Suluhisho la Kivuli
“Vipi kama tukipanda miti?” Cristal aliuliza.
Hadithi ya kweli kutoka Argentina.
“Je, tunaweza kwenda uwandani?” Cristal Dada yake Ivan aliuliza.
Ivan aliangalia nje. “Nataka kwenda,” alisema. “Lakini pengine tunapaswa kusubiri hadi jua litue. Kuna joto sana!”
Uwanda ilikuwa ni uga mkubwa wa nyasi karibu na nyumba yao. Walipenda kucheza tegi au kombolela na marafiki zao. Lakini uwandani hapakuwa na kivuli chochote kwa ajili yao kupumzika kutokana na jua kali. Na msimu huu wa kiangazi, lilikuwa tatizo kubwa.
Cristal alikuwa kimya kwa muda. Kisha akasema, “Vipi tukipanda miti? Kwa njia hiyo uwandani kutakuwa na kivuli. Kisha tutaweza kucheza hata wakati inapokuwa jua kali!”
Ivan alitabasamu “Ninalipenda wazo hilo!”
Ivan na Cristal walimwambia Papá yote kuhusu mpango wao. “Nitaomba ruhusa kutoka jiji,” alisema.
Wiki chache baadaye, walikuwa na ruhusa waliyohitaji na walikuwa tayari kuanza! Papá alimchukua Ivan na Cristal kwenye mti mkubwa ambao ulikua nyuma ya nyumba yao. Chini ya mti, kundi la miti midogo midogo ilikuwa ikichipua.
“Wakati mti mkubwa unapochanua, huangusha mbegu ardhini,” Papá alieleza. “Kisha miti midogo midogo inachipua kutokana na mbegu hizo. Hiyo ni kama miujiza midogo midogo ya asili!”
Papá aliwaonyesha jinsi ya kuchimba miti hiyo midogo kwa uangalifu. Ivan na Cristal taratibu waliipanda miti hiyo midogo katika vyungu vya kupandia maua.
Kisha, Jumamosi moja mchana wakati jua lilipofichwa nyuma ya mawingu, Ivan na Cristal waliipakia miti hiyo midogo kwenye mkokoteni. Taratibu, waliusukuma kwenda kwenye uwanda. Wadogo zake Ivan wa kiume na wa kike walisaidia kubeba ndoo za maji. Mamá na Papá walileta makoleo.
Kwa pamoja, walichagua eneo kwa ajili ya kila mti. Walichimba mashimo na kupanda kila mti kwa upendo. Mamá aliwaonyesha jinsi ya kuchimba mitaro kuzunguka miti ili kuimwagilia maji. “Miti inahitaji mwanga wa jua, maji, na virutubisho vingi ili kuwa imara,” alisema. “Kama vile watoto!”
Ivan alifikiria juu ya mti nyuma ya nyumba yao na kufikiria miti ile ingeonekanaje siku moja. “Mnaweza kuamini?” alisema. “Siku moja miti hii itakuwa mirefu kuliko sisi!”
Katika majira ya kuchipua, miti ingemshangaza kila mtu kwa maua yake mazuri, rangi ya waridi. Wakati wa majira ya kiangazi, kivuli chake kitaenea kote kwenye uwanda huu. Na katika majira ya kupukutisha, majani yangefunika ardhi katika zulia la njano.
Kila siku, Ivan na Cristal walitembelea uwanda kuangalia miti ile. Walihakikisha kila mti ulipata maji ya kutosha. Na kila wakati jani jipya au tawi jipya lilipochipuka, walihisi fahari sana. Kazi yao ngumu ilifanikiwa!
Ivan alihisi furaha akiwafikiria watu wote ambao wangefurahia kivuli kwenye uwanda huo siku moja. Alikuwa amesaidia kuifanya dunia kuwa mahali pazuri zaidi kwa watoto wote wa Baba wa Mbinguni.
Vielelezo na Colleen McKeown