Angazio la Kitabu cha Maelezo
Mpango wa Mungu wa Furaha
Baba wa Mbinguni alitoa mpango wa furaha ili kutuwezesha sisi kufurahia baraka zake zote. Kazi yake na utukufu wake ni “kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39). Kutokufa ni kuishi milele kwenye mwili wa nyama na mifupa uliofufuka. Uzima wa milele, au kuinuliwa, ni kuwa kama Mungu na kuishi kwenye uwepo Wake milele kama familia.
Kazi ya Mungu na Utukufu Wake
“Kwa maana tazama, hii ndiyo kazi yangu na utukufu wangu—kuleta kutokufa na uzima wa milele wa mwanadamu” (Musa 1:39).
Yesu Kristo yu katikati ya mpango wa Mungu. Kwa sababu ya upendo usio na kikomo wa Baba wa Mbinguni kwetu, Alimtuma Mwanawe kutukomboa kutoka kwenye dhambi na kifo kupitia dhabihu Yake ya upatanisho (ona Yohana 3:16). Kupitia upatanisho Wake, Yesu Kristo hutoa hakikisho kwamba kila mmoja wetu aliyezaliwa duniani atafufuliwa na kupata mwili usiokufa.
Ili kupokea uzima wa milele, lazima “twende kwa Kristo” (Moroni 10:32). Upatanisho wa Mwokozi hufanya iwezekane kusafishwa kutokana na dhambi na kuwa na mioyo yetu ikiwa imebadilishwa ili kwamba tuweze kupokea uzima wa milele na utimilifu wa shangwe. Baba wa Mbinguni hutaka wote wa watoto Wake kuchagua kurudi Kwake.