“Mzee Michael Cziesla,” Liahona, Mei 2025.
Mzee Michael Cziesla
Sabini Mkuu mwenye Mamlaka
Mzee Michael Cziesla anakumbuka mapambano ya mwaka 2017 vizuri sana. Siku ya Jumanne mwezi Januari, alipoteza ajira yake kwenye kampuni ya sheria ya kimataifa wakati kampuni hiyo ilipotangaza kufilisika. Siku iliyofuata nyumba yake ilifurika wakati bomba la maji lilipopasuka. Wezi walipora vitu kwenye nyumba yake siku ya tatu wakijaribu kuchukua vitu vya thamani vya familia. Katika siku chache, maisha yake yaligeuka juu chini.
“Nilitabasamu Jumapili ile kama kawaida nilipokaa kwenye jukwaa kama rais wa kigingi,” alisema. “Hakuna aliyejua kilichokuwa kinaendelea. Lakini ndani nilikuwa na huzuni sana. Nilikuwa katika mahali penye giza nene.”
Baada ya mkutano, mtu mtulivu, mpole katika kata alimwuliza ana tatizo gani. “Alisikiliza tu, na kisha akanikumbatia,” Mzee Cziesla alisema. “Nilihisi Bwana akinikumbatia, kwamba Yeye alijua taabu yangu, kwamba yote yangekuwa sawa.”
Michael Cziesla alizaliwa kwa Armin Ludwig na Irmtraut Hanna huko Neumünster, Ujerumani, mnamo Julai 26, 1972. Alikulia huko Schleswig-Holstein na baadaye alihudumu katika Misioni ya Utah Ogden. Mke wake, Margret Anne Rauh, alihudumu katika Misioni ya Temple Square. Walioana katika Hekalu la Frankfurt Ujerumani mnamo Aprili 4, 1997. Wakati wa wito wake, walikuwa wakiishi na watoto wao watano huko Griesheim, Ujerumani, ambapo walifurahia kuzunguka misituni na mapumziko ya likizo katika kisiwa huko Denmark.
Mzee Cziesla alipata shahada ya sheria kutoka Chuo Kikuu cha Mainz mwaka 2000. Alikamilisha kazi yake ya sheria kama mshirika mwandamizi wa ushirika wa McDermott Will & Emery.
Kabla ya wito wake kama Sabini Mkuu mwenye Mamlaka, Mzee Cziesla alihudumu kama Sabini wa Eneo katika Eneo la Ulaya ya Kati, rais wa misioni ya mpito katika Misioni ya Ujerumani Frankfurt, rais wa kigingi, mshiriki wa baraza kuu, na mshauri katika uaskofu.