2025
Je, Mimi ni Mwema vya Kutosha?
Machi 2025


“Je, Mimi ni Mwema vya Kutosha?,” Liahona, Machi 2025.

Picha za Imani

Je, Mimi ni Mwema vya Kutosha?

Nilidhani ningepata imani, upendo, na ukweli wa kiroho kwa kuishi mtindo mbadala wa maisha. Sikupata. Niliipata ndani ya Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na hekaluni.

mtu amekaa katika ofisi ya nyumbani

Picha na Leslie Nilsson

Nilipokuwa kijana wa miaka kumi na kitu hivi katika miaka ya 1960, Vita ya Vietnam ilikuwa inapamba moto. John F. Kennedy alikuwa ameuawa, kama ilivyokuwa kwa Martin Luther King Jr. na Robert Kennedy. Niliasi dhidi ya wazazi wangu na desturi zote na taasisi zote za siku hizo. Sikutaka kuolewa au kuwaleta watoto katika ulimwengu ambao ulikuwa wa vurugu sana, usio wa uaminifu, na wa kudharauliwa.

Niliacha shule ya upili mwaka wangu wa kwanza, nikahamia Wilaya ya Haight Ashbury ya San Francisco, California, Marekani, na kuishi maisha ya hippie kutoka 1969 hadi 1972. Nilikaa katika jumuiya, nilifanya kazi zo zote zile ambazo ningeweza kupata, na kukumbatia maisha ya udhanifu na kuamini katika anasa ndio mtindo wa maisha, ikijumuisha utumiaji wa dawa za kulevya.

mvulana akiwa na nywele ndefu na ndevu

Wakati Randy alipokuwa kijana wa miaka kumi ya kuni na kitu hivi, alifikiri maisha yake hayakuwa na siku za usoni zenye furaha. “Niliasi dhidi ya wazazi wangu na tamaduni zote na taasisi zote za siku,” anasema.

Wakati huo huo, nilikuwa nikitafuta imani, upendo, na ukweli wa kiroho. Nilitafakari na kujifunza dini tofauti, nikitoa kutoka kwao chochote ambacho kilinigusa kama kweli au cha thamani. Utafutaji wangu wote, hata hivyo, uliisha katika kuchanganyikiwa. Kaka yangu, John, akijua kuhusu upekuzi wangu, alinitumia Kitabu cha Mormoni.

“Unapaswa kusoma hiki,” aliandika John, ambaye alikuwa amejiunga na Kanisa mapema.

Nilipofukuzwa kwa kusoma Kitabu cha Mormoni katika kazi yangu kwenye kituo cha gesi, nilifikiri, “Hiki hakiwezi kuwa kizuri.” Nilikitupilia mbali kitabu.

Si muda mrefu baadaye, John aliniambia alikuwa anakuja katika Eneo la San Francisco Bay na kundi la kuimba kutoka Chuo Kikuu cha Brigham Young.

“Ningependa kukuona,” alisema, akipendekeza tukutane katika Hekalu la California Oakland.

Nikiendesha gari kuzunguka Eneo la Bay usiku, mara nyingi ningeliona hekalu. Ilinivutia kiroho, kwa hivyo nilisoma kuhusu hilo na nilitaka kuingia ndani. John na mimi tulikutana mapema asubuhi moja kwenye viwanja vya hekalu. Baada ya maongezi yetu, alisema ulikuwa wakati wa kundi lake kuingia hekaluni.

“Randy, hutaweza kuingia hekaluni,” John aliniambia.

“Najua, mimi ni hippie,” nilijibu, “lakini nimejifunza dini za Mashariki, mimi ni mla mboga za majani, ninaishi katika jumuiya ambapo tunashiriki kila kitu, na nina $ 20. Ni kiasi gani cha kiingilio kinaweza kuwa?”

“Zaidi ya hilo,” John alijibu. “Wewe siyo mwema vya kutosha.”

Wakati huo, nilijifikiria mwenyewe kiakili, kifalsafa, na kiroho kuwa nimesonga mbele. Ni kwa jinsi gani mimi sio mzuri vya kutosha?

Kujazwa na Tumaini

Kwa miaka kadhaa, wazazi wangu hawakujua ni wapi nilipokuwa. Walikuwa watu wema ambao walijaribu kunipa elimu bora iwezekanavyo na walieleweka kusikitishwa na chaguzi zangu. Wakati baba yangu alipougua, mama yangu alinishawishi nirudi nyumbani Washington, D.C. Nilipofika, John alinipata kazi ya wafanyakazi kujenga Hekalu la Washington D.C.

Sikujua, lakini alikuwa amepanga kwa ajili yangu kufanya kazi na wafanyakazi wa wamisionari waliorejea. Nilishangazwa kwamba John Howell, msimamizi kiongozi, angemwomba mshiriki wa wafanyakazi kusali mwanzoni mwa kazi ya kila siku—kitu ambacho sikuwahi kuona na wafanyakazi niliofanya kazi nao hapo awali.

Siku moja kazini, baadhi yetu tulikuwa tukisimamisha mojawapo ya milango mizito ya mbele ya hekalu ilipoanguka na kusaga kidole changu kikawa chembamba kama sarafu. John alinikimbilia, akaangalia kidole changu, akaiita aletewe mafuta yaliyo wekwa wakfu, na kunipa baraka. Kidole changu kilipona haraka kiasi kwamba sikuhitaji kumwona daktari.

Katika tukio jingine, nilipewa wembe wa kunyolea na kuambiwa kwangua chembechembe za vifusi kutoka kwenye sakafu ya zege.

“Kwa nini?” Nilimuuliza mmoja wa wafanyakazi wetu. “Je, hawajaweka zulia chini?”

“Randy, hujui nyumba hii ni ya nani, unajua?” yeye alijibu. “Tunaikamilisha kwa ajili ya Yule aliye Mkamilifu.”

Ulimwengu ulikuwa unazama katika ubeuzi, uchungu, chuki, na hofu, mfano na mafundisho ya vijana hawa niliofanya nao kazi yalinijaza matumaini. Wakati wafanyakazi waliposhiriki imani yao na mimi, nilijua walikuwa waaminifu na halisi. Walikuwa wametoa miaka miwili ya maisha yao kuwahudumia wengine, na walikuwa na matumaini kiakili. Nilitaka mafundisho yao yawe ya kweli. Nilihisi nilikuwa nikipata mwangaza niliokuwa nikiutafuta na kwamba Bwana alikuwa akinitayarisha kiroho.

John Howell alipendekeza nikutane na wamisionari. Badala yake, nilichagua kuwa na kaka yangu na mmoja wa rafiki zake, mmisionari mwingine aliyerejea, wanifundishe. Walipokuwa wakinifundisha, nilitaka ushahidi wa nje, usioweza kupingika kwamba kile nilichokuwa nikijifunza kilikuwa cha kweli. Bila uthibitisho huo, sikutaka majadiliano yoyote zaidi.

Nilipouliza walijuaje ukweli, walijibu, “Tumesoma na kuomba na kuhisi ushahidi kutoka kwa Roho Mtakatifu.” Waliniambia nilihitaji ushahidi kama huo.

Usiku ule niliingia katika kijisitu cha miti karibu na mtaa wangu. Sijui ni kwa muda gani nilisali, lakini nilifanya hivyo kwa kusudi kamili. Nilimwuliza Mungu maswali yale yale manne: “Je, Kitabu cha Mormoni ni neno la Mungu? Je, Wewe na Mwanao mlimtotea Joseph Smith? Hili ni Kanisa la kweli la Yesu Kristo! Je, mimi ni mwema vya kutosha kuwa muumini?”

Jibu kwa kila swali lilikuja kwa mnong’ono kwenye nafsi yangu—“Ndiyo”—mara nne. Minong’ono hiyo iliambatana na hisia tulivu na tukufu.

Kwa kichwa changu kikiwa kimeinamishwa, nikipiga magoti katika sala na nikiwa nimelowa machozi, nilisema kwa mshangao: “Kama hili ndilo jibu Utakalonipa, basi nalikubali na nitayatoa maisha yangu kikamilifu Kwako na kwa injili hii kama Wewe unavyonifunulia.” Maneno hayawezi kuelezea mawazo, hisia, na kweli ambazo zilinifunika.

Ushahidi niliopokea usiku huo ulikuwa haupingiki, na ni imara sasa kama ilivyokuwa wakati huo. Tangu sala hiyo, Mungu amethibitisha hayo majibu kwangu katika maelfu ya njia za kimiujiza na za vitendo.

mwandishi kama mvulana

“Kanisa ni muujiza,” anasema Randy, alipiga picha hapa mwezi mmoja baada ya ubatizo wake. “Na maisha yangu katika Kanisa yamekuwa ya kimiujiza.”

Moto Uliwaka Ndani Yangu

Mara baada ya kubatizwa mnamo 1974, nilihudhuria mkutano wangu mkuu wa kwanza jijini Salt Lake pamoja na kaka yangu, John. Nilishangazwa wakati Mzee Boyd K. Packer (1924–2015) wa Akidi ya Mitume Kumi na Wawili, ambaye alikuwa amekutana na shangazi yangu katika Jiji la New York wiki tatu kabla ya mkutano ule, alimtaja John na mimi wakati wa mahubiri yake ya Jumapili asubuhi.

Akimnukuu shangazi yangu, Mzee Packer alisema: “Wapwa zangu wawili wamejiunga na Kanisa lenu. Siwezi kuamini badiliko ambalo limefanywa katika maisha yao.”

Kwa sababu ya badiliko hilo kubwa (ona Alma 5:14), moto uliwaka ndani yangu ambao nilitaka kuushiriki. Punde, nilijikuta huko Idaho kama mmisionari. Nusu ya muda wa misheni yangu, baba yangu, ambaye alikuwa shujaa wangu mkuu na rafiki yangu wa dhati, alifariki. Mama yangu alimpigia simu rais wangu wa misheni na akaomba nirudi nyumbani nimzike. Wakati rais wangu wa misheni aliponiachia uamuzi wa kuondoka au la, nilimwambia nilitaka kusali na kufunga kwa saa 24 kabla ya kuamua.

Usiku ule alipata ndoto. Baba yangu alinitokea. Katikati ya majadiliano matukufu na yenye maana pamoja naye, aliniambia, “Mwanangu, kaa katika misheni yako.”

Nilifuata ushauri wa Baba na nikabaki.

Mvulana akiwa mmisionari

Kwa sababu ya mabadiliko makubwa ambayo yalifuata uongofu wake, “moto uliwaka ndani” ya Randy kiasi kwamba alitaka kushiriki kama mmisionari.

Miezi sita baada ya misheni yangu, nilishika mkono wa mama yangu alipovuta pumzi yake ya mwisho. Miongo kadhaa baadaye, mke wangu, Lisa, aliona barua kutoka kwa wazazi wangu katika kisanduku cha zamani. Baba alikuwa ameniandikia wakati wa misheni yangu lakini alikufa kabla ya kuituma.

“Mioyo yetu ilikuwa na iko na daima itakuwa imejaa upendo kwako. Ninatambua kwamba mambo daima hayajakuwa makamilifu, lakini hayo ni maisha. … Kristo hakusema, ‘Nifuate na itakuwa rahisi.’ Alisema, ‘Chukua msalaba [wako], na unifuate’ [Mathayo 16:24]. Alibeba msalaba, lakini sisi sote tuna vipasuko vyetu. Pengine nafasi yetu mbinguni itategemea jinsi tunavyoshughulikia yetu. Mwanna wetu tunakupenda sana.”

Kile Nilichokuwa Natafuta

Nikikua, nilikuwa mgumu kwa wazazi wangu, lakini sikuwahi kuwa na shaka na upendo wao. Tangu kupata Kanisa, nimefanya kazi kwa bidii kuwashukuru na kuwaheshimu.

Mnamo Februari 17, 2018, wiki mbili kabla ya Hekalu la Washington D.C. kufungwa kwa ukarabati, niliunganishwa na baba na mama yangu, miaka 42 baada ya wao kuvuka upande wa pili wa pazia kuingia umilele. Mwanangu mkubwa, William, alisimama kwa niaba ya baba yangu, na Lisa alisimama kwa niaba ya mama yangu. Nilihisi kwamba wazazi wangu, ambao walikuwa wameunganishwa wao kwa wao mapema, wote walikuwepo hapo kiroho.

Katika hekalu tunapata kamba ambazo zinatuunganisha milele na wapendwa wetu. Nina uhakika wa hilo.

Nilipokuwa mdogo, sikutaka kufunga ndoa au kupata watoto. Lakini leo mke wangu, watoto, na wajukuu ni hazina zangu kubwa. Kanisa ni muujiza, na maisha yangu katika Kanisa yamekuwa ya kimiujiza. Kama Joseph Smith, ninasema, “nisingepitia kile ambacho nimepitia, mimi mwenyewe nisingekiamini.”

Miaka hamsini iliyopita, nilikuwa mfanyakazi wa ujenzi kwenye Hekalu la Washington D.C. Niliaminishwa kwamba maisha yangu hayakuwa na siku za usoni zenye furaha. Leo mimi ni mfanyakazi wa ibada katika hekalu hilo hilo, nikiwa nimekubali mwaliko wa Bwana wa kumfuata Yeye, kupokea uponyaji Wake, kukumbatia ibada Zake, na kujitahidi kuwa kama Yeye.

mume na mke wamesimama pamoja na kutabasamu

Randy na mkewe, Lisa, wanahudumu katika Hekalu la Washington D.C. ambalo alisaidia kujenga miaka 50 iliyopita.

Picha na Leslie Nilsson

Kanisa lililorejeshwa siyo nadharia, falsafa, au jamii tu au utamaduni. Ni Kanisa la kweli la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

Nilidhani ningepata kile nilichokuwa nikitafuta huko San Francisco. Sikupata. Nilikipata katika Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho na katika nyumba ya Bwana, “taji la vito vya Urejesho.”

Muhtasari

  1. Boyd K. Packer, “Yule Aliyepewa Vingi, Mengi Yanahitajika,” Ensign, Nov. 1974, 87.

  2. Teachings of Presidents of the Church: Joseph Smith (2011), 525.

  3. Russell M. Nelson, “Maneno ya Kuhitimisha,” Liahona, Nov. 2019, 120.