“Baraka za Urejesho,” Liahona, Jan. 2025.
Njoo, Unifuate
Mafundisho na Maagano 1; Joseph Smith—Historia ya 1:1–26
Baraka za Urejesho
Injili ya urejesho ya Yesu Kristo imenibariki mimi na familia yangu, na itaendelea mbele kubariki ulimwengu wote.
Picha ya chumba cha kuunganisha katika Hekalu la Suva Fiji
Katika majira ya kuchipua ya mwaka 1820, mvulana wa miaka 14 anayehitaji majibu aliingia katika kijisitu cha miti. Alitamani kujua ni lipi kati ya makanisa mengi yaliyomzunguka anapaswa kujiunga nalo. Baada ya kujifunza katika maandiko kwamba “lakini mtu wa kwenu akipungukiwa na hekima, na aombe dua kwa Mungu” (Yakobo 1:5), mvulana alienda kwenye kijisitu na kufungua moyo wake kwa Mungu. Alipokuwa akisali, mbingu zilifunguka.
Mungu Baba na Mwanawe, Yesu Kristo, walimtokea Joseph Smith na kujibu sala yake (ona Joseph Smith—Historia 1:16–20). Hili tukio takatifu lilianzisha Urejesho wa utimilifu wa injili ya Yesu Kristo isiyo na mwisho. Ufahamu huu umebariki sana maisha yangu, lakini ulinichukua muda kupata ushuhuda mimi mwenyewe.
Yesu Kristo Alirejesha Kanisa Lake
Miaka kadhaa iliyopita, nilihisi sana kama Joseph mdogo. Nilichanganyikiwa na “vita vya maneno na misukosuko ya maoni” (Joseph Smith—Historia ya 1:10) kutoka makanisa mengi tofauti huko Fiji. Nilipokutana na wamisionari kwa mara ya kwanza, nilikuwa na maswali mengi sana. Wengine wamenitania kwamba mimi ni mwanafunzi nisiyeelewa haraka kwa sababu nilitumia miaka minane kuchunguza Kanisa. Uongofu wangu ulianza kupitia kuelewa jina la Kanisa.
Wakati wa huduma Yake duniani, Yesu Kristo alianzisha Kanisa Lake. Baada ya muda, mafundisho na mamlaka ya ukuhani ya Kanisa Lake yakapotea. Katika siku yetu, Yesu Kristo alirejesha kupitia Nabii Joseph Smith kanisa lile lile aliloanzisha wakati alipoishi duniani (ona Makala ya Imani 1:6). Ilikuwa ni Mwokozi Mwenyewe aliyesema, “Kwani ndivyo kanisa langu litakavyoitwa katika siku za mwisho, hata Kanisa la Yesu Kristo la Watakatifu wa Siku za Mwisho” (Mafundisho na Maagano 115:4).
Kanisa lina jina la Yesu Kristo kwa sababu ni Kanisa Lake! Baada ya miaka minane, ukweli huu ulijirudia tena akilini na moyoni mwangu. Nilibatizwa katika umri wa miaka 27 na punde nikaitwa kama mshauri katika urais wa Wavulana wa kata na mwalimu wa seminari ya asubuhi mapema. Njiani, ushuhuda wangu uliendelea kukua.
Urejesho Unaendelea
Maisha yangu yalibadilika nilipofundisha seminari, nilihudhuria mkutano wa sakramenti, na kusikiliza mkutano mkuu. Pia nilihisi ushawishi wa kutuliza, wa kufariji, na wenye mwongozo wa kiungu wa Roho niliposoma Kitabu cha Mormoni—ushahidi halisi na onyesho la Urejesho na wito wa kinabii wa Joseph Smith.
Wakati Bwana alipomwita Joseph “na kumwambia kutoka mbinguni, na akampa amri” (Mafundisho na Maagano 1:17), Yeye alionyesha kwamba Yeye “huwavutia watu na kuwaita kwenye kazi yake takatifu katika kipindi hiki na kizazi hiki, vile vile katika vizazi vya kale” na kwamba “yeye ni Mungu yule yule jana, leo, na milele” (Mafundisho na Maagano 20:11–12).
Urejesho ambao ulianza na Joseph unaendelea leo. Kama Watakatifu wa Siku za Mwisho, tumeitwa kuzungumza katika jina la Mwokozi ili “kwamba imani hiyo … iweze kuongezeka duniani,” “agano Lake lisilo na mwisho lingeweza kuanzishwa,” na “utimilifu wa injili [Yake] ungeweza kutangazwa na wadhaifu na rahisi hata mwisho wa ulimwengu” (Mafundisho na Maagano 1:21–23). Tumebarikiwa kuwa na uwezo wa kusaidia kujenga Kanisa na kuandaa ulimwengu kwa ajili ya siku hiyo wakati Yesu Kristo atakaporudi.
Mzee na Dada Wakolo (mbali kulia) walipokea endaumenti na kuunganishwa katika Hekalu la Nuku’alofa Tonga mnamo Agosti 1995, mwaka mmoja baada ya Mzee Wakolo kujiunga na Kanisa. Wanaonyeshwa hapa pamoja na urais wa hekalu.
Shukrani kwa Nabii Joseph
Mwaka mmoja baada ya ubatizo wangu, mke wangu, Anita, na mimi tulisafiri kwenda Hekalu la Nuku’alofa Tonga kuunganishwa kwa muda na milele yote. Ushuhuda wangu wa Urejesho ulifanya kwenda hekaluni kuwa wa maana sana. Injili ya urejesho ya Yesu Kristo kwa kweli inamaanisha kila kitu! Moyo wangu umejawa na shukrani kwa ajili ya baraka ambazo umezileta kwangu na kwa familia yangu.
Baraka hizi za thamani zimekuja ulimwenguni kupitia “Joseph Smith, nabii na mwonaji wa Bwana, amefanya mengi, isipokuwa Yesu peke yake, kwa ajili ya wokovu wa wanadamu katika ulimwengu huu, kuliko mwanadamu mwingine yeyote aliyeishi ndani yake” (Mafundisho na Maagano 135:3). Lazima daima tuwe na shukrani kwa ajili ya—na kamwe tusipotee kuona—kile tulichopewa kupitia nabii wa kipindi hiki cha mwisho cha maongozi ya Mungu.
Kupitia Joseph, tunaelewa uhusiano wetu wa agano na Baba wa Mbinguni na Yesu Kristo. Tuna ukuhani na ibada na maagano yaliyorejeshwa. Katika uzoefu wa Joseph katika Kijisitu Kitakatifu, tunajifunza kwamba hata kabla ya Baba kumtambulisha Mwanawe, Yesu Kristo, Yeye alimwita Joseph kwa jina (ona Joseph Smith—Historia 1:17). Yeye pia anatujua sisi kwa jina. Na kama vile alivyofungua mbingu na kujibu sala rahisi, ya dhati ya mvulana wa miaka 14, Yeye pia atajibu maombi yetu kwa mapenzi Yake mwenyewe, njia, na wakati wake, bila kujali umri wetu. Kweli hizi zinavuma ndani ya nafsi yangu. Ninashuhudia kwamba ni kweli.
Natumaini kwamba mimi ni mtu ambaye nafanya mema ulimwenguni. Ikiwa ni hivyo, basi Joseph Smith amefanya mengi ya kuchangia. Maisha yangu yasingekuwa yalivyo leo, nisingekuwa mume na baba kama nilivyo, na nisingekuwa na furaha kama nilivyo bila injili ya urejesho kwamba Nabii Joseph alijitolea maisha yake kuileta ulimwenguni. Injili inanipa mng’aro na tumaini. Kwa hili, daima nitakuwa na shukrani kwa Nabii Joseph.
Wakati Wowote, Popote
Ninabeba nakala ya Kitabu cha Mormoni popote ninapoenda, nikitumaini ninaweza kumpa mtu fulani na kuwatambulisha kwenye injili ya urejesho ya Yesu Kristo. Nimetoa mamia ya nakala ulimwenguni kote. Ninapenda kushiriki ujumbe wa Urejesho—wakati wowote, mahali popote.
Hii imekuwa kweli hasa wakati wa kufundisha na kushuhudia kwa watoto wangu pamoja na Anita ndani ya kuta za nyumba yetu. Binti yetu kwa sasa anatumikia misheni huko New York City, Marekani. Tumemwambia, “Nenda ukamshuhudie Mwokozi upande wako wa ulimwengu. Mama na Baba yako watafanya vivyo hivyo katika sehemu yetu ya ulimwengu.” Tunapenda kujuliana hali juu ya huduma yetu. Na sasa, tuna binti mjukuu mwenye umri wa miaka minne. Tumaini na matamanio ya moyo wangu ni kwamba mara nyingi atasikia na daima kumkumbuka Babu yake akishuhudia juu ya Mwokozi na injili Yake.
Sote tunaweza kushuhudia baraka za injili ya urejesho—wakati wowote, mahali popote—tunapoishi maisha ya mfano wa mwanafunzi wa Yesu Kristo. Tunaweza kushiriki Kitabu cha Mormoni: Ushuhuda Mwingine wa Yesu Kristo. Na tunaweza kushuhudia kwamba Yesu Kristo amerejesha utimilifu wa injili Yake na kuongoza Kanisa leo. Rais Russell M. Nelson alifundisha kwamba “ufunuo unaendelea kutiririka kutoka kwa Bwana wakati wa mchakato endelevu wa urejesho.” Ninashuhudia kwamba hii inaendelea kupitia mstari usiovunjika wa funguo za ukuhani zilizoshikiliwa na manabii, waonaji, na wafunuzi ambao hutuvuvia, hutuongoza na kutusaidia kujifunga wenyewe kwa Mwokozi Yesu Kristo.
Huu ni ushahidi na ushuhuda wangu. Kwa furaha nitaushiriki daima na kamwe nisiwe na shaka.