2025
Maandiko kwa Kiswahili
Desemba 2024


“Maandiko kwa Kiswahili,” Rafiki, Januari 2025, 36–37.

Maandiko kwa Kiswahili

Natamani kungekuwa na kitu ambacho ningeweza kufanya ili kusaidia, Jared aliwaza.

Hadithi ya kweli kutoka Australia.

Jared aliingia katika Shule ya Jumapili na kuketi pamoja na wanadarasa wenzake. Alimwona mvulana ambaye hakumtambua akiingia na kuketi viti kadhaa mbali na yeye.

Mwalimu wa Jared, Kaka Trudgen, alitabasamu kwa darasa. “Huyu ni Emmanuel,” alisema. “Yeye na familia yake wamehamia Australia. Hii ni Jumapili yao ya kwanza katika kata yetu!”

Jared alifikiri ingekuwa vigumu kwenda kwenye kata mpya. Angejaribu kuwa rafiki wa Emmanuel.

Kaka Trudgen alitoa maandiko yake. “Acha sote tugeukie 3 Nefi,” alisema.

Jared alifungua maandiko yake na kumtazama Emmanuel. Hakuwa na maandiko yoyote.

Jared alimpa tabasamu bashasha na akamsogelea. “Halo, mimi ni Jared,” alisema. “Je, ungependa kushiriki maandiko pamoja nami?”

Emmanuel alitabasamu pia. “Um, sijui Kiingereza vizuri,” alisema. “Pole.”

“Unazungumza lugha gani?”

“Kiswahili.”

Jared hakujua Kiswahili chochote. Yeye na Emmanuel hawakuzungumza mengi muda wote uliosalia wa darasa.

Jioni ile wakati wa chakula cha jioni, Jared aliiambia familia yake kuhusu Emmanuel.

“Anaonekana kuwa mwema sana,” Jared alisema. “Lakini hatuwezi kuelewana vizuri sana.”

Mama aliitikia kichwa. “Emmanuel na familia yake wanapitia mengi hivi sasa,” alisema. “Iliwabidi waondoke kwenye nchi yao ghafla kwa sababu mambo mabaya yalikuwa yanatokea huko. Waliacha kila kitu nyuma.”

Jared alishtuka. Ingekuwaje kuondoka nyumbani kesho na kuhamia nchi mpya kabisa? Hilo litakuwa jambo gumu sana!

Natamani kungekuwa na kitu ambacho ningeweza kufanya ili kumsaidia Emmanuel, aliwaza. Lakini ni nini?

Jared hakuweza kuacha kufikiria kuhusu Emmanuel alipokuwa tayari kulala. Aliketi kwenye meza yake pamoja na Kitabu cha Mormoni na kusoma mistari michache. Kusoma maandiko daima kulimfanya ajisikie vyema. Usiku wa leo, maandiko yalimkumbusha pia kwamba Emmanuel hakuwa na maandiko yoyote ya kusoma. Jared alifunga maandiko yake na kutazama kwenye jalada. Kisha akaruka kutoka kwenye kiti chake na kuharakisha kwenda ukumbini.

“Mama!” aliita. Ninadhani najua nini cha kufanya ili kumsaidia Emmanuel.

Jumapili iliyofuata, Jared hakuweza kusubiri kumwona Emmanuel. Aliketi na mashemasi wengine mbele ya kanisa na kungoja akiwa na Kitabu kipya cha Mormoni katika paja lake. Wamisionari walikuwa wamemsaidia kupata nakala hii maalum kwa ajili tu ya Emmanuel.

Wakati Emmanuel alipoingia kanisani pamoja na familia yake, Jared alitabasamu na kumpungia mkono aje. Emmanuel alionekana kukaanganyikiwa alipokuwa ameketi karibu na Jared. Lakini macho yake yalipata nuru wakati Jared alipompa Kitabu cha Mormoni.

Mikono ikibadilishana Kitabu cha Mormoni cha Kiswahili

“Kwa ajili yangu mimi?” Emmanuel aliuliza.

Jared aliitikia kwa kichwa.

Macho yake yalifurahia. Alipekua kurasa za Kitabu chake kipya cha Mormoni. “Kiswahili!” alisema. Alitabasamu kwa Jared na kukumbatia kitabu hicho kifuani mwake. “Asante!”

Moyo wa Jared ulichangamka alipokuwa akitabasamu. Alijua asingeweza kufanya kila kitu kuwa kizuri kwa Emmanuel, na bado hawakuweza kuzungumza wao kwa wao vizuri sana. Lakini hiyo ilikuwa SAWA. Hawakulazimika kuzungumza lugha moja ili kuwa marafiki!

PDF ya hadithi

Kielelezo na Keith Negley