“Kushirki Mwangaza wa Jua,” Rafiki, Mei 2025, 30-31.
Waanzilishi katika Kila Nchi
Kushiriki Mwangaza wa Jua
“Ni wimbo kutoka kanisani kwangu,” Ángel alisema.
Hadithi ya kweli kutoka Argentina.
Ángel alipanda juu ya gari karibu na Papá. Chupa za kioo za maziwa nyuma ziligongana kwa upole huku farasi wao akisonga mbele. Jua lilikuwa linang’aa, na lilimkumbusha juu ya wimbo wake alioupenda sana.
“Yesu ananitaka niwe jua,” Ángel aliimba.
Miezi michache iliyopita, Ángel alikuwa amebatizwa. Mamá na kaka yake mdogo, Oscar, walibatizwa pia. Papá hakujiunga na Kanisa, lakini alikuwa na furaha kwao. Ángel bado alikumbuka jinsi ilivyohisi alipotoka nje ya maji. Ilikuwa ni kama jinsi mwanga wa jua ulivyohisi mgongoni mwake, lakini kwa ndani.
Ángel aliendelea kuimba mwenyewe wakati Papá aliposimamisha gari nje ya nyumba ya Señora Perez. Ángel aliruka chini na kunyakua chupa ya maziwa kutoka nyuma. Señora Perez alikuwa mmoja wa wateja wa familia yake.
“Mgao!” alisema.
Señora Perez alikuwa akifanya kazi katika bustani yake. “Asante,” alisema, akichukua chupa. Akampa sarafu kadhaa. “Ni wimbo gani huo ulikuwa unaimba?”
Angel alihisi mashavu yake yakipata joto. Hakutambua kwamba alikuwa amemsikia!
“Ni wimbo kutoka kanisani kwangu,” Ángel alisema. “Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho.”
Señora Perez alitabasamu. “Kwa nini usiniambie kitu kuhusu kanisa lako?”
Kwa muda mfupi, Ángel hakuwa na uhakika wa nini cha kusema. Kisha akasema, “Tunaamini kwamba kanisa lile lile Yesu Kristo alilolianzisha wakati alipoishi duniani liko hapa tena.”
“Inapendeza,” Señora Perez alisema. “Sijawahi kusikia juu ya kanisa ambalo linaamini hilo.”
“Pengine unaweza kuja wakati mwingine,” Ángel alisema. “Uwe na siku njema!” Kisha akakimbia tena kwa Papá ili kusaidia kutoa maziwa yote.
Mapema Jumapili asubuhi, Ángel aliamka. Aliweza kumsikia Mamá jikoni akitengeneza kifungua kinywa.
“Oscar,” Ángel alisema, “ni wakati wa kujiandaa kwa ajili ya kanisani!”
Ángel na Oscar walivaa nguo zao za kanisani na wakawa tayari kuondoka. Jengo la kanisa lilikuwa umbali wa karibu maili mbili. Yalikuwa matembezi marefu, hivyo ilibidi waondoke mapema.
“Kuwa na wakati mzuri,” Papá alisema walipokuwa wakiondoka.
Walipokuwa wakitembea, Ángel aliimba tena kwa kuvumishawimbo alioupenda sana. Aliimba kwa kuvuma walipokuwa wakipita kwenye nyumba ambapo alipeleka maziwa. Aliimba kwa kuvuma walipokuwa wakipita vibanda vya matunda sokoni. Na aliimba kwa kuvuma walipokuwa wakipinda mtaani ambako jengo la kanisa lilikuwa.
Walipoingia ndani, Ángel alishangazwa. Señora Perez alikuwa pale! Alikuwa ameileta familia yake yote pamoja naye.
“Umekuja kanisani!” Ángel alisema.
Señora Perez aliitikia kwa kichwa. “Nilivutiwa na wimbo wako,” alisema. “Nilimpigia mama yako kwa ajili ya anwani. Nilitaka kuja kujifunza kuhusu kanisa hili mimi mwenyewe.”
Ángel alitabasamu. Alikuwa ameshiriki injili kwa kuimba wimbo tu. Alitumaini Señora Perez angeweza kuhisi mwangaza wa jua moyoni mwake leo pia.
Vielelezo na Jomike Teijido