maumivu na magonjwa ya watu wake” na “mapungufu yao.” Hivyo, zaidi ya kutukomboa sisi kutokana na makosa yetu, rehema na neema ya Bwana inatusaidia sisi kupitia kukosekana kwa haki, na vizuizi vinavyotokana na uzoefu wetu wa duniani.
Kupokea baraka hizi za kufidia huja na masharti kadhaa. Bwana anatutaka tufanye “yote tuwezayo” na “kutoa nafsi [yetu] yote kama matoleo Kwake.” Hii inahitaji hamu ya kina, moyo wa dhati na wa uaminifu, na bidii ya juu kabisa katika kushika amri Zake na kuoanisha mapenzi yetu na Yake.
Jitihada zetu za dhati zinapokuwa pungufu ya matamanio yetu kutokana na hali zilizo nje ya uwezo wetu, Bwana anaweza bado akakubali matamanio ya mioyo yetu kama matoleo yenye kustahili. Rais Dallin H. Oaks alifundisha, “Tutabarikiwa kwa matamanio ya haki ya mioyo yetu hata kama baadhi ya hali za nje zimefanya isiwezekane kwa sisi kutimiza matamanio hayo kwa vitendo.”
Wakati Nabii Joseph Smith alipokuwa na wasiwasi kuhusu kaka yake, ambaye alikuwa amefariki dunia pasipo kupokea ibada muhimu za injili, alipokea ufunuo wenye kufariji: “Wale wote watakaokufa sasa na kuendelea bila kuifahamu [injili] ambao wangeliipokea kwa moyo wao wote, watakuwa warithi wa [selestia wa Mungu].” Kisha Bwana akaongeza, “Kwani Mimi Bwana nitawahukumu watu wote kulingana na matendo yao, kulingana na tamaa za mioyo yao.”
Lililo muhimu kwa Bwana siyo tu kama tunaweza bali kama tuko tayari kufanya yote tunayoweza ili kumfuata Yeye kama Mwokozi wetu.
Wakati mmoja rafiki alikuwa akimfariji mmisionari kijana juu ya kupumzishwa kwake mapema kutokana na sababu za kiafya, licha ya sala zake za dhati na hamu yake ya dhati ya kuhudumu. Rafiki huyu alishiriki andiko ambalo ndani yake Bwana alitamka kwamba watoto Wake “wanapokwenda kwa nguvu zao zote” na “hawaachi juhudi yao” ili kutimiza amri Zake, “na adui zao [ambao wanaweza kujumuishwa hali mbalimbali katika maisha yetu] zinawazuia kutimiza kazi hiyo, tazama inanilazimu Mimi kutoitaka tena kazi hiyo mikononi mwao [watu] hao bali kuyakubali matoleo yao.”
Rafiki yangu alimshuhudia kijana yule kwamba Mungu alijua kuwa yeye ametoa chake kilicho bora katika kujibu wito wa kuhudumu. Alimhakikishia kwamba Bwana amepokea matoleo yake na kwamba baraka zilizoahidiwa kwa wamisionari wote waaminifu hazitazuiliwa.
Baraka za Bwana za kufidia mara nyingi huja kupitia ukarimu na huduma ya wengine ambao wanatusaidia kukamilisha kile ambacho hatuwezi kufanya sisi wenyewe. Ninakumbuka wakati ambapo, tulikuwa tukiishi mbali na binti yetu huko Ufaransa, tulihisi kutokuweza kumsaidia baada ya uzazi mgumu. Wiki hiyo hiyo, kata yetu hapa Utah walitafuta msaada kwa ajili ya mama aliyejifungua watoto mapacha. Mke wangu, Valérie, alijitolea kumletea chakula, akiwa na sala moyoni kwa wote wawili mama huyu mzazi mpya na binti yetu aliye katika uhitaji. Muda mfupi baadaye, tulijua kwamba akina dada katika kata ya binti yetu huko Ufaransa walikuwa wamejipanga kutoa chakula kwa ajili ya familia ya binti yetu. Kwetu sisi, Mungu alikuwa amejibu sala zetu, akiwatuma malaika Zake kupeleka faraja wakati sisi tulipokuwa hatuwezi.
Wakati unapokabiliwa na mapungufu na changamoto, na tutambue baraka zetu wenyewe —zawadi zetu, rasilimali na muda—na tuvitumie kuwahudumia wale walio katika uhitaji. Katika kufanya hivyo, siyo tu tutawabariki wengine bali kualika uponyaji na fidia katika maisha yetu wenyewe.
Mojawapo ya njia zenye nguvu zaidi tunazoweza kuchangia kwenye baraka za kufidia za Mungu ni kupitia kazi ya uwakilishi tunayofanya kwa ajili ya mababu zetu katika nyumba ya Bwana. Tunapofanya ibada kwa niaba yao, kikamilifu tunashiriki katika kazi kuu ya wokovu, tukitumia vipaji vyetu na uwezo ili kutoa baraka kwa wale ambao hawakupata fursa ya kuzipokea wakati wa maisha yao ya duniani.
Huduma ya upendo tunayotoa katika mahekalu matakatifu hutukumbusha kwamba neema ya Mwokozi inaendelea kupita maisha haya. Katika maisha yajayo, yawezekana tukapewa fursa mpya ya kukamilisha kile ambacho hatukuweza kukamilisha katika maisha ya duniani. Nikizungumzia kuhusu akina dada ambao bado hawajawapata wenzi wa milele, Rais Lorenzo Snow kwa upendo alisema: “Hakuna Mtakatifu wa Siku za Mwisho anayekufa akiwa ameishi maisha ya uaminifu ambaye atapoteza chochote kwa sababu ya kushindwa kufanya mambo fulani wakati ambapo fursa hazikuruhusu yeye kufanya hivyo. … Watakuwa na baraka zote, kuinuliwa na utukufu ambako mwanaume au mwanamke yeyote watakuwa navyo ambao walipata fursa hii.”
Ujumbe huu wa matumaini na faraja ni kwa ajili yetu sisi sote, watoto wa Mungu. Hakuna hata mmoja wetu anayeweza kuepuka changamoto na mapungufu ya duniani. Zaidi ya yote, sisi sote tumezaliwa na mapungufu ya kurithi ya kujiokoa wenyewe. Hata hivyo tunaye Mwokozi mwenye upendo, na “tunajua kwamba kwa neema [Yake] tunaokolewa, baada ya kutenda yote tunayoweza.”
Ninashuhudia kwamba hali nyingi katika maisha zinaweza kuwa nje ya udhibiti wetu, lakini hakuna yeyote kati yetu asiyeweza kufikiwa na baraka za Bwana zisizo na kikomo. Kupitia dhabihu Yake ya kulipia dhambi, Mwokozi atafidia kwa kila kukosekana kwa uwezo na kukosekana kwa haki kama tutatoa nafsi yetu yote Kwake. Katika jina la Yesu Kristo, amina.