2025
Baba wa Mbinguni Anataka Kuzungumza Nawe.
Machi 2025


“Baba wa Mbinguni Anataka Kuzungumza Nawe,” Liahona, Machi 2025.

Baba wa Mbinguni Anataka Kuzungumza Nawe

Acha imani yako kwa Baba wa Mbinguni na Mwanawe Mpendwa ikusaidie kuifunua pazia na kupokea sauti ya Baba.

msichana akisali

Sisi ni wana na mabinti wa Mungu, tukishiriki dunia pamoja kutoka nyumbani kwetu mbinguni. Haya ni maisha yetu ya duniani, wakati wa kupokea mwili wetu, kuchagua mema dhidi ya maovu, “kuonja uchungu, ili [sisi] tujue kuthamini mema” (Musa 6:55), kukuza imani yetu katika Mwokozi wetu Yesu Kristo na Upatanisho Wake mtakatifu, na kukumbatia mpango wa furaha wa Baba yetu. Tuko hapa ili kuwa zaidi kama Baba yetu wa Mbinguni.

Bila kumbukumbu ya maisha yetu kabla ya kuja duniani, sisi, wakati mwingine, tunahisi upweke kwa ajili ya ulimwengu tulioacha nyuma. Baba yetu ametupatia zawadi ya kiroho ya kubaki tumeunganishwa Kwake na kupokea mwongozo, maelekezo, na faraja kutoka Kwake. Tunaijua zawadi hii vizuri sana; inaitwa sala.

Sali kwa Baba yako wa Mbinguni

Kwa Adamu na Hawa na wote wangewafuata, malaika alielekeza, “Nawe utatubu na kumlingana Mungu katika jina la Mwana milele yote” (Musa 5:8).

Yesu alifundiisha “Ombeni, nanyi mtapewa; tafuteni, nanyi mtaona; bisheni, nanyi mtafunguliwa” (Mathayo 7:7). “Usalipo, … sali kwa Baba yako … sirini” (Mathayo 6:6). “Basi ninyi salini hivi: Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzwe” (Mathayo 6:9).

Yesu daima alisali kwa Baba Yake “Aliondoka akaenda mlimani ili kuomba, akakesha usiku kucha katika kumwomba Mungu”(Luka 6:12). “Na … akaenda zake mlimani kuomba” (Marko 6:46). “Wakafika mahali palipoitwa Gethsemane; akawaambia wanafunzi wake, Ketini hapa, muda niombapo” (Marko 14:32). Akiwa msalabani, Yesu aliwaombea askari waliomsulubisha: “Baba, wasamehe; maana hawajui watendalo” (Luka 23:34).

Maandiko yanatushauri “kesheni ninyi kila wakati, mkiomba” (Luka 21:36; 2 Nefi 32:9; 3 Nefi 18:15; Mafundisho na Maagano 10:5; 19:38; 20:33; 31:12). Shauriana na Bwana kwenye matendo yako yote, na atakuongoza kwa yale mema” (Alma 37:37). Kwa nyongeza, “tunatoa shukrani zote na sifa ambazo nafsi [zetu] zote zina uwezo wa kuwa nao” (Mosia 2:20), tukitambua yale yote ambayo Baba yetu anafanya kwa ajili yetu.

Rais Russell M. Nelson alieleza: “Kujithamini kiroho huanza na utambuzi kwamba kila asubuhi mpya ni zawadi kutoka kwa Mungu. … Anatuhifadhi siku baada ya siku na kututegemeza kutoka wakati mmoja hadi mwingine (ona Mosia 2:21).”

Nefi alisema “Kwani ikiwa mtasikiliza Roho ambaye anawafundisha wanadamu kusali, mtajua kwamba lazima msali; kwani roho mchafu hawafundishi mwanadamu kusali, lakini humfundisha kwamba lazima asisali.(2 Nefi 32:8).

mwonekano wa wasifu wa Mwokozi

Maelezo kutoka Kristo Akimfufua Binti wa Yairo, na Greg K. Olsen.

Kwa mfano wa Mwokozi wetu na ushauri wa malaika na manabii kupitia karne nyingi, tunajua wazi kusali kila siku kuonyesha shukrani kwa ajili ya baraka zetu, na kuweka sala katika mioyo yetu daima. Tunalo jukumu la kuwasiliana na Baba yetu.

Lakini hata mtukufu zaidi, Baba yetu wa Mbinguni hujibu maombi yetu. Swali la kufikiria katika ulimwengu huu wa duniani ni, ni kwa jinsi gani tunapokea vyema na kuelewa majibu, maelekezo, na faraja inayotoka kwa Baba yetu?

Kupitia zaidi ya miongo yangu saba ya maisha, ninajua kwamba Baba yetu anazungumza nasi. Hatuko peke yetu. Viumbe wa mbinguni hutulinda na kutusaidia tunapotafuta kumfuata Mwokozi.

Kupokea majibu ya maombi ya sala zetu huanza na imani yetu katika Baba yetu wa Mbinguni na Mwanawe, Yesu Kristo. Yesu alisema, “Usiogope, amini tu” (Marko 5:36). Tunamwamini Yeye, tunafanya kadiri tuwezavyo kutii amri, na kutafuta mkono Wake katika mambo yote. “Katika lo lote mwanadamu hamkosei Mungu … isipokuwa wale wasiokiri mkono wake katika mambo yote, na wasiotii amri zake” (Mafundisho na Maagano 59:21).

Mkono wa Mungu katika maisha yetu haimaanishi kwamba Yeye ndiye husababisha maovu au majanga ya kutisha ambayo yapo katika ulimwengu wetu. Hata hivyo, inamaanisha kwamba katika nyakati zako za shida na ukosefu wa haki, Yeye atasimama nawe, ataimarisha uwezo wako, kukufariji, na “kuweka wakfu masumbuko yako kwa faida yako” (2 Nefi 2:2).

Sikia Sauti Yake

Tunapokuwa na imani Kwake na kutii amri Zake, kiuhalisia tunajifunza kuisikia sauti Yake vizuri zaidi.

Mnamo Septemba 1993, mwaka wangu wa kwanza kama Kiongozi Mkuu Mwenye Mamlaka, Rais James E. Faust (1920–2007), wakati huo akiwa mshiriki wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alimwalika mke wangu, Kathy, na mimi kuhudhuria ibada ya Chuo Kikuu cha Brigham Young pamoja naye. Kumbuka, 1993 ilikuwa kabla ya kupatikana kwa simu janja, mitandao ya kijamii, na intaneti.

Katika hotuba yake, yenye kichwa cha habari “Sauti ya Roho,” Rais Faust alionya: “Katika kizazi chenu utazuiliwa na sauti nyingi zikikuambia jinsi ya kuishi, jinsi ya kuridhisha tamaa zako, jinsi ya kuwa na yote. Utakuwa na hadi vituo vya televisheni mia tano kwenye ncha za vidole vyako. Kutakuwa na aina zote za programu, modemu za kompyuta zinazoingiliana, hifadhidata, na bodi za matangazo; kutakuwa na uchapishaji wa eneokazi, wapokeaji wa setilaiti, na mitandao ya mawasiliano ambayo itakupa taaifa nyingi kupita kiasi … Sauti ambayo lazima ujifunze kuitii ni sauti ya Roho.”

Rais Boyd K. Packer (1924–2015), Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, alifundisha juu ya sauti ndogo, tulivu ya Roho katika kusimulia uzoefu wa John Burroughs, mtu wa mazingira, alipokuwa akitembea na marafiki kupitia bustani iliyojaa watu. Haya ni maneno ya Rais Packer:

“Juu ya sauti za maisha ya jiji [Bw. Burroughs] alisikia wimbo wa ndege.

“Alisimama na kusikiliza! Wale waliokuwa naye hawakusikia. Yeye aliangalia huku na huko. Hakuna mtu mwingine aliyetambua.

“Ilimsumbua kwamba kila mtu anapaswa kukosa kitu kizuri sana hivyo.

“Alichukua sarafu kutoka mfukoni mwake na kuirusha angani. Ilipiga sakafu na pete, siyo sauti kubwa zaidi kuliko wimbo wa ndege. Kila mtu akageuka; wangeweza kusikia hiyo!

“Ni vigumu kutenganisha na sauti zote za magari ya jiji wimbo wa ndege. Lakini unaweza kusikia. Unaweza kusikia kwa uwazi kama unajifundisha mwenyewe kuisikiliza.”

Mafundisho ya Rais Packer ya Roho Mtakatifu yalitokea mwaka 1979, wakati ambapo maisha yalikuwa ya ukimya zaidi na kelele za ulimwengu zilikuwa zimefifia zaidi kuliko ilivyo sasa.

Rais Nelson alifundisha, “Ikiwa unatilia maanani sana malisho kutoka kwenye mitandao ya kijamii kuliko ulivyo kwa minong’ono ya Roho, basi unajiweka katika hatari ya kiroho.”

Rais Faust alisema, “Kama tunataka kuisikiliza sauti ya Roho, sisi pia lazima tufungue masikio yetu, tufungue jicho la imani hata kwenye chanzo cha sauti, na kutazama kwa uimara kuelekea mbinguni.”

Sauti hii ya Roho huja kwa vyote viwili akili zetu na hisia zetu. “Nitakujulisha wewe akilini mwako na katika moyo wako, kwa njia ya Roho Mtakatifu, ambaye atakujia na ambaye atakaa moyoni mwako” (Mafundisho na Maagano 8:2). Sikiliza dhamiri yako—ufunuo mara nyingi huanza huko.

Mzee Andersen akizungumza na kikundi

Wakati wa ziara ya Girls’ Home Boys’ Town Complex huko Markina City, Ufilipino, mnamo Februari 2024, Mzee Andersen aliwafundisha vijana kwamba wao ni watoto wa Mungu: “Anawapenda. Ninyi Na unaweza kumwomba Yeye. Yeye atasikia sala zako.

Sali kwa Moyo wa Kuamini

Majibu na misukumo haiwezi kulazimishwa. Tunasali na tunasubiri kwa moyo wa kuamini. Baadhi ya majibu hayatakuja katika maisha haya, lakini kwa wenye haki, Bwana daima atatuma amani Yake (ona Yohana 14:27). Majibu mara nyingi huja tunapoomba ili kuwasaidia wale wanaotuzunguka. Wakati mwingine, yanakuja “mstari juu ya mstari, kanuni juu ya kanuni” (Mafundisho na Maagano 98:12).

Sauti ya mbinguni inaweza kutujia katika nyakati zisizotarajiwa na katika maeneo yasiyotarajiwa, lakini tunapata fursa zetu nzuri katika nafasi tulivu na sehemu takatifu. Katika utulivu wa sala zangu za mapema asubuhi na kutafakari, ninapata baraka zisizo za kawaida. Usomaji binafsi wa maandiko kila siku, usiokatizwa, wakati mwingine, huleta sauti ya Roho ndani ya mioyo yetu kama moto wakati mwingine.

Nyakati zingine, misukumo ni mahususi kutokana na kile tunachosoma, na wakati mwingine, kile tunachotafakari huleta jibu kwa wasiwasi tofauti sana. Kumbuka maneno ya Mzee Robert D. Hales alisema:“Tunapotaka kuzungumza na Mungu, tunasali. Na wakati tunapotaka Yeye azungumze nasi, tunayapekua maandiko.”

Wakati kelele na vivuruga mawazo vya duniani vikituzunguka, Bwana amemwelekeza nabii Wake kujenga mahekalu zaidi na zaidi. Katika nyumba hizi takatifu za Bwana, tunapoacha changamoto zetu nje lakini tukiingia na maombi na wasiwasi wetu, tunafundishwa kweli za milele.

Mwaka mmoja uliopita, Rais Nelson alitupa ahadi hii ya ajabu: “Wapendwa kaka zangu na dada zangu, hapa kuna ahadi yangu. Hakuna kitakachokusaidia ushikilie kwa nguvu zaidi kwenye fimbo ya chuma kuliko kuabudu hekaluni mara nyingi kadiri hali zinavyoruhusu. Hakuna kitakacho kulinda zaidi wakati unapokumbana na ukungu wa giza wa ulimwengu. Hakuna kitakacho imarisha ushuhuda wako juu ya Bwana Yesu Kristo na Upatanisho Wake au kukusaidia uelewe zaidi mpango mtakatifu wa Mungu zaidi. Hakuna kitakachoipa faraja zaidi roho yako nyakati za maumivu. Hakuna kitakacho fungua mbingu zaidi. Hakuna kitu!”

Kila mkutano mkuu huleta baraka za ziada tele. Katika mwezi ujao wa Aprili, kwa mara nyingine tena, tutakutana katika mkutano mkuu kusikia sauti ya Bwana. Tunakuja kwenye mkutano mkuu tukiwa tumesali na kujiandaa. Kwa wengi wetu, kumekuwa na hofu nzito na maswali ya dhati. Sisi tunakuja kufanya upya imani yetu katika Mwokozi, Yesu Kristo, na kuimarisha uwezo wetu wa kuzuia majaribu na kuepuka majaribu. Tunakuja kufundishwa kutoka Juu. Ninawaahidi kwamba mnapojiandaa na kuja kwa maombi kwenye vikao vya mkutano mkuu, mtahisi majibu ya wasiwasi wenu, na mtajua kwamba “mkono wa mbinguni” u juu yenu.

Muwe na imani kwamba Baba yenu wa Mbinguni anazungumza nanyi. Ndiyo! Acha imani yako Kwake na kwa Mwanawe Mpendwa ikusaidie kulifunua pazia na kupokea sauti ya Baba yako. Ninashuhudia Yeye yupo na anawapenda zaidi ya maneno yanavyoweza kusema.

Mihutasari

  1. Russell M. Nelson, “Shangwe Huja Asubuhi,” Ensign, Nov. 1986, 68.

  2. James E. Faust, “The Voice of the Spirit” (Brigham Young University devotional, Sept. 5, 1993), 2, 3, speeches.byu.edu.

  3. Boyd K. Packer, “Prayers and Answers,” Ensign, Nov. 1979, 19.

  4. Ona Russell M. Nelson na Wendy W. Nelson, “Tumaini la Israeli” (worldwide youth devotional, Monday, June 03, 2018), Gospel Library.

  5. James E. Faust, “Sauti ya Roho,” 4.

  6. Robert D. Hales, “Holy Scriptures: The Power of God unto Our Salvation,” Liahona, Nov. 2006, 26–27.

  7. Russell M. Nelson, “Furahia Katika Zawadi ya Funguo za Ukuhani,” Liahona, Mei 2024, 122.

  8. Ona Neil L. Andersen, “Sauti ya Bwana,” Liahona, Nov. 2017, 126.