Mbele ya Macho Yetu
Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linakua kwa waumini na familia, misheni na wamisionari, nyumba za mikutano na mahekalu.
Akina kaka na dada, ninashukuru sana kuwa pamoja nanyi. Tunawapenda, tunashukrani kwenu; na tunahisi kubarikiwa kwa sala zenu.
Rais Russell M. Nelson alisema kwenye mkutano wetu uliopita: “Je, mnaona kinachoendelea mbele ya macho yetu sasa? Ninasali kwamba hatutakosa utukufu wa wakati huu! Bwana kwa hakika anaharakisha kazi Yake.”
Kuharakisha kazi Yake. “Kuharakisha” ni neno lenye maana. Linapendekeza kusonga haraka, kutia kasi, na hata uharaka. Katika ukuaji wa Kanisa na mpango wa Kristo, kuharakisha kunatokea. Na sisi sote tu sehemu yake.
Mnamo Aprili 1834 huko Kirtland, Ohio, Nabii Joseph Smith aliwakusanya wote wenye ukuhani katika nyumba ndogo ya shule karibia futi 14 (4.2m) za mraba. Tungeweza kujaza dazani za nyumba zile za shule kwenye ukumbi huu wa mikutano, na kubaki na nafasi. Joseph Smith alisema, “Ni wachache tu wenye Ukuhani mnaoweza kuwaona hapa usiku wa leo, lakini Kanisa hili litaijaza Amerika ya Kaskazini na Kusini—litaijaza dunia.”
Unabii huo unatimizwa “mbele ya macho yetu sasa.” Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho linakua kwa waumini na familia, misheni na wamisionari, nyumba za mikutano na mahekalu, na katika usajili wa seminari zetu, vyuo, na vyuo vikuu kote ulimwenguni.
Tunashukuru kuwepo duniani wakati Kanisa linaongezeka kwa idadi na ushawishi, lakini muhimu zaidi katika mioyo na maisha ya waumini wake. Sisi tunajulikana kama wanafunzi wa Yesu Kristo. Tunashiriki shuhuda zetu kuhusu Yeye, Kanisa Lake, njia Zake, na njia Yake ya agano. Sisi ni watu Wake, na Yeye ndiye Mwokozi wetu.
Ninastaajabishwa na kile Rais Nelson anachokiita “ukuu wa wakati huu” na kutoa shukrani kubwa kwa Bwana kwa kazi Yake. Ninawahimiza kusimama wima kama wanafunzi Wake, mashahidi wanaona wa utimilifu wa unabii, wa kale na wa sasa.
Kuna wapinzani ambao wanapiga kelele, “‘Lo, huku!’ na … ‘Lo, kule!’” kama walivyofanya wakati wa Nabii Joseph Smith. Hata hivyo, wao ni na watakuwa tu tanbihi katika kazi hii nzuri. Kumbuka maneno ya Joseph Smith: “Hakuna mkono usiofaa unaoweza kuzuia kazi kuendelea; Mateso yanaweza kuja kwa ghadhabu … lakini ukweli wa Mungu utasonga mbele kwa ujasiri, uadilifu, na kwa uhuru, hadi utakapopenya kila bara, kufikia kila tabia nchi, kufagia kila nchi, na kusikika na kila sikio, hadi pale makusudi ya Mungu yatakapokamilishwa, na Yehova mkuu atakaposema kazi imekamilika.”
Katika majukumu yangu mwaka huu, nimekuwa mstari wa mbele kwenye “kuharakisha kazi Yake. Kanisa linajenga mahekalu kwa kasi isiyo na kifani, na kuwapa waumini fursa zaidi ya kuabudu katika nyumba ya Bwana. Pili, kazi ya ummisionari inakusanya idadi kubwa kwenye zizi la Mchungaji Mwema, Yesu Kristo. Na tatu, elimu ya Kanisa katika maumbo mengi na iko katika kiwango cha juu kipya kwa wale ambao “wanamtafuta Yesu huyu.”
Leo Kanisa lina mahekalu 367 katika hatua mbalimbali za usanifu, ujenzi, au utendaji. Na ni kwa lengo gani? Jibu linatangazwa kwenye kila hekalu: “Utakatifu kwa Bwana.” Hekalu linafungua njia ya baraka za juu zaidi ambazo Baba yetu wa Mbinguni anazo kwa kila mmoja wetu. Akina kaka na dada, tunaharakisha “utakatifu” wetu tunapokuwa wastahiki kuingia hekaluni, tunapoabudu katika nyumba ya Bwana, na tunapofanya maagano na Mungu kwa ajili yetu wenyewe na kwa niaba ya mababu zetu upande wa pili wa pazia.
Rais Nelson amesema: “Mashambulizi ya adui yanaongezeka kwa kasi, kwa ukubwa na kwa namna mbalimbali. Hitaji letu la kuwa hekaluni mara kwa mara halijawahi kuwa kubwa kama hivi leo. Ninawasihi mtazame kwa sala jinsi mnavyotumia muda wenu.” Katika nyumba Yake, tunaweza kuhisi uwepo mtakatifu wa Bwana na amani ipitayo zote.
Mwaka uliopita nilipewa heshima ya kusimamia uwekaji wakfu Hekalu la Mendoza Argentina. Katika ujumbe wangu, nilirejelea unabii wa Mzee Melvin J. Ballard wa mwaka 1926 kwamba kazi ya Bwana kwa muda ingekua taratibu huko Amerika Kusini, “kama vile mwaloni unavyochipukia taratibu kutoka mbegu. Haitakuwa kubwa kwa,” lakini maelfu wangejiunga na Kanisa, na mataifa ya Amerika Kusini yangekuwa “nguvu katika Kanisa.” Niliona unabii huo unatimizwa mbele ya macho yangu.
Mendoza, awali ikiwa mbegu ndogo, imekuwa mwaloni mkubwa. Ukuaji huo unajirudia ulimwenguni kote na kwenye visiwa vya bahari.
Tunaona Bwana anaharakisha kazi Yake katika misheni. Katika mwaka 2024, wamisionari 80,000 walikuwa wanahudumu katika misheni 450. Thelathini na sita kati ya hizo ni misheni mpya. Mwaka jana huduma ya ummisionari ilileta waumini wapya Kanisani zaidi ya 308,000. Zaidi ya idadi, roho ya kukusanyika analeta nafsi kwa Yesu Kristo na injili Yake.
Ninafikiria juu ya Mitume Brigham Young na Heber C. Kimball, ambao mnamo 1839 walianza safari kama wamisionari kwenda Visiwa vya Uingereza. Walikuwa wagonjwa; waliacha familia zikiwa wagonjwa na maskini. Hata hivyo, wawili hao walipanda kwenye gari, na wakiwa bado mbele ya wapendwa wao, Heber alisema, “Wacha tuinuke na tuwape furaha.” Wawili hao walijitahidi kusimama na kupiga kelele, “Huree, huree kwa Israeli.”
Niliona shauku hiyo hiyo kwenye kazi ya Bwana huko Lima, Peru, nilipokutana na wamisionari kutoka Kituo cha Mafunzo ya Wamisionari na misheni huko Lima. Ni ya kupendeza kiasi gani! Niliona uharakishaji mbele ya macho yangu. Sasa kuna misheni saba katika jiji la Lima pekee.
Mwishoni mwa mkutano wetu, wamisionari walinishangaza. Waliinuka na kushangilia, “Huree kwa Israeli.” Sitaweza kusahau wakati huo; natamani iwapo ninyi nyote mngekuwepo pale. Mbele ya macho yangu walikuwa wamisionari ambao walikuwa wameweka kando “vitu vya ulimwengu huu” ili kumtumikia Bwana na kusaidia kuharakisha ujio Wake.
Tunamwona Bwana akiharakisha fursa za elimu kwa waumini wetu na hata wale wasio wa imani yetu ulimwenguni kote. Mojawapo ya vitu ambavyo hututofautisha sisi kama kanisa ni msisitizo wetu wa elimu. Bwana aliamuru katika siku za mwanzo wa Urejesho “kutafuta maarifa, hata kwa kujifunza na pia kwa imani.” Hiyo inatokea leo na inastahili “huree” kubwa.
Hivi sasa zaidi ya wanafunzi 800,000 ulimwenguni kote wameandikishwa katika seminari na chuo, uandikishaji wa juu zaidi katika historia ya Kanisa. Vijana wetu hukusanyika kwa njia mbalimbali, kuanzia madarasa ya asubuhi na mapema, wakati wa mchana, na madarasa ya jioni hadi mtandaoni na masomo ya nyumbani. Wao ni kikosi chenye nguvu na kitakatifu, wakipata nguvu kutoka kwa kila mmoja wanapojifunza juu ya Yesu Kristo, kumfuata, na kushuhudia kuhusu Yeye kama Mwana wa Mungu.
Msimu uliopita nilizungumza kwenye ibada kwenye uwanja uliojaa wanafunzi wa seminari na chuo na wazazi wao katika Chuo Kikuu cha Utah. Mahudhurio yao yalisema mengi juu ya hamu yao ya kumjua na kumfuata Yesu Kristo. Ujumbe wangu kwa wanafunzi hao ulikuwa wazi: Mpe Bwana muda sawa. Niliwashauri kusawazisha masomo yao na elimu ya kweli mafunzo ya juu, hata mafunzo ya “Mwana wa Mungu aliye hai.”
Ninahimiza vivyo hivyo kwa kila mtu leo: Chochote kilicho kwenye orodha yako ya “kufanya”, toa muda sawa, sio muda wa ziada, kwa Bwana katika kujifunza maandiko kibinafsi, kujifunza Njoo, Unifuate, kama familia, sala, miito ya Kanisa, huduma, kushiriki sakramenti, kuabudu hekaluni, na kutafakari mambo ya Mungu. Bwana na Mwokozi wetu amesema, “Jifunzeni kwangu … nanyi mtapata pumziko la nafsi zenu.” Muamini Yeye kwa neno Lake. Na Mpeni muda sawa.
Rais Nelson amesema: “Ninawasihi kumwacha Mungu ashinde katika maisha yenu. Mpe sehemu nzuri ya wakati wako. Unapofanya hivyo, tambua kile kinachotokea kwenye kasi yako chanya ya kiroho.”
Tunaona kasi hiyo ikiongezeka katika seminari, vyuo, na vyuo vikuu vya Kanisa. Katika mazingira haya, Bwana ni kipaumbele. Vivyo hivyo Yeye anapaswa kuwa katika maisha ya kila moja.
Eneo lingine ambalo linaonyesha kuongezeka kwa elimu katika Kanisa ni BYU-Pathway Worldwide. Ulimwenguni kote, uandikishaji umefikia karibu 75,000 na unaendelea kukua haraka. Wengi ni waumini, na zaidi ya theluthi-moja wako Afrika. Pathway inahusu upatikanaji wa elimu. Kukamilisha kozi kunamaanisha kupata ajira, na upatikanaji wa ajira unamaanisha maisha bora kwa familia na fursa zaidi za kumtumikia Bwana.
Nilipokuwa nikikutana na viongozi wa kigingi nchini Uganda, nilijifunza kwamba urais mzima wa kigingi ulijiandikisha katika BYU-Pathway. Kadiri tunavyojiandaa kimwili na kiroho, ndivyo tunavyoweza kuzuia mashambulizi ya ujanja ya adui. Kumbuka maneno ya Petro: “Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze.”
Ninatambua kwamba katikati ya habari njema ya injili, kuna wale wanaosumbuka, ambao wana changamoto za imani, mashaka, na maswali ambayo yanaonekana hayana majibu. Akina kaka na dada, Yesu Kristo ni jibu. Anza na Yeye. Tafuta mkono Wake katika maisha yako. Msikilize Yeye. “Mioyo yenu isifadhaike,” Yeye aliwaambia wanafunzi Wake katika saa Yake ya mwisho kabla ya Gethsemane, kabla ya kubeba msalaba Wake katika mitaa ya Yerusalemu, mbele ya Golgota, ambapo Yeye alikamilisha dhabihu Yake ya—upatanisho, kile ambacho Yeye tu, Mwana Pekee wa Mungu, angeweza kufanya.
Jua kwamba Yeye anaelewa. Yeye alichukua juu yake dhambi zetu zote, makosa, taabu, na siku mbaya sana ili tuweze kuishi tena na Baba yetu wa Mbinguni milele. Yeye alisema “Nitegemeeni katika kila wazo; msitie shaka, msiogope.” Imani katika Yesu Kristo inaweza kukuinua na kuponya nafsi yako iliyojeruhiwa. Mtumaini Yeye na utaharakisha kurudi kwako kwenye “mikono ya upendo wake.”
Ninasisitiza tena maneno ya nabii aliye hai: “Je, mnaona kinachotokea mbele ya macho yetu? Ninasali kwamba hatutakosa utukufu wa wakati huu! Bwana anaharakisha kazi Yake.” Sisi kama wanafunzi wa siku zetu tupige kelele, “Huree kwa Israeli” tunapojiandaa kwa ajili ya kurudi kwa Bwana na Mwokozi wetu. Katika jina la Yesu Kristo, amina.