2025
Njia Yangu ya Kuvumilia kwa Subira
Machi 2025


“Njia Yangu ya Kuvimilia kwa Subira,” Liahona, Machi 2025.

Sauti za Watakatifu wa Siku za Mwisho

Njia Yangu ya Kuvumilia kwa Subira

Nilijiuliza kwa nini ninapaswa kutumikia kwa moyo wangu wote na nafsi yangu ikiwa kufanya hivyo kulileta majaribu.

msichana mkubwa akitabasamu

Picha ya mwandishi na Shaun Sutton

Niliporudi nyumbani upande wa kusini mwa Ufilipino mwaka 2016 baada ya kuhudumu misheni ya heshima huko Ufilipino kaskazini, nilikuwa nikitazamia kuhudhuria Chuo Kikuu cha Brigham Young–Hawaii na kupata uzoefu wa matukio mengine yote yanayowasubiri vijana wakubwa.

Ghafla, hata hivyo, nilianza kupoteza uzito. Daktari wangu alitambua hyperthyroidism. Alinishtua kwa madhara kama ugonjwa huo hautatibiwa.

Licha ya matibabu, mwili wangu ulianza kubadilika. Macho yangu yakaanza kuvimba, na nikawa mwembamba sana. Niliepuka kupigwa picha na hata kuangalia kwenye kioo kwa sababu ya muonekano wangu.

Dawa taratibu zikaanza kusaidia. Lakini miaka mitatu baadaye, niligundulika kuwa na ugonjwa wa pili—ugonjwa wa mfadhaiko. Magonjwa haya mawili yaliniibia kujiamini. Nilihangaika kutoka kitandani kwenda kuhudhuria shule, na nilihisi nisiyeweza kuhudumu Kanisani.

Nilikasirika kwamba Mungu aliruhusu hili litokee. Nilijiuliza kwa nini ninapaswa kutumikia kwa moyo wangu wote na nafsi yangu yote kama kufanya hivyo kulileta majaribu? Nilipata faraja, hata hivyo, kutoka kwa maneno haya ya Rais Jeffrey R. Holland, Kaimu Rais wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili: “Akili zilizovunjika zinaweza kuponywa kama vile tu mifupa iliyovunjika na mioyo iliyovunjika inavyoponywa.” Nililia niliposikia maneno hayo. Nilikuwa na akili iliyovunjika ambayo ilihitaji uponyaji.

Nililelewa katika nyumba ya uaminifu, na imani yangu kwa Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo ilibaki imara licha ya maumivu na kutokuwa na uhakika. Pole pole, nilikubali na kuzoea hali yangu mpya.

Sasa, miaka minane baadaye, sijapunguzwa ari tena na maradhi yangu. Ninayakubali kama sehemu ya maisha. “Ninahisi mzima. Ninaweza kuhudumu na kuishi maisha kikamilifu, ingawa changamoto za kiafya zinaweza kuendelea maisha yangu yote. Nimejifunza kwamba kuvumilia kwa subira ni sehemu ya maisha ya duniani (ona Mafundisho na Maagano 121:7–8). Ninajifunza kunywa kikombe changu kichungu na kubaki imara.

Sasa ninafanya kazi katika idara ya wafanyakazi ya kampuni ya akili mnemba na kuchukua madarasa ya mtandaoni usiku kutoka Chuo Kikuu cha Brigham Young–Pathway Worldwide. Nimeacha kuuliza “Kwa nini mimi?” na nimeanza kuuliza “Ninaweza kujifunza nini? Ninawezaje kunufaika kutokana na uzoefu huu?”

Nikitazama nyuma, ninaona kwamba Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo walikuwa pamoja nami kote njiani. Kwenda mbele, ninajua ni katika nani ninaweza kuamini (ona Mithali 3:5–6; 2 Nefi 4:34).