Ujumbe wa Urais wa Eneo
Kufanya Kazi na Bwana kwenye Shamba Lake la Mzabibu
Katika mfano wa miti ya mizabibu ya mwituni na ile ya kawaida, katika Yakobo 5, Bwana anaulinganisha ulimwengu na shamba la mizabibu ambalo matunda yake ni watoto Wake, na katika mfano huo Yeye na wafanyakazi Wake wanafanya kazi kuhakikisha kwamba shamba la mizabibu linazaa matunda mazuri, au kwa maneno mengine, watoto waaminifu. Kuelekea mwishoni mwa mfano huo, tunasoma katika mstari wa 71, “Na Bwana wa shamba la mizabibu akawaambia: Nendeni, na mkatumikie shamba la mizabibu, kwa uwezo wenu. Kwani tazama, hii ndiyo mara ya mwisho nitakayolisha shamba langu la mizabibu; kwani mwisho unakaribia, na wakati unafika kwa haraka.” Bwana aliposema mwisho unakaribia anazungumza kuhusu siku yetu - muda tunaoishi hivi sasa. Hivi sasa, katika siku yetu, ni siku ya mwisho Bwana anatuma watumishi Wake kufanya kazi katika shamba Lake la mizabibu.
Na watumishi hawa ni akina nani? Jibu liko katika Mafundisho na Maagano, sehemu ya 4, mstari wa 3: “Kwa hivyo, kama unayo tamaa ya kumtumikia Mungu wewe umeitwa kwenye kazi hiyo.” Sisi sote ambao ni waumini kwa Kanisa la Yesu Kristo tunayo tamaa hii. Kama Alma alivyofundisha, kwa dhati tuliionyesha pale wakati wa ubatizo wetu, kupitia ibada hii takatifu, tulimwonyesha Bwana kwamba “[sisi] tunatamani kujiunga na zizi la Mungu, na kuitwa watu wake, na [tuko] radhi kubeba mizigo ya mmoja na ya mwingine, ili iwe miepesi; Ndio, na kuomboleza na wale wanaoomboleza; ndio, na kuwafariji wale wanaohitaji kufarijiwa, na kusimama kama mashahidi wa Mungu nyakati zote na katika vitu vyote, na katika mahali popote [tulipo]” (Mosiah 18:8–9).
Hivyo, sisi sote ni watumishi katika shamba la mzabibu la Bwana, tunaofanya kazi kuzileta au kuzirejesha nafsi kwake. Inatia moyo kwamba Yeye hatutumi huko peke yetu. Ndio, katika mstari wa 72 wa Yakobo 5, tunasoma: “na Bwana wa shamba la mizabibu akatumikia shambani pamoja nao.” Bwana yuko pamoja na wafanyakazi Wake, pamoja nasi, kama alivyoahidi tena kupitia kwa Joseph Smith, sehemu ya 84, mstari wa 88: “kwani nitakwenda mbele ya uso wenu. Nitakuwa mkono wenu wa kuume na wa kushoto, na Roho wangu atakuwa mioyoni mwenu, na malaika zangu watawazingira, ili kuwabeba juu.” Hatuko peke yetu; tuna washirika wazuri sana na imara!
Katika Eneo la Kati la Afrika, sisi ni mashahidi wa nguvu ya Bwana ya kusongesha kazi Yake mbele bila kujali vikwazo vyovyote. Amin, kama mstari wa 73 katika Yakobo 5 unavyotuhakikishia, “Na matunda ya kawaida yakaanza kukua tena pale katika shamba la mizabibu; na matawi ya kawaida yakaanza kukua na kufanikiwa sana.” Matawi ya kawaida—watoto waaminifu, waongofu kwenye injili, akina kaka na dada zetu wanaorejea, wale wote wanaochagua kuacha Mungu ashinde katika maisha yao—hawa wote watafanikiwa sana. Kufanikiwa sana, sio kidogo! Kwa maneno mengine, huu ni muda wa mwisho Bwana na watumishi Wake wanafanya kazi kwenye shamba la mizabibu, lakini sio kwa uchache!
Kinyume chake, kama Rais nelson alivyowakumbusha vijana wa Kanisa mnamo Juni 2018, “ukusanyaji huu ni kitu muhimu sana kinachotokea ulimwenguni leo. Hakuna chochote cha kulinganisha kwa ukubwa, hakuna chochote cha kulinganisha kwa umuhimu, hakuna chochote cha kulinganisha kwa utukufu. Na kama utachagua, kama ukitaka, unaweza kuwa sehemu yake kubwa. Unaweza kuwa sehemu kubwa ya kitu kikubwa, kitu kitukufu!” (Worldwide Youth Devotional • June 3, 2018)
Sisi sote ni watoto wa Baba wa Mbinguni. Sote tulichagua, katika baraza lile kuu katika maisha kabla ya kuja duniani, kusimamia ukweli na haki, na kumkubali Bwana kama Mwokozi na Mkombozi wetu! Kila mtu duniani alifanya uchaguzi huu na hivyo wanao ndani yao mwako wa imani, nuru ya Kristo. Hali za maisha na uzoefu, hata hivyo, wakati mwingine huweka kivuli kwenye nuru hii na hata kutishia kuzima mwako huu, na kufanya wasahau wao ni akina nani. Katika hili, Mzee Gary Sabin wa Sabini alitufunza kwamba “watu wanaingia matatizoni pale wanaposahau wao ni akina nani”. (Mawasiliano Binafsi)
Ni juu yetu, sisi, kupitia wema wa Bwana, kuwa na mwako wa imani uwakao ndani yetu ili kuwasha upya na kuendelea kufanya mwako uwake ndani ya mioyo ya wengine na kuwasaidia kutosahau kwamba wao ni watoto wa baba mpendwa ambaye ametengeneza mpango mkamilifu ili kuwasaidia wao kurejea kwake. Lehi anatukumbusha katika 2 Nefi, mlango wa 2 mstari wa 8, “ni muhimu sana kuwajulisha wakazi wa dunia kuhusu vitu hivi, ili wajue -au wakumbuke, hakuna binadamu anayeweza kuishi karibu na Mungu, bila fadhili, na rehema, na neema za Masiya Mtakatifu.”
Tunaweza kufanya nini? Tunapaswa kufanya nini? Ni rahisi: tunapaswa kuwasaidia marafiki zetu, wote waumini na wasio waumini, kufikia upendo wa Baba yao wa Mbinguni, kupitia upendo tunaowaonyesha.
Na kinyume na kile tunachofikiria wakati fulani, sio muda tunaotumia pamoja na mtu, bali udhati wa hisia zetu na roho ndani yetu, ambavyo huonyesha upendo wetu na kugusa moyo. Huduma ya Yesu ilikuwa kwa miaka 3 tu. Huo ni muda mfupi. Mimi pamoja na Dada Giraud-Carrier tunajua kitu kuhusu hilo! Hivyo, sio muda aliotumia pamoja na watu uliowaruhusu wao kuhisi upendo wake, bali ubora wa mchangamano wake pamoja nao kama vile:
-
Mwanamke mwenye ugonjwa wa damu (Luka 8:43–48)
-
Mwanamke aliyezini (Yohana 8:3–11).
-
Mwanamke wa Samaria kwenye kisima (Yohana 4:6–28)
Ndio, sisi sio Yesu, lakini tunaweza kufuata mfano Wake. Ndio, Moroni, mlango wa 7, mstari wa 48 hutufundisha kwamba upendo huu ni zawadi. “Kwa hivyo, ndugu zangu wapendwa, ombeni kwa Baba kwa nguvu zote za moyo, kwamba mjazwe na upendo huu, ambao ametoa kwa wote ambao ni wafuasi wa kweli wa Mwana wake, Yesu Kristo.” Kupitia sala na kujitahidi kuwa wanafunzi wema, tunaweza kujaribu kuhakikisha kwamba kila mchangamano tunaokuwa nao na marafiki wasio waumini, na watu tuliopangiwa kupitia kuwahudumia, na watu tunaokutana nao, ni wa dhati na huakisi upendo wa Mungu. Matendo kama neno la kutia moyo, huduma ndogo, kupiga simu, tabasamu, mwaliko wa kukaa karibu nasi Kanisani, jibu kwa jambo zito, n.k, huonyesha upendo wetu na kuakisi upendo wa Mungu.
Na muujiza katika haya yote ni kwamba si tu wengine watabarikiwa, bali kila mmoja wetu atabarikiwa pia. Ndio, Bwana anasema, katika mstari wa 75 wa Yakobo 5: “Na heri nyinyi; kwani kwa sababu mmekuwa na bidii katika kutumikia na mimi katika shamba langu la mizabibu, na mmetii amri zangu, na kuniletea tena matunda ya kawaida … , tazama mtapokea shangwe na mimi kwa sababu ya matunda ya shamba langu la mizabibu.”
Ninashangilia kutumikia pamoja nanyi katika sehemu hii ya shamba la mizabibu la Bwana katika kipindi hiki cha mwisho ambacho tunaweza kuwasaidia wengi wa akina kaka na dada zetu kuja kwa Kristo. Ninashuhudia kwamba Mungu ni Baba yetu wa Mbinguni, kwamba Yesu kristo ni Mwana Wake, Mwokozi na Mkombozi wetu, kwamba tu wa Kanisa Lake la kweli, na kwamba tunaongozwa na nabii Wake, Rais Nelson.