Waanzilishi katika Kila Nchi
Kidogo Kama Mbinguni
“Je, ungependa kwenda kanisani?” Mjomba Reza aliuliza.
Hadithi ya kweli kutoka India na Kanada.
Tahira alikunja shati la mwisho na kuliweka katika sanduku lake. Alikuwa akifungasha kwa ajili ya safari ya kufurahia majira ya joto na shangazi yake na mjomba wake nchini Kanada. Alikuwa na furaha lakini pia alikuwa na wasiwasi kidogo. Kanada ilikuwa mbali sana na nyumbani kwake nchini India.
“Je, una kila kitu?” Mama aliuliza.
“Nadhani hivyo.” Tahira alifunga sanduku lake.
“Utakuwa na wakati mzuri. Hakikisha unampa mjomba Reza na Shangazi Misu kumbatio kubwa kutoka kwangu,” Mama alisema.
Wakati Tahira aliposhuka kutoka kwenye ndege nchini Kanada, alimpa Mjomba Reza na Shangazi Misu kumbatio kubwa. “Hili linatoka kwa mama yangu,” alisema.
Walitumia siku chache zilizofuata kuchunguza mji na maeneo ya karibu. Alipata kutembelea bustani yake ya kwanza ya burudani na kuona Maporomoko ya Niagara. Ilikuwa burudani sana!
Jumamosi mchana, Tahira alisaidia kutengeneza kuku wa makhani kwa ajili ya chakula cha jioni. Baada ya kula, Mjomba Reza alimuuliza swali.
“Je, ungependa kwenda kanisani na sisi kesho?” aliuliza. “Tunaenda kwenye kanisa la Kikristo. Tunajifunza kuhusu Yesu Kristo na injili Yake huko.”
“Hakika,” Tahira alisema. Mama na Baba waliamini katika dini tofauti, lakini Tahira alienda katika shule ya bweni ya Kikristo nchini India. Kwenda kwenye kanisa jipya hakungekuwa tofauti sana.
Siku iliyofuata, Tahira alivalia gauni ambalo shangazi yake alimpa alivae. Walipofika kanisani na kuingia ndani, kila mmoja alikuwa akiimba. Tahira alisimama na kuwatazama watu wote. Kulikuwa na akina mama na akina baba waliokaa na watoto wao. Kila mtu alionekana mwenye furaha. Uimbaji ulikuwa mzuri sana.
Hili linaonekana kama mbinguni, Tahira aliwaza.
Tahira aliketi kwenye moja ya benchi akiwa na Shangazi Misu na Mjomba Reza. Alitazama trei za mkate na maji zikipitishwa. Aliwasikiliza wazungumzaji wakizungumza kuhusu Yesu Kristo. Na alisikia uimbaji zaidi. Wimbo wa mwisho ulikuwa kuhusu familia kuwa pamoja milele. Alipenda jinsi maneno yalivyomfanya ahisi.
Baada ya sala ya mwisho, Tahira alimgeukia Mjomba Reza. “Kuwa pamoja milele kunamaanisha nini?”
Mjomba Reza alitabasamu. “Tunaamini kwamba kama tutamfuata Yesu Kristo na kufanya na kutunza ahadi na Mungu, tunaweza kuishi mbinguni na familia zetu siku moja—wote pamoja.”
Tahira alihisi vizuri kutoka kichwani mwake hadi vidole vyake. Alipenda wazo la kuwa pamoja na familia yake milele.
Baada ya kutoka kanisani, Tahira aliendelea kufikiria kuhusu muziki mzuri. Alitaka kujifunza zaidi kuhusu Yesu Kristo na familia za milele. Aliamua kukutana na wamisionari. Wiki zilipokuwa zikipita, Tahira alijua zaidi na zaidi kwamba injili ilikuwa ya kweli.
Tahira aliwapigia wazazi wake kuwaambia kuhusu kile alichokuwa akijifunza. Kisha akawauliza swali muhimu. “Je, ninaweza kubatizwa?” Walisema ndiyo!
Siku ya ubatizo wake, Tahira, Mjomba Reza, na Shangazi Misu waliimba “Mimi ni Mtoto wa Mungu.” Mjomba Reza alikuwa ameutafsiri ili waweze kuimba kwa Kihindi. Kihindi kilikuwa lugha aliyozungumza nyumbani India.
Tahira alipoimba, alihisi hisia nzuri moyoni mwake. Ilikuwa kama mbinguni. Na Tahira alijua kwamba kwa sababu ya Yesu Kristo, kama angetii ahadi zake kwa Baba wa Mbinguni, angeweza kuishi na Wote wawili tena siku moja.
Vielelezo na Ekata Mandal