2025
Kanisa Jipya kwa Ajili ya Jamesi
Mei 2025


Kanisa Jipya kwa Ajili ya Jamesi

Jamesi alijisikia tofauti hapa kuliko ilivyokua katika kanisa lao lingine.

Hadithi ya kweli kutoka Fiji.

Jamesi alitembea kwenda kwenye eneo dogo la ua ambako familia yake iliwaweka nguruwe. “Haya chukua, nguruwe!” Aliwarushia chakula, na nguruwe wakakoroma kwa furaha.

Kisha Jamesi akabeba chupa safi za maji hadi kwenye bomba nje. Maji baridi yalitiririka ndani ya chupa alipokuwa akifungua bomba. Kuwalisha nguruwe na kupata maji kwa ajili ya familia yake ndivyo alivyosaidia kila siku.

“Jamesi!” Mama alimwita. “Uko tayari kwa ajili ya kanisani?”

Jamesi alifunga bomba la maji na kupeleka chupa nzito ya mwisho ndani. “Niko tayari sasa.”

Kila Jumapili familia ya Jamesi ilienda kwenye kanisa la Kikristo katika mji wao. Alipenda kujifunza kuhusu Yesu Kristo.

Punde Jamesi na dada zake wadogo, Unaisi na Marama, walikuwa wakitembea pamoja na familia yao yote kwenda kanisani. Kuku wachache waliopotea walipiga kidoko mtaani.

Familia ikiwa imesimama mbele ya jengo la Kanisa

Lakini walipofika huko, milango ilikuwa imefungwa. “Nilisahau kwamba kanisa limefungwa wiki hii na wiki ijayo tangu mchungaji aondoke,” Baba alisema.

“Je, kuna kanisa lingine tunaweza kwenda?” aliuliza Jamesi. Angehuzunika kukosa kanisani wiki hii.

Baba aliwaza kwa muda. “Ndio,” alisema. “Nafikiri ninalijua moja.”

Jamesi na familia yake walimfuata Baba kurudi nyumbani kwao. Wote waliingia katika mashua yao ndogo ya mbao pembeni mwa mto. Baba aliketi nyuma kuongoza chombo.

Familia katika mashua ndogo ya mbao ikishuka mtoni

Mashua iliunguruma ikishuka mtoni. Jamesi aliwatazama ndege waliojificha kwenye miti mirefu ya kijani kibichi. Baada ya takribani dakika 15, waliona jengo dogo la kanisa. Lilikuwa na bango lililosema, “Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.”

“Hili ndilo kanisa ambalo nilikuwa nalifikiria,” alisema Baba. Aliendesha mashua hadi ufukweni, na kila mtu akashuka. Waliweza kusikia muziki ukitoka ndani ya jengo la kanisa.

Ndani, Jamesi aliketi na wazazi wake na ndugu zake. Waliwasikiliza wazungumzaji na nyimbo. Jamesi alijisikia vizuri, akiwa na furaha ndani yake.

Mkutano ulipokwisha, mwanamke mwema alikuja kuzungumza nao. “Tuna darasa maalumu kwa ajili ya watoto,” alisema. “Linaitwa Darasa la Watoto. Je, ungependa kuja?”

Jamesi aliwaangalia dada zake. Alijisikia wasiwasi kidogo kwenda darasani ambapo hakumjua yeyote! Angalau dada zake wangeweza kuja pia. Pengine itakuwa ya kufurahisha!

“Hakika,” alisema.

“Twendeni!” Marama alionekana kusisimka.

Jamesi na dada zake wadogo walimfuata mwanamke yule darasani. Kulikuwa na watoto wengi waliokaa kwenye viti vidogo, wakizungumza na kucheka. Wakati Jamesi alipoketi, walitabasamu kwake. Kila mtu alikuwa mkarimu sana!

Waliimba nyimbo, na watoto wengine walimsaidia Jamesi na dada zake kujifunza maneno. Kisha walikuwa na somo kuhusu Yesu Kristo. Jamesi alijisikia tofauti hapa kuliko ilivyokua katika kanisa lao lingine. Ilikuwa tofauti nzuri.

Familia yenye furaha mbele ya kanisa

Ibada lilipokwisha, familia ya Jamesi ilipanda tena ndani ya mashua ili kwenda nyumbani. Jamesi aliangalia ishara ile nje ya jengo la kanisa tena. Ilikuwa na jina la Yesu Kristo juu yake. Kwa hiyo lazima liwe Kanisa la Yesu Kristo! Jamesi alitaka kumfuata Yesu.

“Je, tunaweza kuja hapa tena wiki ijayo?” Jamesi aliuliza.

Mama na Baba walitabasamu. “Tulikuwa tunafikiria jambo hilo hilo,” Mama alisema.

“Yay!” Unaisi alishangilia.

Jamesi alitabasamu. Alijua walikuwa wamepata kitu maalumu. Na hakuweza kusubiri kujifunza zaidi.

Ukurasa wa PDF

Vielelezo na Bethany Stancliffe