“Kwenda Kanisani pamoja na Ghuka,” Rafiki, Januari 2025, 30–31.
Wanzilishi katika Kila Nchi
Kwenda Kanisani na Ghuka
Kelvin hakuwahi kuona kanisa kama hili hapo awali.
Hadithi ya kweli kutoka Kenya.
Kelvin kwa uangalifu aliweka chupa za kioo chenye kung’aa za maziwa kwenye rafu. Hivi karibuni alikuwa ameenda kuishi na babu na bibi yake katika kijiji nje ya mji. Walimiliki duka la maziwa, na Kelvin alipenda kusaidia.
“Usiku wa leo tutafanya shughuli kanisani kwetu,” Ghuka (Babu) alisema. “Unataka kuja pamoja nasi? Itakuwa ya kuburudisha.”
Kelvin alipenda burudani. “Ndio!,” alisema. “Nitaenda pamoja nawe!”
Baada ya kufunga duka, Kelvin na babu na bibi yake walitembea kuelekea kwenye shughuli. Waliyapita maduka mengine ya kuuza vitambaa, matunda, na mimea vyunguni. Baada ya muda, walifika kanisani.
Kelvin alisimama kwa mshangao alipokuwa akitazama jengo zuri. Hakuwahi kuona kanisa kama hili hapo awali. Makanisa mengi yalikuwa na msalaba juu, lakini hili halikuwa hivyo.
Ndani, babu na bibi wa Kelvin walimtambulisha kwa watu wengi wema. Walikula chakula kitamu sana na wakacheza michezo.
Lakini Kelvin alikuwa mtafiti. Hivyo alizunguka kwenye kumbi za kanisa. Aliaona mchoro wa Yesu Kristo. Kisha akaingia darasani na kuona baadhi ya picha ukutani.
Watu hao ni akina nani? Kelvin alijiuliza.
Baada ya kuondoka chumbani, aliwaona vijana wawili ukumbini. Walikuwa wamevalia mashati meupe na tai. “Jambo,” mmoja wao alisema. “Sisi ni wamisionari. Jina lako ni nani?”
Kelvin alijitambulisha mwenyewe. Kisha akauliza, “Ni nani huyo aliye katika picha hiyo?” Alionyesha nyuma kwenye mojawapo ya picha chumbani.
“Huyo ndiye nabii,” mmisionari mwingine alisema. “Je, Unajua nabii ni nani?”
Kelvin alitabasamu na kutikisa kichwa chake hapana.
“Nabii ni mjumbe kutoka kwa Mungu,” alisema mmisionari. Anatufundisha kile ambacho Mungu anataka sisi tujue.
Wakati Kelvin alipotembea kwenda nyumbani na babu na bibi yake usiku ule, alikuwa ameshikilia nakala ya Kitabu cha Mormoni ambacho wamisionari walikuwa wamempa. Alikuwa na shauku ya kujifunza zaidi kuhusu manabii na kanisa hili jipya.
“Je, utatusomea?” Ghuka aliuliza walipofika nyumbani. Babu na bibi wa Kelvin hawakujua kusoma.
“Ndiyo!” Kelvin alisema. Alifungua Kitabu cha Mormoni na kusoma kwa sauti. Hakuelewa maneno yote, lakini alihisi kitu maalum.
Siku ya Jumapili, Kelvin alitembea na babu na bibi yake kurudi kanisani. Alikwenda kwenye darasa la watoto wote. Linaitwa Darasa la Watoto. Alipata marafiki wengi! Alijifunza zaidi kuhusu manabii na Yesu.
Wamisionari walikuja kumfundisha zaidi Kelvin. Siku moja walimwuliza swali. “Je, utafuata mfano wa Yesu na kubatizwa?
Kevin alitoa tabasamu bashasha. “Ndiyo!”
Siku ya ubatizo wake, Kelvin aliingia ndani ya maji. Yalikuwa ya baridi sana. Lakini Kelvin alipokuwa akitazama kumzunguka, aliwaona babu na bibi yake, wamisionari, na marafiki zake wote wapya kutoka kanisani. Alihisi kupendwa sana!
Kwa kuchagua kumfuata Yesu Kristo, Kelvin alikuwa mwanzilishi katika familia yake. Hakuweza kusubiri kuendelea kumfuata Yeye—na kuwasaidia wengine wamfuate pia Yesu Kristo!
Vielelezo na Kristin Sorra