2025
Nyuma ya Matukio: Huduma za Ukalimani na Huduma za Wageni
Mei 2025


“Nyuma ya Matukio: Huduma za Ukalimani na Huduma za Wageni,” Liahona, Mei 2025.

Nyuma ya Matukio: Huduma za Ukalimani na Huduma za Wageni

Wikiendi moja kila baada ya miezi sita tunafurahia mkutano mkuu. Lakini nyuma ya matukio, maelfu ya wafanyakazi wa kujitolea na wafanyakazi wa Kanisa hufanya kazi kwa miezi kadhaa ili kufanya mkutano uweze kufanyika.

Wanaandaa kila kitu ili kutangaza jumbe za kinabii kwa mamilioni ya watu ulimwenguni kote. Hapa ni mtazamo mdogo wa kazi hii kubwa.

Huduma za Ukalimani

Timu mia moja na arobaini na tatu za lugha ulimwenguni kote zinafanya ukalimani wa hotuba za mkutano mkuu kwa wakati halisi ili waumini waweze kusikiliza bila kuchelewa katika lugha zao za asili. Ni timu 57 tu zinazofanya ukalimani huo kutokea makao makuu ya Kanisa katika Jiji la Salt Lake.

Ukalimani unatofautiana na tafsiri, ambayo inahusisha kubadilisha maneno yaliyoandikwa kuwa lugha nyingine. Kwa ukalimani, timu za lugha lazima ziwe tayari kufanyia ukalimani mabadiliko ya dakika za mwisho na maoni yanayotolewa kwenye mimbari. Wakalimani huwasaidia waumini ulimwenguni kote kuisikia injili katika ndimi zao za asili (ona Mafundisho na Maagano 90:11).

Huduma za Wageni

Kama umehudhuria mkutano mkuu katika Jiji la Salt Lake, Marekani, umegundua waelekezaji wanaokuelekeza kwenye kiti chako. Takribani wamisionari 400 huko Temple Square wanajitolea takribani masaa 9,000 katika kipindi chote cha mkutano mkuu ili kuwasaidia wageni kuingia na kutoka kwenye Kituo cha Mkutano bila shida.

Wanawaongoza wageni 20,000 kwa kila kikao cha mkutano mkuu. Mara baada ya kikao kumalizika, wanafanya kazi kuwaongoza wageni nje haraka iwezekanavyo ili waweze kusafisha njia kwa wengine kuhudhuria kikao kinachofuata.