2025
Safari ya Imani: Njia ya Miaka 25 ya Familia ya Waji kwenda Hekaluni
Machi 2025


Kurasa za Karibu

Safari ya Imani: Njia ya Miaka 25 ya Familia ya Waji kwenda Hekaluni

Familia ya Waji, ikiongozwa na Waji Boru na mkewe, Zenbech, ina hadithi inayosisimua ya imani na uvumilivu ambayo imedumu kwa zaidi ya miaka 25. Kama wazazi wa watoto saba na bibi na babu wa wajukuu sita, ndoto yao ya muda mrefu ya kuingia hekaluni na kuunganishwa pamoja kama mume na mke ilikuwa uhalisia baada ya miaka ya changamoto na kuahirisha.

Safari yao kwenye injili ilianza wakati wa safari ya kikazi huko Addis Ababa, Ethiopia, ambapo walitambulishwa Kanisani na walijiunga na Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho. Wakati huo, hakukuwa na tawi la Kanisa katika mji wao wa Debra Zeit, na kuhudhuria kanisani kulihitaji safari ya kilomita 47 kila wiki kwenda Addis Ababa. Licha ya ugumu, familia ilifanya juhudi ya kusafiri kila wiki. Hatimaye, waliweza kuabudu karibu na nyumbani, wakikusanyika pamoja na waumini wengine ndani ya nyumba ya Rais Ayele Asfaw Kelkaye, Mtakatifu mwenzao wa Siku za Mwisho. Miaka ya mwanzo ya uongofu wao iliwekewa alama na kujitolea huku kwenye injili, lakini njia mara zote haikuwa rahisi.

Kwa kipindi cha miaka minane, familia ya Waji iliacha kushiriki kikamilifu Kanisani, ikikabiliwa na changamoto za kiroho na binafsi. Ilikuwa katika wakati huu ambapo Mzee na Dada Moyer, wamisionari waandamizi, walipozuru nyumbani kwao. Matembezi yale yalileta badiliko katika maisha yao. Ada Worq, mmoja wa mabinti wa Waji na Zenbech, anakumbuka umuhimu wa wasaa ule: “Kamwe sitasahau kile walichokisema wakati walipotutembelea. Waliuliza, ‘Ni kipi tunaweza kuwafanyia?’ na kisha walizungumza nasi kuhusu upendo wa Kristo na imani. Kila mmoja alikuwa akitokwa machozi, akiwa ameguswa na Roho.”

Matembezi haya yaliwasha mwendelezo wa imani ndani ya familia. Waliweka upya msimamo kwenye injili na walirejea kwenye kushiriki kikamilifu Kanisani. Hata hivyo, njia yao ya kwenda hekaluni bado ilibaki na changamoto. Kwa Waji na Zenbech, kuunganishwa hekaluni kwa muda na milele yote lilikuwa lengo lenye thamani, lakini safari yao ilikutana na vikwazo kadhaa. Safari zao zilizopangwa za hekaluni zilishindikana mara tatu. Licha ya juhudi zao zote, vikwazo visivyoonekana viliwazuia kufanya safari. Lakini kupitia imani na uungu kuingilia kati, safari yao hatimaye iliwezekana. Kwa usaidizi wa rais wa misioni, Rais Oliva Cowley na Dada Rebecca Cowley, walianza safari yao kuelekea Hekalu la Accra Ghana.

Mnamo Juni 17, baada ya miaka 25 ya uumini na kusubiri, Waji na Zenbech waliingia ndani ya hekalu na waliunganishwa pamoja. Siku hiyo ilikuwa wakati muhimu katika maisha yao, iliyojaa maana ya kina ya kiroho. Mekonnen, kijana wao mkubwa, alivuta taswira kwenye uzoefu huo: “Niliona ni jinsi gani watu wamebarikiwa kwa sababu ya kuwa na hekalu katika nchi yao.” Waji, akipata msukumo kutoka kwenye nguvu ya hekalu, alisema, “Hekalu ni kama dira—linatuelekeza njia ya uzima wa milele. Ni sala yangu kwamba kutakuwa na hekalu nchini Ethiopia siku moja.”

Dada Zenbech alishiriki hisia zake nyingi kutoka kwenye uzoefu wao hekaluni, akisema, "Niliuhisi upendo wa Baba wa Mbinguni na upendo wa watu wakati nilipokuwa ndani ya hekalu." Kwa wote wawili, Waji na Zenbech, kuunganishwa ndani ya hekalu haikuwa tu kilele cha miaka ya imani na dhabihu bali pia utimizwaji wa ahadi waliyoitamani kwa muda mrefu.

Kufuatia uunganishwaji wao, familia iliendelea kukua kiroho. Kujitolea kwao kulikofanywa upya kuliwaongoza kutumikia katika miito mbalimbali ndani ya Kanisa, wakijenga shuhuda zao na zaidi kuimarisha imani yao. Binti yao, Bemnet, akishawishiwa kwa uzoefu wa familia na imani yake mwenyewe, alianza kujitayarisha kutumikia misioni, akichangia kwenye urithi unaoendelea wa msimamo na huduma ndani ya familia ya Waji.

Safari ya familia ya Waji inakuwa kama ukumbusho wenye nguvu kwamba imani, subira na uvumilivu katika injili huleta baraka tele. Japokuwa Waji na Zenbech walikabiliwa na vikwazo vingi, ndoto yao ya kuunganishwa hekaluni ilikuwa uhalisia, ikionesha kwa mfano nguvu ya wakati wa Bwana. Hadithi yao inatoa tumaini kwa wale wote wanaojitahidi kwa ajili ya baraka za hekalu, ikionesha kwamba kupitia imani, chochote kinawezekana.