Rahisi kwa Kusoma
Maneno Matamu na Rahisi
Hadithi ya kweli kutoka Marekani.
Kaci alitabasamu alipokuwa akichukua kiti chake katika Darasa la Watoto. Leo ilikuwa ni mawasilisho ya watoto kwenye mkutano wa sakramenti. Ilikuwa ya kuogopesha kusema sehemu yake, lakini alifanya hivyo!
Dada Dench, rais wa Darasa la Watoto, alisimama mbele. “Kazi nzuri katika mkutano wa sakramenti leo!” alisema. “Ninajua kila mmoja alifanya kazi kwa bidii ili kujifunza sehemu yake.”
“Isipokuwa Kaci,” mmoja wa wavulana wakubwa alisema. “Hakuna mtu aliyeelewa kile alichokisema.”
Dada Dench alionyesha uso wa kuchukia kwa mvulana yule, kisha akageuka kwa Kaci na kutabasamu. “Ulifanya kazi nzuri sana.”
Kaci alijaribu kutokulia. Alifanya awezavyo kujifunza sehemu yake. Lakini wakati mwingine maneno yake hayakutoka kwa usahihi.
Njiani kuelekea nyumbani, Kaci hakuweza kuzuia machozi tena.
“Kuna tatizo gani?” Mama aliuliza.
“Mmoja wa wavulana alinifanyia mzaha. Alisema sikusema sehemu yangu kwa usahihi.” Alianza kulia kwa sauti kubwa.
“Ulifanya kazi nzuri. Mimi na baba tunajivunia wewe,” Mama alisema. “Je, unamjua nani mwingine anajivunia wewe?”
Kaci alitikisa kichwa chake.
“Baba wa Mbinguni,” Mama alisema. “Anajua ulifanya kadiri uwezavyo.”
Kaci alihisi vizuri sasa. Alitaka kutumia maneno yake kuwasaidia watu wengine wahisi furaha pia.
Shuleni, Kaci alimwambia mwalimu wake kwamba alikuwa akifanya kazi nzuri kwa kuwafundisha.
Nyumbani, Baba alikuwa akitengeneza rafu. Kaci alimwambia alikuwa akifanya kazi nzuri ya kuifanya nyumba yao iwe nzuri.
Nje, Kaci na kaka yake walicheza mpira pamoja. Kaci alimwambia kwamba alikuwa akifanya kazi nzuri ya kurusha mpira.
Kuwaambia watu walikuwa wakifanya kazi nzuri ilimfanya Kaci kuhisi vizuri moyoni. Alipowaona wengine wakitabasamu, alijua kwamba maneno yake rahisi yalileta tofauti kubwa!
Vielelezo na Greg Paprocki