“Kuwa wa Sehemu ya Mpango wa Mungu na wa Hekaluni,” Liahona, Machi 2025.
Kuwa wa Sehemu ya Mpango wa Mungu na wa Hekaluni
Kanuni tatu zinatukumbusha kwamba sisi sote tunaweza kupokea baraka ambazo Mungu hutoa kwa watoto Wake.
Picha ya Hekalu la Barranquilla Colombia na Leslie Nilsson
Nilikaa katika kikundi cha waumini wa Kanisa. Hatukuwahi kukutana kabla, lakini sote tulikuwa na kitu kimoja kinachofanana: tulikuwa waseja.
Sasa, nataka kurudi nyuma kwa sekunde. Katika injili ya Yesu Kristo, hatutambuliwi kwa vibandiko. Utambulisho wetu wa kweli, Rais Russell M. Nelson alifundisha, ni kwamba sisi “kiuhalisia ni watoto wa kiroho wa Mungu.” Ninaelewa kwamba kwa sababu ya umuhimu tunawaita baadhi ya waumini wa Kanisa waseja. Kuna sababu za kiutendaji za hilo. Lakini wakati mwingine, kama ilivyoonekana kuwa suala katika hali hii, inaweza kuchangia kuwafanya waumini kujisikia kama watu wa nje. Inaweza hata kufanya iwe vigumu kwao kujisikia wamejumuishwa kikamilifu katika baraka za Mungu za wokovu na kuinuliwa.
Unaona, tulikuwa tunazungumza kuhusu hekalu—na baadhi ya watu katika kundi walihisi kwamba kuwa mseja kuliwatenga kutokana na kupokea utimilifu wa baraka za hekaluni. Ninaelewa; wakati unapokuwa hujaoa au kuolewa katika Kanisa ambalo kitovu chake ni familia, inaweza kuwa vigumu kuona jinsi unavyofaa. Lakini pia najua kwamba Bwana hahukumu kama mtu anastahili kupokea baraka zilizoahidiwa kulingana na mwonekano au vitambulisho vya nje. Yeye “hutazama moyo” (1 Samweli 16:7) na hufanya baraka Zake zipatikane kwa wote wanaochagua kumfuata Yeye. Ninaamini hili kwa moyo wangu wote. Kwa hiyo, kwa hilo akilini, hizi ni kanuni tatu za kuwasaidia Watakatifu wa Siku za Mwisho ambao hawajaoa au kuolewa kujua kwamba wao ni sehemu ya mpango wa Mungu na wa hekaluni.
1. Mungu alisanifu mpango Wake kwa ajili ya kila mmoja wa watoto Wake.
Kwa sababu agano jipya na lisilo na mwisho la ndoa linahitajika kwa ajili ya kuinuliwa, inaweza kuonekana kwamba mpango wa Mungu haukufanywa kwa ajili ya wale ambao hawajaoa au kuolewa (ona Mafundisho na Maagano 131:1–3). Lakini Mzee Patrick Kearon alifundisha: “Mpango mzuri wa Baba Yetu, hata ‘mpango Wake mzuri’, umesanifiwa ili kukuleta wewe nyumbani, sio kukuweka nje. Hakuna mtu aliyejenga kizuizi na kumweka mtu pale wa kukugeuza na kufukuza. Hakika, ni kinyume kabisa. Mungu yuko katika kukutafuta wewe bila kusita. Yeye ‘anataka watoto Wake wote wachague kurudi Kwake,’ na Yeye anatumia kila njia inayowezekana kukurudisha Kwake.”
Mungu hakusudii kuwafukuza wale hawajaoa au kuolewa wasifurahie baraka alizotoa. Rais M. Russell Ballard (1928–2023), Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alifundisha, “Maandiko na manabii wa siku za mwisho wanathibitisha kwamba kila mtu ambaye ni mwaminifu katika kushika maagano ya injili atakuwa na fursa ya kuinuliwa.” Kila nafsi ina thamani kubwa machoni pa Baba wa Mbinguni—kiasi kwamba alimtuma Mwanawe wa Pekee kufa na kutukomboa sisi sote kutokana na dhambi ili tuweze kuwa na zawadi ya uzima wa milele (ona Yohana 3:16–17; Mafundisho na Maagano 18:10–12).
Kama maisha yatajifunua tofauti kuliko ilivyotarajiwa, tunaweza kujikuta tukitilia shaka madhumuni yetu katika mpango wa Mungu. Hata hivyo mpango Wake kamwe haukuhakikishia maisha yetu wote tungefanana. Hatujui ni shangwe gani, kuchanganyikiwa, mafanikio, au maumivu ya moyo yanaweza kutujia. Rais Dallin H. Oaks, Mshauri wa Kwanza katika Urais wa Kwanza, alisema, “Kuna mengi sana hatujui kwamba tegemeo letu pekee la uhakika ni kumtumaini Bwana na upendo Wake kwa watoto Wake.”
Yawezekana tusijue kwa nini njia yetu inaonekana jinsi inavyoonekana hivi sasa. Lakini kumtumainia Mungu na katika upendo Wake kunaweza kuleta uwazi kuhusu jinsi Yeye alivyosanifu mpango Wake kwa ajili ya watoto Wake wote—ikijumuisha wewe.
Picha ndani ya Kituo cha Wageni cha Hekalu la Roma Italia na Massimo Criscione
2. Hekalu linashikilia baraka binafsi kwa kila mtu.
Tunaweza kufikiria kuwa kuunganishwa kunatumika tu kwa mume na mke. Lakini pamoja na kuwaunganisha wanandoa na Bwana, kuunganisha huiunganisha familia milele. Kupitia kuunganishwa, watoto wote wa Mungu wanaweza kufurahia baraka za milele ikiwa watashika maagano yao.
Nguvu ya kuunganisha inahalalisha ibada zote za ukuhani mbinguni na duniani. Mzee D. Todd Christofferson wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili alifundisha: “[Nguvu ya kuunganisha] hufanya wokovu wa mtu binafsi na kuinuliwa kwa familia uwezekane ulimwenguni kote kwa watoto wote wa Mungu popote na kwa kipindi chochote walichoishi duniani. Hakuna theolojia au falsafa au mamlaka inayoweza kulingana na fursa hii inayo wajumuisha wote. Nguvu hii ya kuunganisha ni dhihirisho kamilifu la haki, rehema na upendo wa Mungu.” Baraka ambazo Bwana hutoa ni za mjumuisho mno kiasi kwamba zinapatikana kwa kila mtu ambaye atafanya na kushika maagano Naye.
Tunaweza kuelewa vyema jinsi mpango wa Mungu unavyojumuishwa wakati tunapoabudu katika nyumba ya Bwana. Kutumia muda hekaluni, Rais Nelson alifundisha, “kutakusaidia ufikirie selestia na kukamata ono la wewe ni nani hasa, unaweza kuwa nani na aina ya maisha ambayo unaweza kuwa nayo milele.” Pia alielezea kwamba kuabudu katika hekalu kutatupa ulinzi, ushuhuda imara, faraja, ufunuo binafsi, ongezeko la maarifa na nguvu, na uelewa mkubwa wa mpango wa Mungu.
Iwe tuko katika ndoa au waseja, hekalu linashikilia faida binafsi za kiroho kwa ajili yetu sote—ni mahali ambapo huimarisha na kuwapa nguvu wote wanaotamani ukaribu na Mungu. Kwa nyongeza, ona ubao wa pembeni “Uliowezeshwa na Ibada za Hekaluni.”
3. Hekaluni, tunaweza kuongeza kwa kina uhusiano wetu na Yesu Kristo.
Hekaluni, fokasi kuu ni Yesu Kristo. Yeye ndiye kitovu cha mpango wa Mungu na ndiyo sababu sisi sote tunaweza kupokea wokovu na kuinuliwa. Rais Nelson alifundisha: “Nyumba ya Bwana ni nyumba ya kujifunza. Huko, Bwana hufundisha katika njia Zake mwenyewe. Huko kila ibada inafundisha kuhusu Mwokozi. Huko, tunajifunza jinsi ya kuifunua pazia na kuwasiliana kwa uwazi zaidi na mbingu. Huko, tunajifunza jinsi ya kumkemea adui na kuvuta nguvu za ukuhani wa Bwana ili zituimarisha sisi na wale tunaowapenda. Ni hamu kubwa iliyoje kila mmoja wetu anapaswa kuwa nayo ya kutafuta kimbilio huko.”
Tunaweza kupata kimbilio na kuwa wa sehemu ya hekalu kwa kumtafuta Mwokozi katika ibada na maagano. Kwa kufanya hivyo, tutapata ushahidi kwamba Yeye anatupenda na kwamba “wote ni sawa kwa Mungu” (ona 2 Nefi 26:33). Kwa sababu ya upendo Wake kwetu, Yeye anatutaka tuunde “uhusiano usio na mwisho” pamoja Naye na kupokea njia ya “aina maalum ya upendo na rehema” kupitia maagano yetu. Kama tutafanya na kushika maagano ya hekaluni, tunaweza kuimarisha uhusiano wetu na Yeye, wenye kutuletea “tumaini, shangwe, na msimamo wa kutumaini mema katika maisha yetu yote”—bila kujali hali zetu.