Staha kwa ajili ya Vitu Vitakatifu
Staha kwa ajili ya vitu vitakatifu hukuza shukrani halisi, huongeza furaha ya kweli, huongoza akili zetu kwenye ufunuo, na huleta shangwe kuu kwenye maisha yetu.
Katika kitabu cha Kutoka, tunasafiri pamoja na Musa hadi kwenye miteremko ya Mlima Horebu alipokuwa alipogeuka kutoka kwenye shughuli zake za kila siku—kitu ambacho sisi sote tunapaswa kuwa radhi kufanya—ili kuona kichaka kinachowaka moto lakini hakikuteketea. Alipokuwa akikisogelea, “Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kichaka, na akasema, Musa, Musa. Naye alisema, “Mimi hapa.” Naye [Mungu] akasema, … “vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapo unaposimama ni nchi takatifu.” Kwa staha nyingi, unyenyekevu, na mshangao, Musa alivua viatu vyake na kujiandaa mwenyewe kusikia neno la Bwana na kupata uzoefu wa uwepo Wake mtakatifu.
Hilo onyesho takatifu la mlimani lilikuwa uzoefu uliojaa staha yenye kuvutia, iliyomuunganisha Musa na utambulisho wake wa kiungu na ukawa, kwa kweli, kipengele muhimu cha mabadiliko yake kutoka kuwa mchungaji mnyonge hadi kuwa nabii mwenye nguvu sana, ikimwongoza kutembea katika njia mpya katika maisha. Vivyo hivyo, kila mmoja wetu anaweza kubadilisha uanafunzi wetu kuwa mpangililo wa juu wa kiroho kwa kufanya maadili ya staha kuwa sehemu takatifu ya sifa yetu ya kiroho.
Neno staha linaweza kufuatiliwa hadi kwenye kitenzi cha Kilatini revereri, ambacho kinamaanisha “simama kwa heshima ” Katika hisia ya injili, maelezo haya yanaingiliana na hisia au mtazamo wa heshima kubwa, upendo, na shukrani. Dhihirisho kama hilo kwa ajili ya yaliyo matakatifu na wale walio na moyo uliopondeka na uchamungu wa kina kwa Mungu na Yesu Kristo hukuza ongezeko la shangwe katika nafsi zao.
Staha kwa ajili ya vitu vitakatifu ni dhihirisho kuu la sifa muhimu ya kiroho; ni zao la muunganiko wetu na utakatifu na huakisi upendo wetu kwa ajili ya na ukaribu wetu na Baba yetu wa Mbinguni na Mwokozi wetu, Yesu Kristo. Pia ni mojawapo ya uzoefu ulioinuka wa nafsi. Maadili kama hayo huelekeza mawazo yetu, mioyo yetu, na maisha yetu kwa Mungu. Kwa kweli, staha si tu kipengele cha kiroho; hiki ni kiini chake—msingi ambao juu yake hali ya kiroho hujengwa, ukitengeneza muunganiko binafsi kwa uungu, kama tunavyofundishwa na watoto wetu wanapoimba, “Ninapokuwa na staha, ninajua moyoni mwangu Baba wa Mbinguni na Yesu wako karibu,”
Kama wanafunzi wa Yesu Kristo, tumealikwa kukuza kipawa cha staha katika maisha yetu ili tujifungue wenyewe kwenye ushirikiano wa kina na Mungu na Mwanawe, Yesu Kristo, wakati huo huo kuimarisha sifa yetu ya kiroho. Tungekuwa na hisia nyingi kama hizo katika mioyo yetu, kungekuwa na shangwe kubwa na furaha bila shaka katika maisha yetu, na kungekuwa na nafasi ndogo ya huzuni na majonzi. Lazima tukumbuke kwamba kuonyesha staha kwa ajili ya vitu vitakatifu hutoa maana kwa mengi ya kile tunachofanya kila siku na huimarisha hisia zetu za shukrani—heshima yenye mwongozo, heshima, na upendo kwa vitu vya juu na vitakatifu sana.
Cha kusikitisha, tunaishi katika ulimwengu ambapo kuonyesha staha kwa ajili ya vitu vitakatifu kunaongezeka kuwa si kawaida. Kwa kweli, ulimwengu husherehekea visivyokuwa na staha, kama vile kupitia jarida la vioja, vipindi vya runinga, au uthibitisho wa intaneti. Kukosekana kwa heshima kwa vile vilivyo vitakatifu huzaa ongezeko la uzembe katika mtazamo na utovu wa nidhamu, ambavyo kwa upesi vinaweza kuangusha kizazi kimoja katika kutojali na kukizamisha kizazi kijacho katika dhiki.
Kukosekana kwa staha pia hutuongoza sisi mbali na muunganiko ambao maagano na Mungu hutoa na kufifisha hisia yetu ya uwajibikaji wetu mbele ya Mungu. Matokeo yake, tunakuwa katika hatari ya kujali tu faraja yetu wenyewe, kuridhisha tamaa zetu zisizodhibitika; na hatimaye kufika sehemu zisizo takatifu za kubeza vitu vitakatifu, hata Mungu, na kama matokeo asili yetu ya kiungu kama watoto wa Baba wa Mbinguni. Kukosekana kwa staha kwa vitu vitakatifu hukuza malengo ya adui kwa kuvuruga mikondo yetu ya utambuzi wa ufunuo ambao ni muhimu kwa ajili ya kunusurika kwetu kiroho katika siku yetu.
Maana na umuhimu wa staha kwa ajili ya kile kilicho kitakatifu imeelezwa vyema kote katika maandiko. Mfano mmoja katika Mafundisho na Maagano ungeonekana kuashiria kwamba staha kwa Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, ni maadili muhimu kwa wale wanaoingia katika ufalme wa selestia.
Kama kanisa tunajitahidi kuwaweka Baba na Mwana katika utakatifu wa juu kabisa na heshima katika kila njia, ikijumuisha jinsi tunavyoonyesha picha Zao. Mwongozo wa Roho Mtakatifu ni sehemu muhimu katika kuamua jinsi picha hizi zinavyopaswa kuakisi asili takatifu, hulka, na sifa za kiungu za Baba na Mwana. Tunakuwa makini sana ili kuepukana na kuonyesha vipengele ambavyo vinaweza kutuvuruga kutoka kwenye fokasi yetu ya msingi juu ya Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo, na mafundisho Yao, ikijumuisha jinsi tunavyotumia vyombo vya hali ya juu vinavyotolewa na tekinolojia kama vile kutumia akili mnemba (AI) kutengeneza maudhui na picha.
Kanuni hii hii inatumika kwa chanzo chochote cha habari kinachopatikana kupitia mikondo yetu rasmi ya mawasiliano ya Kanisa. Kila somo, kitabu, kitabu cha kiada na ujumbe hutengenezwa kwa makini na kuidhinishwa chini ya maelekezo ya Roho ili kuhakikisha tunadumisha maadili matakatifu, thamani, na viwango vya injili ya Yesu Kristo. Katika ujumbe wa hivi karibuni kwa ajili ya vijana wakubwa wa Kanisa, Mzee David A. Bednar alifundisha, “Ili kuongoza njia katika mkingamano changamani wa kiroho na teknolojia, Watakatifu wa Siku za Mwisho wanapaswa kwa unyenyekevu na kwa sala (1) kutambua kanuni za injili ambazo zinaweza kuongoza matumizi yao ya akili mnemba na (2) kujitahidi kwa dhati kwa ajili ya wenzi wa Roho Mtakatifu na kipawa cha kiroho cha ufunuo.”
Kaka zangu na dada zangu wapendwa, kama vile tekinolojia ya kisasa inavyoweza kuwa ya uchangamano, kwa urahisi haiwezi kusisimua maajabu, heshima, na mshangao unaopatikana katika aina ya staha inayozaliwa kutokana na ushawishi wa Roho Mtakatifu. Kama wafuasi wa Kristo, tunahitaji kuwa makini tusidhoofishe muunganiko wetu na Mungu na Mwanawe kwa kutumia maudhui na picha zilizotengenzwa na Akili Mnemba isivyo sahihi. Tunapaswa kukumbuka kwamba kutegemea teknolojia ya kisasa ya “mkono wa mwanadamu” ni mbadala usiotosha na usio na heshima kwa ajili ya mwongozo, ujenzi wa maadili, na ushahidi ambao unaweza tu kupokelewa kupitia nguvu za Roho Mtakatifu. Kama vile Nefi alivyotamka, “Ewe Bwana, nimekuamini, na nitakuamini milele. Sitaweka tumaini langu kwenye mkono wa mwanadamu.”
Katika ufunuo mwingine, Nabii Joseph Smith alielekezwa kwamba mahekalu yaliyojengwa kwa ajili ya Bwana yanapaswa kuwa mahali pa staha Kwake. Kote katika huduma yake, nabii wetu mpendwa, Rais Russell M. Nelson, amesisitiza kwa nguvu sana kuabudu kwetu katika staha ndani ya hekalu takatifu. Katika nyumba ya Bwana, tunafundishwa kuhusu kuingia katika uwepo mtakatifu wa Baba na Mwana. Mimi daima nimepata hii kuwa ni yenye kuelekeza na yenye kuvutia kwamba mojawapo ya vitu vya kwanza tunavyofanya baada kuingia ndani ya hekalu na kujiandaa wenyewe ili kushiriki katika ibada takatifu hapo ni kuvua viatu vyetu na kubadilisha na kuvaa nguo nyeupe. Kama vile Musa, ikiwa tumekusudia, tunaweza kutambua kwamba kuvua viatu vyetu vya kiulimwengu ni mwanzo wa kukanyaga ardhi takatifu na kubadilishwa katika njia za juu sana na takatifu sana.
Akina kaka na akina dada, hatuhitaji kukwea juu ya mlima, kama vile Musa alivyofanya, ili kugundua staha kwa ajili ya vitu vitakatifu na kugeuza uanafunzi wetu kuwa kiwango cha kina cha mambo ya kiroho na kuabudu. Tunaweza kuipata, kwa mfano, tunapojitahidi kulinda mazingira ya nyumba zetu kutokana na vishawishi vya kiulimwengu. Hii inaweza kutimizwa kwa kusali kwa dhati na kwa ari mbele ya Baba yetu wa Mbinguni katika jina la Yesu Kristo na kutafuta kumjua vyema Mwokozi wetu kupitia kujifunza kwetu kwa bidii neno la Mungu linalopatikana katika maandiko na mafundisho ya manabii wetu. Kama nyongeza, mabadiliko kama hayo ya kiroho yanaweza kuja tunapojitahidi kuheshimu maagano tuliyofanya na Bwana kwa kuishi kwa utiifu wa amri. Juhudi hizi zinaweza kuleta utulivu na unyamavu fulani katika mioyo yetu. Kufokasi kwenye vitendo kama hivyo hakika kunaweza kubadilisha nyumba zetu kuwa mahali pa staha pa kimbilio la kiroho—mahali patakatifu pa binafsi pa imani ambapo Roho anaweza kuishi, zaidi kama vile uzoefu wa Musa mlimani.
Sisi pia tunaweza kupata uzoefu wa mabadiliko ya kiroho kama hayo tunaposhiriki kwa uaminifu katika ibada za kuabudu za Kanisani, ikijumuisha kugeuza mioyo yetu kwa Bwana kupitia kuimba kwetu kwa dhati nyimbo takatifu. Kugeuka—kama Musa—kutoka kwenye vivuruga mawazo vya kiulimwengu, hasa simu zetu za mkononi au kitu cho chote ambacho hakiwiani na wakati huu mtakatifu, hutuwezesha kugeuza kikamilifu usikivu wetu kwenye kupokea sakramenti, akili na mioyo yetu ikifokasi kwa Mwokozi na dhabihu Yake ya kulipia dhambi pamoja na maagano yetu wenyewe. Fokasi ya kisakramenti kama hiyo itakuza wakati wa staha wa kufanywa upya kwa ushirikiano wetu na Mwokozi na kutafanya Sabato kuwa shangwe na kubadilisha maisha yetu.
Hatimaye, tunaweza kupata uzoefu wa badiliko hili la kiroho katika uanafunzi wetu tunapoabudu mara kwa mara katika mlima wa nyumba ya Bwana—mahekalu yetu matakatifu—na kujitahidi kuishi kwa kujiamini kimaagano, hasa wakati tunapokabiliana na majaribu ya maisha ya duniani.
Mimi na mke wangu kwa namna binafsi tumepata uzoefu wa baadhi ya nyakati takatifu za mlimani katika staha kadiri tunavyojitahidi kutumia kanuni hizi katika maisha yetu, ambazo zimesababisha mabadiliko ya maana katika uanafunzi wetu. Ninakumbuka kama vile ilikuwa jana nikitembea makaburini kabla ya kumzika mtoto wetu wa pili, ambaye alizaliwa kabla ya wakati wake na hakunusurika, wakati huo mke wangu akiwa bado anaendelea kupata nafuu hospitalini. Ninakumbuka kusali kwa Mungu kwa dhati sana na staha, nikiomba msaada wa kustahimili jaribio lenye changamoto. Katika wasaa ule, nilipokea hakikisho la kiroho la wazi na la nguvu katika moyo wangu: kila kitu katika maisha yetu kitakuwa sawa ikiwa mimi na mke wangu tutavumilia, tukishikilia shangwe ambayo huja kwa kuishi injili ya Yesu Kristo. Kile kilichoonekana kama changamoto isiyo na suluhisho, yenye huzuni wakati huo ilibadilika kuwa uzoefu mtakatifu, wa staha, upeo ambao umesaidia kuhimili imani yetu na imetupa sisi kujiamini katika maagano tuliyofanya na Bwana na katika ahadi Zake kwangu na familia yangu.
Akina kaka na akina dada, staha kwa ajili ya vitu vitakatifu hukuza shukrani halisi, huongeza furaha ya kweli, huongoza akili zetu kwenye ufunuo, na huleta shangwe kuu kwenye maisha yetu. Inaiweka miguu yetu kwenye ardhi takatifu na inainua mioyo yetu kwa Mungu.
Ninashuhudia kwenu kwamba tunapojitahidi kuunganisha maadili kama hayo katika maisha yetu ya kila siku, tutaweza kuongeza unyenyekevu wetu, kuongeza uelewa wetu wa mapenzi ya Mungu kwa ajili yetu, na kuimarisha kujiamini kwetu katika ahadi za maagano tuliyofanya na Bwana. Ninashuhudia kwamba tunapokumbatia kipawa cha staha kwa ajili ya vitu vitakatifu—iwe ni katika mlima wa nyumba ya Bwana, katika jengo la mkutano, au katika nyumba yetu wenyewe—tutajazwa na mshangao wa ajabu na heshima tunapounganika na upendo mkamilifu wa Baba yetu wa Mbinguni na Yesu Kristo. Kwa staha ninashuhudia kweli hizi katika jina takatifu la Mwokozi na Mkombozi wetu, Yesu Kristo, amina.