Upatanisho wa Yesu Kristo Hutoa Uokoaji wa Msingi
Tunapomgeukia Yesu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu, Yeye anatuokoa kutokana na dhoruba za maisha kupitia Upatanisho Wake.
Upatanisho wa Yesu Kristo hutoa uokoaji wa mwisho kutokana na majaribu tunayokabiliana nayo katika maisha haya. Rais Russell M. Nelson alinipangia kazi ya kuweka wakfu Hekalu la Casper Wyoming mwishoni mwa mwaka uliopita. Lilikuwa tukio kubwa, la kihisia na la kiroho. Lilileta katika fokasi ya wazi kazi inayofanywa na mahekalu katika kuwaokoa watoto wa Mungu kupitia Upatanisho wa Mwokozi.
Vigingi katika wilaya ya Hekalu la Casper Wyoming hujumuisha sehemu ya njia ya nchi kavu iliyotumiwa na waanzilishi Watakatifu wa Siku za Mwisho kati ya 1847 na 1868. Katika kujiandaa kwa ajili ya uwekaji wakfu, wa hekalu, nilisoma upya baadhi ya historia ya njia hii kando ya Mto Platte karibu na Casper kuendelea kwenda Jijini Salt Lake. Njia hii ilikuwa njia ya kupita kwa mamia ya maelfu ya wahamiaji wa magharibi. Msisitizo wangu wa msingi ulikuwa kwa zaidi ya waanzilishi Watakatifu wa Siku za Mwisho 60,000 waliosafiri katika njia hii.
Waanzilishi wetu wengi walikuja kwa mikokoteni ya kukokotwa na farasi au maksai, lakini takribani watu 3,000 walivuka katika kombania kumi za mikokoteni ya kusukumwa kwa mkono. Kombania nane za mikokoteni hii ya kusukuma kwa mikono walipita njia hii ya kukumbukwa kwa mafanikio na vifo vichache. Kombania za mikokoteni ya kusukuma kwa mkono za Willie na Martin za mwaka 1856 zilikuwa za kipekee.
Nilirejelea hadithi za kombania za mikokoteni hii ya kusukuma kwa mkono za Willie na Martin kuanzia wakati ule hali mbaya ya hewa ilipoanza. Nikawa nafahamu kwa undani changamoto waliyokabiliana nayo kwenye kuvuka Mto wa Sweetwater, Ghuba ya Martins, Rocky Ridge na Rock Creek Hollow.
Between Stoms, na Albin Veselka
Sikuwahi kuingia ndani ya Hekalu la Casper kabla ya uwekaji wakfu huu. Wakati nilipoingia kwenye ukumbi, umakini wangu ulivutwa mara moja kwenye picha ya kuchorwa ya mkokoteni halisi wenye jina Between Storms. Kwa uwazi kabisa mchoro ule haukukusudiwa kuonyesha majanga yale yaliyotokea. Nilipoitazama kwa karibu, nilifikiria, “Mchoro huu wa rangi ulikuwa sahihi; idadi kubwa ya waanzilishi wa mikokoteni hawakupitia majanga haya.” Sikuweza kujizuia kuhisi kwamba hii ni kama maisha kwa ujumla. Wakati mwingine tunakuwa katikati ya dhoruba na wakati mwingine katikati ya mawingu na mwangaza wa jua.
Heaven’s Portal, na Jim Wilcox
Wakati nilipogeukia ile picha halisi kwenye ukuta mwingine, iliyopewa jina la Heaven’s Portal, nilitambua kwamba picha hii nzuri ya kiangazi ya kile kilichoitwa “Devil’s Gate,” yenye Mto Sweetwater mtulivu na msafi ukitiririka kupitia hapo, uliwasilisha urembo wa uumbaji wa Bwana, siyo tu changamoto ambazo waanzilishi walikabiliana nazo katika yale majira ya kutisha ya baridi.
Kisha nilitazama mbele, nyuma ya dawati la vibali vya hekaluni, nikaona picha nzuri ya kuchora ya Mwokozi. Hii mara moja ilizua hisia nyingi za shukrani. Katika ulimwengu wenye uzuri mwingi, pia kuna changamoto nyingi. Tunapomgeukia Yesu Kristo, Mwokozi wa ulimwengu, Yeye anatuokoa kutokana na dhoruba za maisha kupitia Upatanisho Wake kulingana na mpango wa Baba.
Kwangu mimi, ukumbi ule ulikuwa maandalizi kamili kwa ajili ya vyumba vya ibada za hekaluni ambavyo huturuhusu sisi kupokea ibada za kuinuliwa, kufanya maagano matakatifu, na kikamilifu kukubali na kuonja baraka za Upatanisho wa Mwokozi. Mpango wa furaha wa Baba umejikita kwenye uokoaji wa Mwokozi wa kulipia dhambi.
Tukio hili la waanzilishi linawapa Watakatifu wa Siku za Mwisho desturi ya kihistoria ya kipekee na urithi wa pamoja wenye nguvu za kiroho. Kwa baadhi, uhamiaji umekuwa kwa miaka mingi baada ya kufukuzwa kwa nguvu kutoka kote Missouri na Nauvoo. Kwa wengine ulianza baada ya Rais Brigham Young kutangaza mpango wa mikokoteni ya kusukuma kwa mkono, ambao ulikusudiwa kufanya uhamiaji kuwa wenye kuwezekana. Mikokoteni ya mkono ina gharama ndogo kuliko mikokoteni ya farasi na madume ya ng’ombe.
Mmisionari huko Uingereza, Millen Atwood, alisema wakati mpango huu wa mkokoteni wa mikono ulipotangazwa, “ulikimbia kama moto kwenye makapi makavu, na mioyo ya Watakatifu masikini iliruka kwa shangwe na furaha.” Wengi “walikuwa wamesali na kufunga siku hadi siku, na usiku hadi usiku ili wapate nafasi ya kuungana na kaka zao na dada zao huko milimani.”
Wengi wa Watakatifu wa mikokoteni ya mkono walipitia magumu lakini waliepuka matukio mabaya makubwa. Lakini kombania mbili za mikokoteni ya mikono, kombania ya Willie na kombania ya Martin, zilipitia baa la njaa, kupigwa na hali ya hewa ya baridi kali na vifo vingi.
Wengi wa wasafiri hawa, walisafiri kwa njia ya bahari kutoka Liverpool, Uingereza, mwezi Mei 1856 wakipanda meli mbili. Waliwasili kwenye eneo la kuvalia nguo za mikokoteni huko Mji wa Iowa mwezi Juni na Julai. Licha ya maonyo, kombania zote mbili ziliondoka kwa safari ya Bonde la Salt Lake wakiwa wamechelewa sana katika msimu huo.
Rais Brigham Young alikuja kujua kwa mara ya kwanza juu ya hali hiyo hatarishi ya kombania hizi mbili mnamo Oktoba 4, 1856. Siku iliyofuata alisimama mbele ya Watakatifu wa Siku za Mwisho na kusema, “Wengi wa kaka zetu na dada zetu wako mbugani wakiwa na mikokoteni ya kusukuma kwa mkono, … na ni lazima waletwe hapa; lazima tutume usaidizi kwao … kabla ya majira ya baridi kuanza.”
Aliomba maaskofu kutoa timu 60 za nyumbu, magari 12 ya kukokotwa na farasi au zaidi, na tani 12 za unga, na kutangaza, “Nendeni na muwalete wale watu ambao sasa wako mbugani.”
Idadi ya jumla ya waanzilishi waliokuwa katika kombania za Willie na Martin ilikadiriwa kuwa watu 1,100. Watu wapatao 200 kati ya Watakatifu hawa wa thamani walifariki wakiwa njiani. Pasingelikuwa na uokoaji huu wa wakati muafaka, wengi zaidi wangeangamiana.
Dhoruba hii ya majira ya baridi ilianza wiki mbili baada ya waokoaji wa kwanza kuondoka Jiji la Salt Lake. Hadithi za washiriki wa kombania za Willie na Martin zinaelezea changamoto mbaya baada ya dhoruba kuanza. Hadithi hizi pia zinaonyesha shangwe kubwa pale waokoaji walipowasili.
Wakielezea mazingira ya kuwasili kwao, Mary Hurren alisema: “Machozi yalitiririka mashavuni kwa wanaume, na watoto walio cheza dansii kwa shangwe. Watu walipoweza kudhibiti hisia zao, wote walipiga magoti chini kwenye barafu na kutoa shukrani kwa Mungu.”
Siku mbili baadaye, kombania ya Willie ilipaswa kusafiri sehemu ngumu zaidi ya njia hii, kuvuka Rocky Ridge, katika dhoruba ya baridi kali. Mtu wa mwisho hakufika kambini hadi saa 11:00 alfajiri ya siku iliyofuata. Watu kumi na watatu walikufa na wakazikwa katika kaburi la pamoja.
Mnamo Novemba 7, kombania ya Willie ilikuwa inakaribia Bonde la Salt Lake, lakini asubuhi ile, bado kulikuwa na vifo vitatu. Siku mbili baadaye, kombania ya Willie mwishowe iliwasili Salt Lake, mahali ambapo walipata mapokezi ya kupendeza na kukaribishwa katika nyumba za Watakatifu.
Siku hiyo hiyo, kombania ya Martin ilikuwa bado maili 325 (km 523) nyuma njiani, wakiendelea kuteseka na baridi na upungufu wa chakula. Siku kadhaa baadaye, walivuka Mto Sweetwater ili kufikia kile ambacho sasa kinaitwa Ghuba ya Martin, mahali ambapo walitumaini kupata ulinzi kutokana na hali mbaya. Mmoja wa waanzilishi alisema, “Ilikuwa ni uvukaji mbaya zaidi wa mto katika safari yao.” Baadhi ya waokoaji, kama vile babu wa baba yangu, David Patten Kimball, ambaye alikuwa na umri wa miaka 17 tu, sambamba na marafiki zake vijana, “George W. Grant, Allen Huntington, Stephen Taylor na Ira Nebeker, walitumia saa nyingi ndani ya maji yaliyoganda,” kwa ushujaa wakiwasaidia kombania kuweza kuvuka maji ya Sweetwater.
Wakati tukio hili limepokea umakini mku wa sana, kadiri nilivyojifunza mengi kuhusu waokoaji hawa, niligundua kwamba hawa wote walikuwa wakimfuata nabii na kufanya kazi muhimu katika kuwaokoa Watakatifu waliokwama. Waokoaji wote walikuwa mashujaa, kama walivyokuwa wahamiaji hao.
Kwa kujifunza hadithi yao, ilinifanya nithamini uhusiano wao wa thamani na ono la milele la muda mrefu miongoni mwa wahamiaji John na Maria Linford na wana wao watano walikuwa washiriki wa kombania ya Willie. John alifariki saa kadhaa kabla ya waokoaji wa kwanza kuwasili. Alikuwa amemwambia Maria kwamba alikuwa amefurahi kwamba walifanya safari hiyo. “Mimi sitakuwa hai kufika Salt Lake,” alisema, “ lakini wewe na wavulana mtafika, na sijutii yale yote tuliyoyapitia kama wavulana wetu wataweza kukua na kulea familia zao katika Sayuni.”
Rais James E. Faust alitoa muhtasari huu wakupendeza “Katika juhudi za kishujaa za waanzilishi wa mikokoteni ya mkono, tunajifunza ukweli mkuu. Wote lazima wapitie moto wa msafishaji, na visivyo na maana na visivyo na umuhimu katika maisha yetu vinayeyuka kama dongo la chuma na kufanya imani yetu ing’ae, kamili na imara. Kunakuwepo na kipimo kamili cha uchungu, huzuni na mara nyingi kuvunjika moyo kwa kila mtu, ikijumuisha wale ambao kwa dhati wanatafuta kufanya vyema na kuwa waaminifu. Ndiyo hii ni sehemu ya kusafishwa ili kumjua Mungu.”
Katika Upatanisho na Ufufuko Wake wenye kutengeneza umilele, Mwokozi alikata “kamba za kifo akiwa amepata ushindi dhidi ya mauti” kwa ajili ya kila mtu. Kwa wale walio tubu dhambi, Yeye “amejitwika mwenyewe maovu yao na makosa yao, baada ya kuwakomboa, na kutosheleza madai ya haki.”
Pasipo Upatanisho, hatuwezi kujiokoa wenyewe kutokana na dhambi na kifo. Wakati dhambi inaweza kufanya kazi ya kipekee katika majaribu yetu, shida za maisha zinachangiwa na makosa, maamuzi mabaya, matendo maovu ya wengine na mambo mengi yaliyo nje ya udhibiti wetu.
Hubiri Injili Yangu inafundisha: “Tunapomtegemea Yesu Kristo na Upatanisho Wake, Yeye anaweza kutusaidia kuvumilia majaribu yetu, magonjwa na uchungu. Tunaweza kujawa na shangwe, amani na faraja. Yale yote ambayo si haki juu ya maisha yanaweza kufanywa kuwa sahihi kupitia Upatanisho wa Yesu Kristo.”
Wakati huu wa majira ya Pasaka, fokasi yetu ni juu ya Mwokozi na dhabihu Yake ya kulipia dhambi. Upatanisho unatoa matumaini na nuru wakati ambapo kwa wengi huona giza na woga. Rais Gordon B. Hinckley alitamka, “Wakati historia yote imechunguzwa, … hakuna kitu kilicho cha ajabu sana, kikuu sana na kikubwa zaidi kama kitendo hiki cha neema.”
Ninashiriki mapendekezo matatu ambayo nafikiri yanahusika kipekee kwa siku yetu.
Kwanza, usidharau umuhimu wa kufanya kile tunachoweza ili kuwaokoa wengine kutokana na changamoto za kimwili na hususani za kiroho.
Pili, kwa shukrani kubali Upatanisho wa Mwokozi. Sisi sote tunapaswa kuonyesha shangwe na furaha hata kama tunakabiliwa na changamoto za maisha. Lengo letu linapaswa kuwa kuishi kwa matumaini kwenye upande wa jua wa mtaa. Nimemwangalia mwenzi wangu wa thamani, Mary, akifanya hili katika maisha yake yote. Nimethamini njia yake inayong’ara, yenye kuinua hata pale tulipokabiliwa na matatizo miaka yote.
Ushauri wangu wa tatu ni kutenga muda endelevu wa kutafakari kwa uaminifu Upatanisho wa Mwokozi. Kuna njia nyingi za kufanya hili katika maadhimisho yetu binafsi ya kidini. Hata hivyo, kuhudhuria mkutano wa sakramenti na kupokea sakramenti ni muhimu hasa.
Lililo na umuhimu sawa ni uhudhuriaji wa mara kwa mara hekaluni pale inapowezekana. Hekalu linatoa kumbukumbu endelevu ya Upatanisho wa Mwokozi na kile upatanisho ilichoshinda. Na, hata la muhimu zaidi, uhudhuriaji hekaluni unaruhusu sisi kutoa uakoaji wa kiroho kwa ajili ya wapendwa wetu waliofariki dunia na mababu zetu wa mbali zaidi.
Rais Russell M. Nelson, katika mkutano wetu wa mwisho, alisisitiza kanuni hii na kuongeza, baraka za “[hekalu] … husaidia kuwaanda watu ambao watasaidia kuuandaa ulimwengu kwa ajili ya Ujio wa Pili wa Bwana!”
Lazima tusisahau ile dhabihu na mifano ya vizazi vilivyotangulia, lakini kusifu kwetu, kuthamini na kuabudu kunapaswa kulenga kwa Mwokozi wa ulimwengu na dhabihu yake ya kulipia dhambi. Ninashuhudia kwamba muhimu kwenye mpango wa furaha wa Baba ni Upatanisho uliofanywa na Mwokozi wetu Yesu Kristo. Yeye yu hai na analiongoza Kanisa Lake. Upatanisho wa Yesu Kristo hutoa uokoaji wa mwisho kutoka kwenye majaribu tunayokabiliana nayo katika maisha haya. Katika jina la Yesu Kristo, amina.