“Muujiza wa Biskuti,” Rafiki, Machi 2025, 30–31.
Waanzilishi katika Kila Nchi
Muujiza wa Biskuti
“Baba wa Mbinguni, hatuna chakula kwa ajili ya mlo wa jioni. Tafadhali tusaidie.”
Hadithi ya kweli kutoka Marekani.
Upepo wa baridi kali ulivuma, na theluji ikazunguka mkokoteni. Jane alivuta blanketi lake jembamba kuzunguka mabega yake. Miguu yake ilihisi ganzi, lakini aliendelea kutembea. Walikuwa njiani wakielekea Jijini Salt Lake, Utah.
Jane na familia yake walikuwa wamejifunza kuhusu Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho huko Uingereza. Wakati nabii alipowaomba waumini wa Kanisa kuja Utah, familia yake waliweka akiba kila pesa ambayo wangeweza kupata ili kufanya hii safari. Walisafiri kuvuka bahari. Sasa walikuwa wakisafiri kwa mikokoteni kuvuka nyanda. Walikuwa wametembea kwa miezi kadhaa, na walikuwa wakiishiwa chakula.
Machozi yalidondoka kwenye mashavu ya Jane. “Nina njaa sana,” alimwambia kaka yake mkubwa Thomas. “Sidhani kama naweza kutembea hatua nyingine!”
Thomas alikata kipande cha ngozi mbichi iliyolegea kutoka kwenye gurudumu la mkokoteni. “Chukua, tafuna hii, alisema. “Itakuwa SAWA.”
“Asante,” Jane alinong’ona alipokuwa akitafuna kipande kigumu cha ngozi.
Punde ikawa wakati wa kupiga kambi usiku. Baadhi ya wanaume waliondoka kwenda kuwinda nyati. Jane alitumaini wangepata kiasi. Tumbo lake lilikuwa tupu. Walipokuwa wakisubiri, Jane na familia yake walikumbatiana karibu na moto mdogo, wachovu, wenye njaa na wenye baridi.
“Acha tusali,” Jane alisema.
Familia ilipiga magoti pamoja, na Mama alisali. “Baba wa Mbinguni, hatuna chakula kwa ajili ya mlo wa jioni. Tafadhali tusaidie.”
Jane na kaka zake na dada zake walikaa kimya kwa muda. Kisha Mama akaketi wima.
“Kuna nini?” Thomas aliuliza.
“Nimekumbuka tu kitu fulani.” Mama aliharakisha hadi kwenye mkokoteni na kufungua sanduku la familia. Kisha akatoa kisanduku kidogo cha chuma na kukifungua. Ndani kulikuwa na biskuti mbili ngumu sana. Zilikuwa mabaki kutoka safari yao ya baharini miezi kadhaa kabla.
Jane alihisi kiputo cha msisimko ndani yake. Hatimaye walikuwa na chakula! “Tunaweza kuzivunja katika vipande vidogo vidogo vya kushiriki,” alisema.
Lakini walipojaribu, biskuti zilikuwa ngumu sana kuvunja hata nusu yake tu.
“Acha tujaribu hili,” Mama alisema. Aliweka biskuti katika tanuru ya Uholanzi na kumwaga maji kidogo juu yake. Kisha akaweka kifuniko na kuweka chungu kizito juu ya makaa ya mawe.
Jane na familia yake waliomba tena. Alifikiria hadithi ya Yesu Kristo katika maandiko, wakati alipowalisha watu elfu tano kwa mikate na samaki wachache tu. Alijua Baba wa Mbinguni angeweza kuwasaidia pia.
Baada ya muda mfupi, Mama pole pole alifungua chungu. Killikuwa kimejaa kabisa kwa chakula! Kulikuwa kingi cha kulisha familia yao yote.
Jane alimkumbatia mama yake kwa nguvu. “Ni muujiza.”
Vielelezo na Simini Blocker