2025
Pesa Sokoni
Mei 2025


Pesa Sokoni

Wakati huu, ninakwenda kufanya kile hasa Mama alichoomba, Anane aliwaza.

Hadithi ya kweli kutoka Ghana.

Mvulana akiwa ameshikilia pesa na akiangalia bidhaa kwenye rafu za sokoni

Anane alitabasamu alipokuwa akitembea mtaani. Harufu ya samaki wakikaangwa na kelele za shughuli nyingi za watu vilienea sokoni. Alikuwa njiani kuelekea nyumbani kwa Mjomba wake. Mama alikuwa amempa Anane pesa kiasi kwa ajili ya kumpa Mjomba.

Alitazama kote kwenye sehemu zote za kuuza mazao, vyakula, na vitu vingine. Kisha kitu kilinasa jicho lake.

Kulikuwa na stendi ya chakula ambayo ilikuwa na vitafunwa vyake pendwa viwili, pipi na biskuti. Aliangalia pesa Mama alizompa. Cedis mia moja ni nyingi, aliwaza. Vitafunwa vyake pendwa vilikuwa ni cedis 10 tu. Mjomba labda hata asingegundua kama pesa imepungua.

Anane alinunua vitafunwa. Aliweka pipi kinywani mwake na kuendelea kutembea kuelekea nyumbani kwa mjomba.

Mjomba alikuwa amesimama nje ya nyumba yake wakati Anane akitembea kuelekea kwenye nyumba.

“Si huyu ni Anane mdogo! Njoo, alisema Mjomba. “Naweza kufanya nini kwa ajili yako?”

“Nimekuletea pesa kiasi kutoka kwa Mama.” Anane alimpa pesa zile, kisha akaweka mikono yake mifukoni mwake. Je, Mjomba angegundua kwamba baadhi ya pesa zinakosekana? Alitazama wakati Mjomba akihesabu.

“Asante kwa kuzileta hizi,” Mjomba alisema.

Anane alikuwa na furaha Mjomba hakugundua pesa iliyokosekana. Alisema kwaheri na kuanza matembezi marefu kurudi nyumbani. Akiwa njiani, alimalizia kula pipi yake na biskuti.

“Je, matembezi ya kwenda kwa mjomba yalikuwaje?” Mama alimwuliza Anane alipofika nyumbani.

Aliinua mabega. “Yailikuwa mazuri.”

“Asante kwa kumpelekea pesa hizo kwa niaba yangu,” alisema Mama.

Anane aliangalia chini sakafuni. Alianza kuhisi mwenye hatia. Vipi kama wazazi wake wangegundua alikuwa ametumia kiasi cha pesa hizo? Hakutaka kupoteza imani yao.

Asubuhi iliyofuata, Mama alimwomba Anane kununua baadhi ya vitu kwenye duka lililo karibu. “Njoo nyumbani moja kwa moja baada ya kumaliza kununua, SAWA?”

“SAWA.” Anane alitembea kupitia sokoni, lakini hakusimama kununua chochote. Alichezesha kope za macho yake na kufikiria, sasa nitafanya sawa sawa na kile Mama alichoniomba.

Punde tu alipomaliza, alienda nyumbani moja kwa moja. Alimpa Mama pesa zote zilizobaki.

Jumapili hiyo, Anane alikwenda kwenye darasa lake la Watoto. “Habari ya asubuhi!” mwalimu wake alisema. “Leo tunazungumzia kuhusu utiifu. Ni muhimu kwetu sisi kuwasikiliza wazazi wetu na kufanya chaguzi nzuri.”

Anane alifikiria kuhusu ile fedha aliyotumia kwenye pipi na biskuti. Alihisi tumbo lake likishuka. Alijua kuwa alifanya chaguo baya.

Baada ya kutoka kanisani, Anane alitaka kuzungumza na wazazi wake. Moyo wake ulikuwa unaenda mbio.

“Mama, Baba? Mnakumbuka pesa mliyonipa ili niipeleke kwa Mjomba?” Anane aliuliza. “Basi, nilinunua vitafunwa kwa kiasi fulani cha pesa hizo.” Aliangalia chini sakafuni. “Samahani.”

“Asante kwa kuwa mwaminifu.” Baba alisema. “Najivunia wewe.”

Anane alitabasamu. Alikuwa na furaha sana kwamba alisema ukweli. Na alihisi vizuri moyoni baada ya kuwaambia wazazi wake. Alikuwa tayari anafanya uchaguzi mzuri zaidi.

Ukurasa wa PDF

Kielelezo na Aleksandar Zolotic