“Ono la Kwanza,” Rafiki, Januari 2025, 26–28.
Hadithi za Maandiko
Ono la Kwanza
Unaweza kusoma hadithi hii katika Joseph Smith—Historia ya 1:1–20.
Wakati Joseph Smith alipokuwa mdogo, makanisa mengi yalifundisha mambo tofauti kuhusu Yesu Kristo. Joseph hakujua ni kanisa gani la kujiunga nalo.
Siku moja, alisoma Yakoba 1:5 katika Biblia. Ilisema kama tunahitaji hekima, tunaweza kumwomba Mungu. Joseph aliamua kufanya hivyo.
Katika siku nzuri ya majira ya kuchipua, Joseph alikwenda msituni kusali kwa Baba wa Mbinguni.
Joseph alipiga magoti na kuanza kusali. Lakini kisha alihisi giza likimzunguka. Joseph aliogopa. Alimwomba Mungu msaada.
Ghafla, Joseph aliona mwanga mkali ukishuka kutoka mbinguni. Aliwaona Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo wamesimama juu angani. Baba wa Mbinguni aliliita jina la Joseph. Kisha Yeye alimwonyesha Yesu na akasema, “Huyu ni Mwanangu Mpendwa. Msikilize Yeye!”
Yesu alimwambia Joseph asijiunge na kanisa lolote.
Joseph angesaidia kurejesha utimilifu wa injili duniani.
Joseph hakukanganyikiwa tena. Alijawa na shangwe! Alijua Mungu alimpenda. Baadhi ya watu hawakuamini kwamba alikuwa amewaona Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, lakini yeye alijua ilikuwa ni kweli.