Kurasa za Karibu
KNV ya Uganda Inajenga na Kuwezesha
KNV ni kifupi cha “Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana.” Ni programu ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho kwa ajili ya vijana wa umri wa miaka 14 hadi 18. Programu imekusudiwa kuwasaidia vijana kuendelea kiroho, kijamii, na kimwili na kuwaandaa kwa ajili ya majukumu ya uongozi ya baadaye katika Kanisa na katika jumuiya zao.
Mkutano ulianza mnamo tarehe 26 Agosti na kumalizika tarehe 30 Agosti, 2024 katika Shule ya Kimataifa ya Hana Barabara ya Nsangi-Buloba Kampala, Uganda. Mkutano huu uliwajumuisha washiriki kutoka Wilaya ya Busia Uganda/Kenya, Kigingi cha Kampala North, Wilaya ya Gulu na kata na matawi ya misioni ya Uganda Kampala.
Huwezi Kuifanya Wewe Peke Yako
Watu wengi walikuja kwa nabii Musa kuanzia asubuhi mpaka jioni ili kushauriwa na kuelekezwa. Kwa sababu ya wingi wa watu, Yethro, baba mkwe wa Musa, alimwona Musa akilemewa na yale yote aliyoyafanya kwa watu kwani wengi waliendelea kuja kwa Musa ili kutafuta ushauri wa nabii wa Mungu. Yethro alimshauri Musa awafundishe wanaume wenye uwezo ili wamsaidie. Musa aliitikia hekima ya baba mkwe wake na akawafunza wanaume wenye uwezo wa Israeli na kunaibisha maadhi ya majukumu yake ili kuifanya kazi yake iwe yenye fokasi zaidi na endelevu.
Tunapowasikiliza wenye hekima na kufanyia kazi ushauri wao kama Musa alivyofanya, tutawabariki wengi wa watoto wa Baba wa Mbinguni. Kuwaandaa kizazi kinachoinukia kwa ajili ya maisha ya imani na huduma huitaji uendelevu wa kuwafunza na kuwasaidia wajenge imani, hekima na kujitoa. Sehemu ya mara kwa mara ya kuwafunza na kuwapa msukumo vijana wa Kanisa ni Vikao vya Kwa Ajili ya Nguvu kwa Vijana (KNV). Kwenye kikao cha KNV kuna wanandoa waelekezi, waratibu, waratibu wasaidizi na washauri, wote wakibariki maisha ya washiriki.
Siku ya 1
Viongozi wote ikiwa ni pamoja na waelekezi huwakaribisha kwa shauku washiriki kutoka vigingi na wilaya tofauti tofauti. Kadiri mabasi yalivyowasili kwenye eneo la KNV washiriki walielekezwa kwenye vyumba vyao na kusaidiwa mizigo yao.
Siku ya 2
Siku hii ilijumuisha ibada ya asubuhi, kujifunza injili na ibada ikiwa na wanandoa waelekezi wa kikao. Pia, shughuli za Siku ya 2 zikijumuisha shughuli za burudani kama vile muziki, maonyesho mbalimbali, dansi na michezo. Vijana washiriki walijifunza mengi kuhusu Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo, na walipata burudani!
Siku ya 3
Fokasi ya siku ya tatu ya KNV Uganda ilikuwa Hubiri Injili Yangu, sura ya sita na ya kumi, ambazo zinafundisha juu ya kukuza sifa kama za Kristo na kujenga imani katika Yesu Kristo. Kaka na Dada Wafula, waelekezi wa kikao, sambamba na waratibu wa kikao Fred Ouma na Zaina Apori, waliwafunza vijana kuhusu kuwa kama Yesu Kristo na kukuza imani Kwake. Sifa kama za Kristo hukuzwa katika maisha ya vijana kadiri wanavyofokasi kwa Yesu Kristo, walifundisha Kaka na Dada Wafula. Kaka Ouma na Dada Apori waliwaalika vijana kukuza imani katika Yesu Kristo kwa kufanya dhabihu, kushiriki shuhuda na kuwaalika wengine kuja kwa Kristo. Waliwahimiza vijana kuwa kama mwanamke Msamaria ambaye Yesu alikutana naye kisimani. Baada ya kukutana na Mwokozi, aliuacha mtungi wake wa maji na kwenda kijijini na kushuhudia juu ya Yesu na kuwaalika wengine waje na kumwona Yesu. (Yohana 4:11–30)
Siku ya 4
Siku ya nne ilikuwa siku ya burudani na kushiriki talanta. Wakati wengi wakiwa wamekusanyika kwenye ukumbi, wengi wa vijana kwenye KNV walikwenda jukwaani na kudansi au kuwaimbia wenzao waliohudhuria kikao. Wote walikuwa wakiwashangilia na kuwaunga mkono wale waliokuwa wakifanya maonyesho. Siku ilijumuisha maonyesho mbalimbali ya talanta ambayo ilikuwa moja kati ya shughuli zilizofurahiwa zaidi za kikao cha KNV.
Siku ya 5
Siku ya 5 ilikuwa siku nzima ya mwisho ya Kikao cha KNV Uganda. Siku ilianza kwa ibada ya asubuhi ambapo waelekezi wa kikao waliwakumbusha vijana kubaki wakweli kwenye imani yao, kutii amri na kuendelea kutumikia Kanisani. Siku na Kikao cha KNV, vilihitimishwa kwa maonyesho ya slaidi yakiwa na washiriki na shughuli zao wakati wa siku tano za kupendeza walizozitumia pamoja.
Vijana kwenye KNV ya Uganda walikumbushwa kwamba nabii wa Bwana aliye hai, Rusell M. Nelson, amesisitiza kwamba kazi kuu kuliko zote duniani leo ni kuikusanya Israeli pande zote mbili za pazia kwa kuleta nafsi kwa Kristo. Wavulana na wasichana nchini Uganda walishauriwa kumfuata nabii, kusoma maandiko, kuhudumu kanisani na kusaidia kuikusanya Israeli. Kwa kufanya kazi ya umisionari na kazi ya historia ya familia, wanawasaidia watoto wa Mungu pande zote mbili za pazia kuishi na Baba yetu wa Mbinguni.
Katika vikao viwili, vijana elfu moja na mia mbili walifunzwa, walipata msukumo, waliimarisha imani yao, walihisi muunganiko na vijana wengine Watakatifu wa Siku za Mwisho na walipendwa na viongozi na washauri. Maoni kutoka kwa baadhi ya vijana yanafuata:
Misanya Sharon – 17: Nilikuwa na hofu ya kuondoka nyumbani kwenda kuhudhuria KNV, ilikuwa mara yangu ya kwanza na sikutaka kuiacha familia yangu kwa sababu ni mahali ambapo ninahisi kupendwa na ninahisi salama, hivyo kwenda KNV kwa siku 5 hakika ilinipa hofu. Lakini, wakati wa KNV ndipo nilipokuza ujasiri mkubwa. Sasa ninaweza kusimama imara kwenye umati mkubwa na kushiriki umaizi pamoja na wengine. KNV ilikuwa kama nyumbani - nilihisi kupendwa na kila mtu. Nilikuwa salama. Niliwatazama viongozi vijana wakati wa KNV wakiburudika, wakifunza kwa mfano na kutuhudumia kwa upendo na subira.
Omoriti Cyprian – 18: Wakati wa KNV ndipo nilipotambua umuhimu wa kusoma maandiko kila siku kwa sababu kila asubuhi, tulishiriki katika kujifunza injili. Nilijifunza mengi mimi binafsi na kutoka kwa wengine, niligundua mambo mengi kutoka kwenye maandiko. Tangu wakati huo tamanio langu kwenye usomaji maandiko kila siku limeongezeka.
Jane Lugosi –16: Nimekuza tamanio la kuwasaidia wamisionari kwa sababu ninataka wengi wa rafiki zangu wajiunge na kanisa ili kwamba wapate kufurahia kile nilichofurahia wakati wa KNV. Ulikuwa uzoefu mzuri na daima nitawaambia rafiki zangu kuhusu kanisa na nitatoa ushuhuda wangu mara kwa mara. Nilifurahia shughuli zote za KNV. Hakika, mimi ni mwanafunzi wa Yesu Kristo.